Friday, December 30, 2022

Friday, December 23, 2022

MAELEKEZO YA WN-OR (MUUUB) MHE. JENISTA MHAGAMA KWA WAAJIRI KUHUSU UTEKELEZAJI WA AGIZO LA KUWAREJESHEA MICHANGO WALIYOCHANGIA KATIKA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII WATUMISHI WALIOONDELEWA KATIKA UTUMISHI WA UMMA KWA KUGHUSHI VYETI

Mnamo tarehe 27 Oktoba, 2022 nilitoa maelekezo ya Serikali ya namna ya kushughulikia watumishi wa umma walioondolewa kazini kwa sababu ya kughushi vyeti. Katika maelekezo hayo, niliwahimiza waajiri kutekeleza masuala yafuatayo:-

a)   Kutoa ushirikiano kwa watumishi walioghushi vyeti pindi wanapofika katika Ofisi zao kukamilisha taratibu za ulipwaji ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka muhimu kwa ajili ya kulipwa michango yao walioiachanga kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwa ni pamoja na kujaza na kusaini Hati ya Ridhaa (Commitment Bond). Aidha, niliwaagiza waajiri wote kuwasiliana na Ofisi za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii za Wilaya na Mikoa ili kupata taarifa sahihi za watumishi hao zinazohusiana na zoezi hilo.

b)   Kuandaa na kuwasilisha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hati ya ridhaa (Commitment Bond) pamoja na nyaraka nyingine kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Mifuko husika;

c)   Kuandaa Dawati la Msaada (Help Desk) ili kufanikisha na kurahisha mchakato wa ulipaji wa michango hiyo ikiwa ni pamoja na ujazaji wa mkataba wa makubaliano (Commitment Bond);

d)   Kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa zoezi hili.

Pamoja na kutoa maelekezo hayo, mara kadhaa Ofisi yangu imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya walengwa wanaohusika na zoezi hili kuwa baadhi ya waajiri hawatekelezi maelezo hayo ya Serikali kwa ukamilifu na hasa kutokutoa ushirikiano katika ujazaji wa Hati ya Ridhaa (Commitment Bond) pamoja na kuchelewesha kuwasilisha vielelezo husika kwa ajili ya kuwawezesha walengwa kurejeshewa michango yao, jambo ambalo linaleta usumbufu kwa walengwa kufuatilia msamaha ambao Mhe. Rais ameutoa.

Kwa kuwa nina dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, natumia fursa hii kwa mara nyingine kuwaelekeza tena waajiri wote kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo maelekezo ya Serikali niliyoyatoa mnamo tarehe 27 Oktoba, 2022.

Hata hivyo, kupitia Ofisi yangu, nimekwisha kuunda Timu ya kufanya uhakiki na kufuatilia mienendo ya waajiri wote katika kutekeleza maelekezo haya ya Serikali. Ninaamini kila mwajiri atatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza utekelezaji wa agizo la kuwarejeshea michango waliyochangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii watumishi walioondelewa katika utumishi wa umma kwa kughushi vyeti.


 

Thursday, December 22, 2022

MAAFISA TARAFA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI MUDA WA KAZI KUWAHUDUMIA WANANCHI – Bw. Xavier Daudi

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 22 Disemba, 2022

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Maafisa Tarafa 48 waliohudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo kiutendaji, kuutumia vizuri muda wa kazi katika kuwahudumia wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia. 

Bw. Daudi ametoa wito huo kwa Maafisa Tarafa hao jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili waendane na kasi ya utendaji kazi ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Bw. Daudi amewataka Maafisa Tarafa kutotumia muda wa kazi katika mitandao ya kijamii wakati wana jukumu la msingi la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Bw. Daudi ameongeza kuwa, ofisi yake imeshirikiana na TAMISEMI kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Tarafa, kwa kutambua kuwa maafisa hao ni kiungo muhimu kati Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma.

