Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini wakifuatilia mada mjini Dodoma leo.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini imepanga kuwachukulia hatua waajiri wote nchini kwa kushindwa
kuwasilisha taarifa za wahitimu wa
elimu ya juu wanaodaiwa na Bodi hiyo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Bw. Robert Kibona alipokuwa akitoa mada
kuhusu urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa
Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini mjini Dodoma leo.
“Mpaka sasa tumewachukulia hatua jumla ya waajiri watano ambao
wameshindwa kuwasilisha taarifa za watumishi wao wanaodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu” alisema
Bw.Robert.
Alisema, mwajiri atakayeshindwa kutoa taarifa za wahitimu wa elimu ya
juu katika Bodi kwa wakati atatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni saba au
kutumikia kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Aidha,Bw. Robert alisema kuwa mpaka sasa takribani waajiriwa 18
wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Bw.Robert alifafanua kuwa ili kufanikisha zoezi la urejeshaji mikopo kutoka kwa wadaiwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inatunga
sheria na mifumo mbalimbali ya
kuwadhibiti wadaiwa hao.
“Tunatengeneza sheria ambazo zitawazuia wadaiwa wa mikopo ya elimu ya
juu kupata hati ya kusafiria nje ya nchi au kibali cha kusafiri hadi
atakapowasiliana na Bodi.”
Pia,alisema mhitimu atakayeshindwa kulipa mkopo taarifa zake
zitatangazwa kwenye vyombo vya habari na kwenye taasisi za mikopo ili asipate
huduma yoyote ya kifedha.
Naye, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Dk.
Veronica Nyahende amewataka wahitimu wa elimu ya juu nchini kutumia elimu
waliyonayo kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.
Alisema changamoto ya kurejesha mikopo ni kubwa kwa upande wa wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana
kazi ama hawajajiajiri.
“Changamoto iliyopo ni wahitimu kushindwa kulipa mikopo hiyo kutokana na
kuwa na kipato cha chini ama kukosa ajira.”
Alisema Bodi imeingia mkataba na kampuni zitakazokusanya mikopo kwa walionufaika
na mikopo hiyo na kushindwa kuilipa .
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iko katika mchakato wa kuelimisha umma na
watendaji wakuu Serikalini ili kuhakikisha wanawasilisha taarifa za watumishi
wao wanaodaiwa mikopo hiyo.
|