Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 10 Agosti, 2021
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Dkt. Francis Michael amekabidhi kiwanja
kwa Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi
Watumishi Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya
Jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma litakaloongeza ufanisi wa utoaji wa
huduma kwa umma.
Akikabidhi eneo hilo kwa Mkandarasi, Dkt. Michael amesema, ofisi yake
imepewa eneo jingine kubwa zaidi ya lile la awali ili kuwezesha ujenzi wa jengo
la ghorofa sita lenye uwezo wa kutumiwa na watumishi 380 kutoa huduma kwa
wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo, Dkt. Michael amesema kuwa, anatarajia
Mkandarasi ataanza ujenzi mapema iwezekanavyo kwa kasi na kiwango kinachotakiwa
ili kukamilisha ujenzi kwa wakati kama mkataba unavyojiainisha.
“Tunatambua kwenye taratibu za uhandisi huwa kuna hatua zinazozingatiwa,
hivyo naamini taratibu hizo zitazingatiwa ipasavyo, msiharakishe kumaliza
ujenzi halafu jengo likawa na mapungufu”, Dkt. Michael amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu
Majengo wa WHC amemshukuru Dkt. Francis Michael kwa kuwakabidhi eneo kwa ajili
ya kuanza usimamizi rasmi wa ujenzi wa jengo kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI
kwenye Mji wa Serikali, na kuongeza kuwa watahakikisha jengo linajengwa kwa
kiwango na linakamilika kwa wakati.
Jengo hilo kubwa la ghorofa sita la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora linaloanza kujengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba
jijini Dodoma litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 7912 na linatarajiwa
kukamilika ndani ya miezi 18 hadi 24.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Dkt. Francis Michael akikabidhi kiwanja
kwa mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Mshauri Mwelekezi Watumishi
Housing Company (WHC) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Awamu ya Pili ya Jengo
kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi, Bw. Peter Mmalavi Msanifu Majengo wa WHC
akimuahidi Dkt. Francis Michael usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo kubwa la
Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.
Baadhi ya Wataalam wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Watumishi Housing
Company (WHC) wakiwa katikati ya eneo la kiwanja walichokabidhiwa kujenga Jengo
kubwa la Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma Bw. Cosmas Ngangaji akihimiza ufanisi wa utendaji kazi kwa Mkandarasi
(TBA) na mshauri Mwelekezi (WHC) waliopewa dhamana ya ujenzi wa jengo kubwa la
Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenye Mji wa Serikali.
No comments:
Post a Comment