“Ninyi ni kiungo kikubwa cha kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo ukisikia Serikali inalaumiwa kwa kutotoa huduma bora kwa wananchi au kupongezwa kwa kutoa huduma bora ninyi Maafisa Tarafa mnahusika, na ndio maana tumeamua kuwapatia mafunzo ili mkatekeleze majukumu yenu kikamilifu,” Bw. Daudi amefafanua.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewataka Maafisa Tarafa kusimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa ngazi ya tarafa kwani Sheria inamtambua Afisa Tarafa kuwa ni mwakilishi wa Afisa Tawala wa Wilaya kwenye ngazi ya tarafa ambapo moja ya jukumu la Afisa Tawala Wilaya ni kuhakikisha mamlaka zote za Serikali kwenye ngazi ya wilaya zinatimiza majukumu ya kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma iliyopo.

Naye, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Edith Rwiza amesema, mafunzo kwa Maafisa Tarafa hao yametolewa kwa siku mbili yakilenga kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Tarafa waliopatiwa mafunzo, Bw. Titho Cholobi ambaye ni Afisa Tarafa wa Elerai Wilaya ya Arusha amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yamewawezesha kuzaliwa upya kiutendaji na kuongeza kuwa, yeye binafsi mafunzo hayo yamemuwezesha kubaini mapungufu aliyokuwa nayo katika utendaji kazi wake.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Maafisa Tarafa wa Mikoa (hawapo pichani) wakati akifunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi kufunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima, akitoa nasaha kwa Maafisa Tarafa wa Mikoa walioshiriki Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.

 


Afisa Tarafa wa Elerai Wilaya ya Arusha, Bw. Titho Cholobi akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (katikati) akifurahia jambo wakati Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima (Wa kwanza kulia) akiagana na Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza mara baada ya kufunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tafara wa Mikoa yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa mara baada ya kufunga Mafunzo ya Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima na kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza.


 

Wednesday, December 21, 2022

PROGRAMU YA TAKUKURU RAFIKI KUMUWEZESHA KILA MTANZANIA KUSHIRIKI MAPAMBANO DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA - Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 21 Disemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Programu ya TAKUKURU RAFIKI aliyoizindua inatoa fursa kwa kila Mtanzania kushirikiana na Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kutekeleza jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo ni kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizindua Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper.

Mhe. Jenista amesema kuwa, kupitia TAKUKURU RAFIKI kila Mtanzania atajiona kuwa ni sehemu ya TAKUKURU na anao wajibu wa kuzuia vitendo vya rushwa mahali alipo, anapoishi, anapofanya biashara au kazi yoyote ambayo inaendesha maisha yake.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa TAKUKURU kupitia programu ya TAKUKURU RAFIKI itajiweka karibu na jamii na kuwa rafiki wa wananchi hivyo, kuwawezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa urahisi ambazo zitaiwezesha TAKUKURU kutekeleza wajibu wake kwa manufaa ya taifa.

“Leo nimezindua TAKUKURU RAFIKI ambayo faida yake kwa taifa ni kuboresha mifumo ya utoaji wa taarifa na elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, ili kila mwananchi ashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, programu ya TAKUKURU RAFIKI itajenga utayari wa wananchi kuichukia rushwa na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa ni adui mkubwa wa maendeleo katika taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, ACP Salum Hamduni amesema TAKUKURU RAFIKI ni programu ambayo itaongeza wigo wa wananchi kushiriki katika utambuzi na utatuzi wa vitendo vya rushwa katika jamii na kuongeza kuwa, katika kutekeleza programu hiyo taasisi yake itajielekeza zaidi kwenye usimamizi wa utoaji wa huduma za kijamii na fedha zilizotolewa na Serikali kutekeleza miradi katika sekta za kipaumbele za maji, elimu, kilimo, afya, barabara na ardhi.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amesema kuwa Programu ya TAKUKURU RAFIKI itamuwezesha mwananchi kutambua thamani ya mradi unaotekelezwa katika eneo alilopo na ni kwa namna gani atashiriki katika kusimamia utekelezaji wake ili uwe na tija katika jamii. 

Programu ya TAKUKURU RAFIKI imezinduliwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU ambao kaulimbiu yake ni ‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu: Tutimize Wajibu Wetu’.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Viongozi wa TAKUKURU wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma. 


Sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipozungumza nao wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma. 


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Viongozi wa TAKUKURU wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma. 


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akitoa salamu za Kamati yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni Nakala ya Program Ya TAKUKURU RAFIKI wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma.

