Na. James K. Mwanamyoto-Mpanda
Tarehe 5 Agosti, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amezitaka Taasisi zote zote za Umma nchini kuwa na utamaduni wa kushirikiana na kupeana mrejesho wa utendaji
kazi, ili kuepuka migogoro ya kiutendaji baina yao kwa lengo la kujenga taswira
nzuri ya utendaji kazi wa Taasisi za Serikali kwa Umma.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa
Taasisi za Umma wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Umma mkoani Katavi
kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani humo.
Mhe. Ndejembi amesema, ni jambo la
kushangaza pale kiongozi anapokwenda kukagua utekelezaji wa majukumu ya Taasisi
za Serikali katika eneo lake la utawala na kubaini baadhi ya taasisi
kutoshirikiana kiutendaji na badala yake zinatupiana lawama.
“Inakuwaje Watumishi wanaohusika na
masuala ya ardhi wanakwenda kubomoa nyumba inayodaiwa kujengwa kinyume na
utaratibu, wakati nyumba hiyo imepewa huduma ya maji na umeme na Taasisi
nyingine za Serikali”, Mhe. Ndejembi amefafanua.
Ameongeza kuwa, mgogoro kama huo
unatokana na baadhi ya Taasisi za Umma kutoshirikiana na kutopeana mrejesho
kiutendaji.
Pia, Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa
Taasisi za Umma zinategemeana kiutendaji hivyo zinapaswa kujenga utamaduni wa
kupeana mrejesho ili kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau.
Pamoja na kusisitiza taasisi za umma
kushirikiana, Mhe. Ndejembi amehimiza
ushirikiano wa kiutendaji ndani ya Taasisi za Umma na kuhoji kwanini kuwe na kazi inafanywa na
taasisi mojawapo ya Serikali ndani ya Sekretarieti ya Mkoa lakini Katibu Tawala
wa Mkoa (RAS) hajapewa taarifa, hivyo amezitaka taasisi za umma kuacha kufanya
kazi kimazoea.
“Ni mara nyingi mambo yanaendelea
ndani ya taasisi hususani yenye maslahi wakati viongozi wa juu wa taasisi hiyo
hawana taarifa yoyote, lakini jambo likiharibika wao ndio wanawajibika kutoa
taarifa Serikalini”, Mhe. Ndejembi amefafanua.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi
wa Umma Mkoani Katavi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe
Bi. Catherine Mashalla amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji na
kutoa maelekezo ambayo anaamini yatakuwa ni dira ya utendaji kazi unazingatia
weledi kwa watumishi wote mkoani humo.
Bi. Mashalla amemuahidi Mhe.
Ndejembi kuwa, yeye na viongozi wenzie watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa
maelekezo aliyoyatoa ili wananchi wapate huduma bora.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya
kikazi Mkoani Katavi yenye lengo la kukutana na Watumishi wa Umma ili
kusikiliza kero, changamoto zinazowakabili na kuzitatua ikiwa ni pamoja na
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao mkoani humo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Katavi
wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika
katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Baadhi ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika
katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Mmoja wa Watumishi wa Umma Mkoani Katavi, Bi. Mercy Salimu akiwasilisha
changamoto yake ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani)
wakati wa kikao kazi Naibu Waziri huyo na watumishi hao kilichofanyika katika
Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za Watumishi wa Umma mkoani Katavi
wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao (hawapo pichani) kilichofanyika
katika Ukumbi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Catherine
Mashalla akitoa shukrani kwa Mhe. Ndejembi kwa niaba ya Watumishi wa Umma Mkoani Katavi mara baada ya
Naibu waziri huyo kuzungumza na Watumishi wa Umma mkoani humo.
No comments:
Post a Comment