Saturday, April 30, 2022
MHE. NDEJEMBI AIELEKEZA e-GA KUZICHUKULIA HATUA TAASISI ZINAZOKIUKA SHERIA YA SERIKALI MTANDAO
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 30 Aprili, 2022
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)
kuzichukulia hatua stahiki taasisi zote za umma zinazokiuka matakwa ya Sheria
ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo
hayo jijini Dodoma alipokuwa akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo
vya TEHAMA Serikalini kilichohusu mafunzo ya uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za
Serikali Mtandao.
Mhe. Ndejembi amesema e-GA ni mamlaka kamili hivyo, inapaswa
kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria pale inapoona taasisi za umma zinajenga
mifumo ya TEHAMA bila kibali cha mamlaka hiyo au zinapokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu
na Miongozo ya Serikali Mtandao.
“e-GA mna meno kisheria hivyo anzeni kuitekeleza Sheria ya Serikali
Mtandao kwa vitendo kwa kuzichukulia hatua mara moja taasisi zote zinakwenda
kinyume na sheria hiyo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Akizungumzia malalamiko ya
upatikanaji wa mtandao kwenye baadhi ya maeneo, Mhe. Ndejembi amewataka Wakuu
wa Idara na Vitengo vya TEHAMA kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ambayo wananchi
wamekuwa wakiilalamikia pindi wanapohitaji huduma zinazotolewa na Taasisi za
Umma kupitia mifumo ya TEHAMA.
“Unakuta mwananchi anatembea
umbali mrefu kufuata huduma ya kulipa kodi kwa manufaa ya taifa, halafu
anaambiwa mtandao hakuna kwani mfumo haufanyi kazi, na wakati mwingine kwenye
halmashauri zetu kutengeneza namba ya malipo mwananchi anaambiwa mtandao uko
chini jambo ambalo linakwamisha utoaji wa huduma,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Ameongeza kuwa, Serikali ya
Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuwa na Serikali ya Kidijitali itakayoondoa
changamoto ya wananchi kutopata huduma bora na kwa wakati, hivyo amewaasa wataalam
wa TEHAMA kutumia ujuzi wao katika kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji
wa huduma Serikalini.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge
amesema, kikao kazi hicho cha wataalam wa TEHAMA kinadhihirisha dhamira ya
ofisi yake kupitia mamlaka ya Serikali Mtandao kuwa na jukwaa la kudumu la
kukumbushana mkakati wa kuhakikisha TEHAMA inatumika ipasavyo kurahisisha
utendaji kazi wa taasisi za Serikali kwa
lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka
ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi
Benedict Ndomba amemhakikishia Mhe. Ndejembi kuwa, e-GA itaendelea kutekeleza
jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za serikali
mtandao kwa taasisi za umma na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni na
miongozo ya Serikali Mtandao.
Kikao kazi hicho cha siku
mbili kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa TEHAMA wa Wizara, Wakuu wa TEHAMA wa Idara
Zinazojitegemea, Mamlaka na Wakala za Serikali, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa
Mikoa, Majiji na Manispaa, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Halmashauri za Wilaya
na Wakuu wa TEHAMA wa Taasisi za Umma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kikao kazi chao kilichofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Bw. Hassan Kitenge akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Mhe. Deogratius
Ndejembi kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini
kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)
Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri
Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga
kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika
jijini Dodoma.
Friday, April 29, 2022
BW. HASSAN SHAIBU MFANYAKAZI HODARI WA OFISI YA RAIS - UTUMISHI KWA MWAKA 2021/2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasalimia watumishi wa Ofisi yake
jijini Dodoma kabla ya kuanza kwa kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa
Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi
wa ofisi yake kwenye kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.
Mkurugenzi wa Utawala na
Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na
Utawala Bora, Bw. Mussa Magufuli akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Katibu Mkuu, ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro kuzungumza na watumishi wa ofisi hiyo wakati wa kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi
hiyo kwa mwaka 2021/2022.
Sehemu ya Wakurugenzi wa Idara
na Vitengo wa Ofisi ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakimsikiliza
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro (hayupo pichani) kwenye kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo
kwa mwaka 2021/2022.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi
ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
(hayupo pichani) alipokuwa akimtangaza mfanyakazi hodari wa Ofisi yake kwa
mwaka 2021/2022.
Mfanyakazi hodari wa Ofisi ya
Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Hassan Shaibu akiwa
amesimama mbele ya Watumishi wenzake kuwashukuru mara baada ya kuchaguliwa kuwa
mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka
2021/2022.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro
(wapili kutoka kushoto) akiwaongoza wasimamizi waliokuwa wakizihesabu kura baada
ya kumchagua mfanyakazi hodari wa ofisi yake.
Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala Rasilimaliwatu Bw. Mussa Magufuli na
kushoto kwake ni Mwakilishi wa TUGHE Tawi la Utumishi Bi. Mwadawa Nchemwa.
Baadhi
ya watumishi wa Ofisi ya Rais - Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora wakimpongeza mtumishi mwenzao Bw. Hassan Shaibu (watatu kutoka kushoto) baada
ya kutangazwa kuwa mfanyakazi hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.
Mwakilishi wa TUGHE Tawi la
Ofisi ya Rais - UTUMISHI Bi. Mwadawa Nchemwa akiwafahamisha watumishi wa Ofisi
hiyo vigezo vya kumpata mfanyakazi hodari wakati wa kikao cha kuchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi
hiyo kwa mwaka 2021/2022. Wakwanza kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro na wapili kulia
ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw. Mussa Magufuli.
Mmoja kati wa wasimamizi wa
uchaguzi wa kumpata mfanyakazi hodari wa
Ofisi ya Rais Memeijimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Elibariki Kahungya akigawa karatasi za
kupigia kura kwa ajili ya kumpata mtumishi mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa
mwaka 2021/2022.