Tuesday, August 10, 2021

UTUMISHI YAMKABIDHI MKANDARASI KIWANJA KUANZA UJENZI WA JENGO KUBWA LA OFISI KWENYE MJI WA SERIKALI

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 10 Agosti, 2021 

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.  Francis Michael amekabidhi kiwanja kwa Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi Watumishi Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma litakaloongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa umma.

Akikabidhi eneo hilo kwa Mkandarasi, Dkt. Michael amesema, ofisi yake imepewa eneo jingine kubwa zaidi ya lile la awali ili kuwezesha ujenzi wa jengo la ghorofa sita lenye uwezo wa kutumiwa na watumishi 380 kutoa huduma kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo, Dkt. Michael amesema kuwa, anatarajia Mkandarasi ataanza ujenzi mapema iwezekanavyo kwa kasi na kiwango kinachotakiwa ili kukamilisha ujenzi kwa wakati kama mkataba unavyojiainisha.

“Tunatambua kwenye taratibu za uhandisi huwa kuna hatua zinazozingatiwa, hivyo naamini taratibu hizo zitazingatiwa ipasavyo, msiharakishe kumaliza ujenzi halafu jengo likawa na mapungufu”, Dkt. Michael amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu Majengo wa WHC amemshukuru Dkt. Francis Michael kwa kuwakabidhi eneo kwa ajili ya kuanza usimamizi rasmi wa ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali, na kuongeza kuwa watahakikisha jengo linajengwa kwa kiwango na linakamilika kwa wakati.

Jengo hilo kubwa la ghorofa sita la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora linaloanza kujengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 7912 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 hadi 24.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.  Francis Michael akikabidhi kiwanja kwa mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi Watumishi Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. 

Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu Majengo wa WHC akimuahidi Dkt. Francis Michael usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.


Baadhi ya Wataalam wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Watumishi Housing Company (WHC) wakiwa katikati ya eneo la kiwanja walichokabidhiwa kujenga Jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Cosmas Ngangaji akihimiza ufanisi wa utendaji kazi kwa Mkandarasi (TBA) na mshauri Mwelekezi (WHC) waliopewa dhamana ya ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.





 






Thursday, August 5, 2021

MHE. NDEJEMBI AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUSHIRIKIANA KIUTENDAJI ILI KUEPUKA MIGOGORO

Na. James K. Mwanamyoto-Mpanda

Tarehe 5 Agosti, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amezitaka Taasisi zote zote za Umma nchini kuwa na utamaduni wa  kushirikiana na kupeana mrejesho wa utendaji kazi, ili kuepuka migogoro ya kiutendaji baina yao kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya utendaji kazi wa Taasisi za Serikali kwa Umma.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa Taasisi za Umma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Umma mkoani Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amesema, ni jambo la kushangaza pale kiongozi anapokwenda kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Serikali katika eneo lake la utawala na kubaini baadhi ya taasisi kutoshirikiana kiutendaji na badala yake zinatupiana lawama.

“Inakuwaje Watumishi wanaohusika na masuala ya ardhi wanakwenda kubomoa nyumba inayodaiwa kujengwa kinyume na utaratibu, wakati nyumba hiyo imepewa huduma ya maji na umeme na Taasisi nyingine za Serikali”, Mhe. Ndejembi amefafanua.

Ameongeza kuwa, mgogoro kama huo unatokana na baadhi ya Taasisi za Umma kutoshirikiana na kutopeana mrejesho kiutendaji.

Pia, Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Taasisi za Umma zinategemeana kiutendaji hivyo zinapaswa kujenga utamaduni wa kupeana mrejesho ili kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau.

Pamoja na kusisitiza taasisi za umma kushirikiana, Mhe. Ndejembi amehimiza  ushirikiano wa kiutendaji ndani ya Taasisi za Umma  na kuhoji kwanini kuwe na kazi inafanywa na taasisi mojawapo ya Serikali ndani ya Sekretarieti ya Mkoa lakini Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) hajapewa taarifa, hivyo amezitaka taasisi za umma kuacha kufanya kazi kimazoea.

“Ni mara nyingi mambo yanaendelea ndani ya taasisi hususani yenye maslahi wakati viongozi wa juu wa taasisi hiyo hawana taarifa yoyote, lakini jambo likiharibika wao ndio wanawajibika kutoa taarifa Serikalini”, Mhe. Ndejembi amefafanua.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Bi. Catherine Mashalla amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji na kutoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa ni dira ya utendaji kazi unazingatia weledi kwa watumishi wote mkoani humo.

