Friday, July 5, 2024

MHE. SIMBACHAWENE ATEMBELEA FAMILIA YA MWL. NYERERE NA JUMBE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amemtembelea Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam leo tarehe 5 Julai, 2024.

Mhe. Simbachawene amefika nyumbani kwa mama Maria Nyerere kwa lengo la kumsalimia, kumjulia hali na kusikiliza chagamoto alizonazo na kuzitafutia ufumbuzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake kama Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na utawala bora.

Aidha, Mama Maria amemshukuru Mhe. Simbachawene kwa kupata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali. Vile vile amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali familia yake na kuwatunza wakati wote bila kuchoka na amemuombea kwa Mungu aendelee kuiongoza vyema Tanzania.

Awali, Mhe. Simbachawene aliitembelea familia ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, 1972 - 1984 Hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Mhe. Simbachawene amekutana na kufanya mazungumzo na Wenza wa Hayati Jumbe (Bi. Zeyana Rashid Mwinyi na Bi. Fatma Mohammed Mwinyi) ambao kwa pamoja wamemshukuru kwa ziara hiyo ya kuwatembelea na kuwajulia hali.

Mhe. Simbachawene amesema pamoja na kufika mahali hapo na kuwajulia hali na kusikiliza changamoto zinazowakabili, ameongeza kuwa amebeba salaam za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anathamini sana mchango wa viongozi waliomtangulia na ataendelea kusimamia na kutunza familia hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

“Rais, amenielekeza kuwafikishia salaam zake na amesema yuko pamoja nanyi na ndio maana amenituma kufika kuwajulia hali na kusikiliza changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi” amesema Mhe. Simbachawene.

Aidha, ameahidi kuwaelekeza watendaji katika ofisi yake, kushughulikia changamoto zinazojitokeza na kuwafanya wenza wa viongozi hao kuendelee kuishi kwa amani na usalama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na Mama Maria Nyerere alipomtembelea nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai, 2024.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na Mama Maria Nyerere alipomtembelea nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai, 2024. 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Wenza wa Hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi alipotembelea familia hiyo Kigamboni Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai, 2024. Kutoka kushoto ni Bi. Zeyana Rashid Mwinyi na Bi. Fatma Mohammed Mwinyi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akijadili jambo na Wenza wa Hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi alipotembelea familia hiyo Kigamboni Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai, 2024. Kutoka kushoto ni Ms. Kauthar Ally Rashid (Mpwa wa Hayati Sheikh Aboud Jumbe), Bi. Zeyana Rashid Mwinyi na na Bi. Fatma Mohammed Mwinyi.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na Ms. Kauthar Ally Rashid (Mpwa wa Hayati Sheikh Aboud Jumbe) alipotembelea familia hiyo Kigamboni Jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai, 2024. Wakifuatilia ni Wenza wa Hayati Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi Bi. Zeyana Rashid Mwinyi na Bi. Fatma Mohammed Mwinyi.




No comments:

Post a Comment