Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 12 Agosti, 2021
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael amesema, ofisi yake imejiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi ya watumishi wote kwa pamoja mara moja kwa wiki ili kujenga afya ya mwili na akili ya watumishi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
Dkt. Michael amesema hayo, mara baada ya kukamilika kwa mazoezi ya watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yaliyofanyika kwenye eneo la wazi la ofisi yake lililopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa, mazoezi ni muhimu kwa kujenga mwili kwani mwili wenye afya unakuwa na akili yenye afya, hivyo watumishi watakuwa na afya itakayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.
“Tuko kwenye kipindi kigumu cha kukabiliana na janga la corona ambacho miili yetu inatakiwa kuwa imara kiafya ili kujikinga na ugonjwa wa corona”, Dkt. Francis amesisitiza.
Dkt. Francis amefafanua kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni msimamizi wa Utumishi wa Umma nchini, hivyo imeanza utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuwa mfano bora wa kuigwa na taasisi nyingine za umma lengo likiwa ni kuimarisha afya za watumishi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Prisca Lwangili amefurahia hatua ya uongozi kuwajali watumishi kwa kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuboresha afya za watumishi na hatimaye waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Bi. Lwangili amesema, mazoezi yatasaidia kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuwapata Watumishi wa Umma kwa sababu ya kufanya kazi kwa muda mrefu bila kushiriki mazoezi na kuongeza kuwa atafurahi kuona watumishi wakiendelea kushiriki mazoezi hayo kwa faida ya afya zao.
Kwa niaba ya watumishi wenzie, Bw. Humfrey Mbuma amesema watumishi wamefurahi kuanza rasmi mazoezi kwani mazoezi ni furaha na ni afya hivyo amewakaribisha watumishi wa taasisi nyingine za umma kushiriki mazoezi ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanza utaratibu wa watumishi wake kufanya mazoezi walau mara moja kwa wiki kwa lengo la kujenga afya za watumishi wake na kuboresha utendaji kazi unaoendana na Kaulimbiu ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael (katikati) akiongoza mazoezi ya viungo kwa Watumishi wa ofisi yake yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifanya mazoezi ya viungo kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Anayesimamia ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakicheza mpira wakati wa mazoezi ya kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Prisca Lwangili akiushukuru uongozi wa ofisi yake kuwajali watumishi kwa kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuboresha afya.
Mtumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Humfrey Mbuma akitoa wito kwa watumishi wa taasisi nyingine za umma kushiriki mazoezi ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
No comments:
Post a Comment