Bi. Mashalla amemuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, yeye na viongozi wenzie watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ili wananchi wapate huduma bora.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Mkoani Katavi yenye lengo la kukutana na Watumishi wa Umma ili kusikiliza kero, changamoto zinazowakabili na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao mkoani humo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Katavi wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

 

Baadhi ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.


Mmoja wa Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Bi. Mercy Salimu akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Naibu Waziri huyo na watumishi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za Watumishi wa Umma mkoani Katavi wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Catherine Mashalla akitoa shukrani kwa Mhe. Ndejembi kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi mara baada ya Naibu waziri huyo kuzungumza na Watumishi wa Umma mkoani humo.


 

Wednesday, August 4, 2021

MHE. NDEJEMBI AELEKEZA TAKUKURU MKOANI KATAVI KUCHUNGUZA MATUMIZI YA FEDHA ZA TASAF ZILIZOTOLEWA KUJENGA KARAKANA YA WENYE MAHITAJI MAALUM


Na. James K. Mwanamyoto-Mpanda

Tarehe 4 Agosti, 2021 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi wa jengo la karakana ya wenye mahitaji maalum mkoani Katavi ambalo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulitoa fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi huo ambao haujakamilika mpaka sasa.

Akizungumza na Viongozi wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi ambao ndio waasisi wa mradi huo, Mhe. Ndejembi amesema TASAF ilitoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wenye ulemavu mkoani Katavi kujenga karakana hiyo ili waweze kufanya shughuli zao kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Mhe. Ndejembi amesema watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii, na licha ya kuwa na ulemavu wameonyesha dhamira ya kujishughulisha na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kuungwa mkono na Serikali na jamii kwa ujumla.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, chama hicho cha walemavu kilikuja na wazo la kuanzisha mradi huo ili wajishughulishe na ushonaji na kuwa na ofisi ya kikundi ambayo itaratibu ushiriki wao katika uzalishaji kwa manufaa ya taifa, hivyo atakaa na uongozi wa TASAF ili kuangalia namna ya kuwezesha ukamilishaji wa ujenzi huo baada ya uchuguzi wa TAKUKURU kukamilika.

Mhe. Ndejembi amesisitiza umuhimu wa TAKUKURU kukamilisha uchunguzi kabla ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo, lengo likiwa ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa awali pamoja na kulinda hadhi ya Mwenge wa Uhuru ambao Kiongozi wake aliweka jiwe la msingi tarehe 20 Septemba, 2012.

Aidha, Mhe. Ndejembi amezungumzia hoja ya mgogoro wa kiwanja uliowasilishwa na Viongozi wa Chama Cha Walemavu waliodai kiwanja chao kuvamiwa na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph kujiridhisha na mmiliki halali wa kiwanja hicho ili fedha zikipatikana ujenzi uanze mara moja badala ya kuanza kutatua mgogoro.

Naye Katibu wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi, Bw. Godfrey Sadala amesema lengo la kujenga karakana hiyo ni kutoa fursa kwa walemavu wengine mkoani humo ili wapate eneo la kujifunza na kuondokana na dhana potofu kuwa mtu akiwa mlemavu hawezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bw. Joshua Sankala amesema mradi huo uliibuliwa kipindi cha pili cha TASAF ili kusaidia watu wenye ulemavu kufanya shughuli zao zitakazowakwamua kiuchumi.

Katika hatua nyingine Mhe. Ndejembi amewasisitiza walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao.

Mhe. Ndejembi amesema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini ulianzishwa na Serikali kwa lengo kuboresha maisha ya kaya maskini, ndio maana katika Kijiji cha Kawanzige pekee kiasi cha shilingi milioni 118 zimetolewa kwa walengwa badala ya kupelekwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu zoezi la uandikishaji kwa wale ambao hawajaandikishwa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu amesema kipaumbele cha uandikishaji kilitolewa kwenye vijiji ambavyo havikuwahi kuandikishwa kabisa.

Ameongeza kuwa, zoezi la uandikishaji litaendelea kuanzia tarehe 10 mwezi huu, hivyo amewataka ambao hawajaandikishwa kuvuta subira mpaka zoezi hilo litakapoanza.

Mhe. Ndejembi amewatembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku wanayoipokea kutoka TASAF ili waweze kuboresha maisha yao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi, Bw. Dominick Pesambili akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa karakana ya watu wenye ulemavu mkoani Katavi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.


Mwonekano wa jengo la karakana ya watu wenye ulemavu mkoani Katavi ambalo TASAF ilitoa fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wake.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.



Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akitoa ufafanuzi kuhusu uandikishwaji wa walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.

Mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bw. Shija Shimela akitoa ushuhuda wa namna Mpango huo ulivyosaidia kuboresha maisha yake. 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bibi Zena Kangamili wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.