Wednesday, June 11, 2014

TAARIFA KUHUSU MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2014

Kaimu Katibu Mkuu Utumishi Bw.HAB Mkwizu akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2014 katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO mapema leo.Wengine ni Mkurugenzi Idara ya Habari MAELEZO Bw.Assah Mwambene (kulia kwake), Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Bi.Roxana Kijazi (kushoto kwake) na Mkurugenzi Msaidizi Bw. Hassan Kitenge (wa kwanza kulia).



Baadhi ya waandishi wa habari (kushoto) wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Utumishi Bw.HAB Mkwizu (wa pili kutoka kulia) kwenye mkutano uliofanyika Idara ya Habari Maelezo mapema leo. 
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS

Simu ya Upepo "UTUMISHI", DSM.                                    Menejimenti ya Utumishi wa Umma,  Simu: 2118531/4 au 2122908                                Utumishi House
Barua Pepe: permsec@estabs.go.tz                                 8 Barabara ya Kivukoni
                   Tovuti: www.utumishi.go.tz                                              11404 Dar es Salaam

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
          
Kama mnavyofahamu Siku ya Utumishi wa Umma huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kila tarehe 23 Juni ya kila mwaka kwa lengo la kutathimini kazi zinazofanywa na sekta ya Utumishi wa Umma katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hapa nchini maadhimisho haya huratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Siku ya Utumishi wa Umma itatanguliwa na maonesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za Umma katika kiwanja cha Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu ni:

“Mkataba wa Misingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi”.

Kama sehemu ya maadhimisho hayo, yatafanyika mambo yafuatayo;

·      Kongamano la Miaka 50 ya Muungano katika Utumishi wa Umma Nchini.  Kongamano hili litasimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi Ombeni Sefue na litanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere, jijini Dar es salaam tarehe        19-20 Juni, 2014.

·      Maonesho ya wiki moja ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za Serikali. Maonesho hayo yatakayoshirikisha zaidi ya Taasisi 30 za Serikali hapa nchini  yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma tarehe 16 Juni, 2014.
·      Huduma Mbalimbali zitatolewa ikiwa ni pamoja na upimaji wa afya na ushauri kuhusu saratani ya kizazi, magonjwa sugu yasiyoambukiza, kutoa vyeti vya kuzaliwa, kutoa vyeti vya Bima ya afya, kuelekeza namna ya kujua kusoma upimaji wa magari katika mizani, kutoa elimu kuhusu matumizi ya vifaa vya TEHAMA na kuepuka utapeli unaotokea katika mitandao na ushauri kuhusu masuala mbalimbali.

·      Kilele cha maonesho na Siku ya Utumishi wa Umma itakua Tarehe 23, Juni, 2014 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Taasisi zilizoonyesha ubunifu katika utoaji huduma na kupunguza urasimu, kutatua kero za wateja na wadau wengine kwa uikamilifu zitapewa tuzo ili kutambua juhudi zilizofanyika kuwahudumia Watanzania. Ieleweke wananchi ndio wadau wakuu wa Serikali.

Uamuzi wa kuwa na Siku ya Utumishi wa Umma ulifikiwa na Mawaziri wa Utumishi wa Umma wa nchi za Afrika waliokutana katika Mji wa Tangiers Morocco Mwaka 1994. Siku hiyo imekuwa inaadhimishwa katika ngazi ya Bara katika mojawapo ya nchi za Afrika mara moja katika kipindi cha miaka miwili.
          
Wananchi wanakaribishwa kufika kwa wingi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 16  hadi 23 Juni, 2014 ili kutoa maoni kuhusu huduma zinazotolewa na vyombo mbalimbali vya Serikali, kupata huduma moja kwa moja kutoka kwa baadhi ya Taasisi na kuelimishwa kuhusu huduma mpya na zile ambazo zimefanyiwa maboresho ili kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.
  
Imetolewa Na:

Kaimu Katibu Mkuu,

Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
DAR ES SALAAM,



No comments:

Post a Comment