Na.
James K. Mwanamyoto-Mpanda
Tarehe
4 Agosti, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa
wa Katavi kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi wa jengo la karakana ya wenye
mahitaji maalum mkoani Katavi ambalo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulitoa
fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi huo ambao haujakamilika mpaka sasa.
Akizungumza na Viongozi wa
Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi ambao ndio waasisi wa
mradi huo, Mhe. Ndejembi amesema TASAF ilitoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wenye
ulemavu mkoani Katavi kujenga karakana hiyo ili waweze kufanya shughuli zao kwa
lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Mhe. Ndejembi amesema watu
wenye ulemavu ni sehemu ya jamii, na licha ya kuwa na ulemavu wameonyesha
dhamira ya kujishughulisha na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa, hivyo
wanapaswa kuungwa mkono na Serikali na jamii kwa ujumla.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa,
chama hicho cha walemavu kilikuja na wazo la kuanzisha mradi huo ili wajishughulishe
na ushonaji na kuwa na ofisi ya kikundi ambayo itaratibu ushiriki wao katika
uzalishaji kwa manufaa ya taifa, hivyo atakaa na uongozi wa TASAF ili kuangalia
namna ya kuwezesha ukamilishaji wa ujenzi huo baada ya uchuguzi wa TAKUKURU
kukamilika.
Mhe. Ndejembi amesisitiza
umuhimu wa TAKUKURU kukamilisha uchunguzi kabla ya kuendelea na ujenzi wa mradi
huo, lengo likiwa ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa awali
pamoja na kulinda hadhi ya Mwenge wa Uhuru ambao Kiongozi wake aliweka jiwe la
msingi tarehe 20 Septemba, 2012.
Aidha, Mhe. Ndejembi amezungumzia
hoja ya mgogoro wa kiwanja uliowasilishwa na Viongozi wa Chama Cha Walemavu
waliodai kiwanja chao kuvamiwa na kumuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe.
Jamila Yusuph kujiridhisha na mmiliki halali wa kiwanja hicho ili fedha
zikipatikana ujenzi uanze mara moja badala ya kuanza kutatua mgogoro.
Naye Katibu wa Chama cha
Walemavu Mkoa wa Katavi, Bw. Godfrey Sadala amesema lengo la kujenga karakana
hiyo ni kutoa fursa kwa walemavu wengine mkoani humo ili wapate eneo la
kujifunza na kuondokana na dhana potofu kuwa mtu akiwa mlemavu hawezi kufanya
shughuli yoyote ya maendeleo.
Kwa upande wake Mratibu wa
TASAF Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bw. Joshua Sankala amesema mradi huo
uliibuliwa kipindi cha pili cha TASAF ili kusaidia watu wenye ulemavu kufanya
shughuli zao zitakazowakwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine Mhe.
Ndejembi amewasisitiza walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutumia ruzuku
wanayoipata kuboresha maisha yao.
Mhe. Ndejembi amesema Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini nchini ulianzishwa na Serikali kwa lengo kuboresha
maisha ya kaya maskini, ndio maana katika Kijiji cha Kawanzige pekee kiasi cha
shilingi milioni 118 zimetolewa kwa walengwa badala ya kupelekwa kwenye shughuli
nyingine za maendeleo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu zoezi
la uandikishaji kwa wale ambao hawajaandikishwa, Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu amesema kipaumbele cha uandikishaji
kilitolewa kwenye vijiji ambavyo havikuwahi kuandikishwa kabisa.
Ameongeza kuwa, zoezi la
uandikishaji litaendelea kuanzia tarehe 10 mwezi huu, hivyo amewataka ambao hawajaandikishwa
kuvuta subira mpaka zoezi hilo litakapoanza.
Mhe. Ndejembi amewatembelea
walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Mpanda mkoani
Katavi kwa lengo la kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku wanayoipokea kutoka
TASAF ili waweze kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza
matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
Mwenyekiti wa
Chama cha Walemavu Mkoa wa Katavi, Bw. Dominick Pesambili akiwasilisha taarifa
ya utekelezaji wa ujenzi wa karakana ya watu wenye ulemavu mkoani Katavi kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF
kwa walengwa.
Mwonekano wa
jengo la karakana ya watu wenye ulemavu mkoani Katavi ambalo TASAF ilitoa fedha
kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wake.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji
cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda wakati wa ziara yake ya kikazi
ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza matumizi mazuri ya ruzuku
inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji
wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akitoa ufafanuzi kuhusu uandikishwaji wa walengwa wa
TASAF katika Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya
Manispaa ya Mpanda.
Mlengwa wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya
Mpanda, Bw. Shija Shimela akitoa ushuhuda wa namna Mpango huo ulivyosaidia
kuboresha maisha yake.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akiwa katika picha ya pamoja na mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa
Kijiji cha Kawanzige, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bibi Zena Kangamili wakati
wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuhimiza
matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF kwa walengwa.
No comments:
Post a Comment