 

Kwaya ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikitumbuiza kwa wimbo maalum wa kuhamasisha utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa TAKUKURU mara baada ya Waziri huyo kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma.

 



Tuesday, December 20, 2022

SERIKALI HAITOMVUMILIA KIONGOZI YEYOTE ATAKAYESHINDWA KUSIMAMIA VIZURI RASILIMALIWATU KWA USTAWI WA TAIFA

 Na. James K. Mwanamyoto-Kilosa

Tarehe 20 Disemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita haitosita kumchukulia hatua za kinidhamu na kisheria kiongozi yeyote atakayeshindwa kusimamia vizuri rasilimaliwatu kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Mhe. Jenista amesema hayo, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.

Mhe. Jenista amesema, hatomuonea aibu wala huruma kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu ambaye atabainika kukiuka sheria na taratibu za usimamizi wa rasilimaliwatu.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, viongozi wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu wanapaswa kuiheshimu, kuithamini na kuhakikisha inakuwa kwenye mikono salama kwasababu inategemewa na Serikali kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya taifa.

“Rasilimaliwatu ambayo ndio watumishi wa umma ikisimamiwa vizuri itaisaidia Serikali kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo katika taifa,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, watumishi wa umma ndio wanategemewa kutoa huduma bora za afya, kuboresha huduma za maji, kuboresha huduma za elimu, kuboresha huduma za miundombinu pamoja na kilimo. 

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Kilosa, Mwalimu Richard Shagungu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa kila mwezi madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi katika Halmashauri hiyo na kuomba waajiri wasizalishe madai mapya ili Serikali iyamalize madai yaliyopo sasa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ili kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.


Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akitoa salaam za wananchi wa jimbo lake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.


Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mhe. Dennis Londo akitoa salaam za wananchi wa jimbo lake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.


Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Kilosa, Mwalimu Richard Shagungu akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Kilosa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiimba Wimbo wa Taifa na viongozi wengine walio meza kuu kabla ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wakati ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mara baada ya kuwasili Wilayani humo ili kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo, wakati ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi walio katika halmashauri hiyo.



Saturday, December 17, 2022

MHE. NDEJEMBI AWATAKA WATUMISHI KUSIMAMIA MIRADI INAYOTEKELEZWA KATIKA MAENEO YAO YA KAZI BILA KUSIMAMIWA NA VIONGOZI

 Na. Veronica E. Mwafisi-Temeke na Ubungo

Tarehe 17 Disemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa umma kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo yao ya kazi bila kusimamiwa na viongozi wa ngazi za juu kwani ni wajibu wao kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Serikali inakamilika kwa wakati kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Ubungo, Mhe. Ndejembi amesema, kuna baadhi ya maeneo usimamizi wa miradi ya serikali ni hafifu hivyo inamlazimu Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi wa halmashauri aende kuhimiza usimamizi wa miradi.

 “Hakuna mradi wa umma au wa Serikali ambao hausimamiwi na mtumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi wa umma katika eneo lake na kwa nafasi yake kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya taifa,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, miradi yote inayotekelezwa na Serikali ina umuhimu kwa wananchi katika eneo la utoaji wa huduma za afya, elimu na nyinginezo, hivyo ni lazima watumishi wa umma waisimamie kikamilifu.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Jaffery Naigesha amemshukuru Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kwa maelekezo mbalimbali ya kiutumishi aliyoyatoa, na kuongeza kuwa anaamini yatawajenga kiutendaji watumishi wa umma.

Mhe. Naigesha amemweleza Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kuwa, mafanikio yote ambayo Manispaa ya Ubungo imeyapata yanatokana na fedha za utekelezaji wa miradi walizopatiwa  na  Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bw. Elihuruma Mabelya amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.

Bw. Mabelya ameahidi kuwaongoza watumishi wa halmashauri yake katika kusimamia miradi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Manispaa hiyo.

Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo  wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Manispaa hiyo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Jaffrery Naigesha akitoa shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kumaliza kuzungumza na watumishi wa Manispaa hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bw. Elihuruma Mabelya akitoa shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kumaliza kuzungumza na watumishi wa Manispaa hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma









HALMASHAURI ZATAKIWA KUWAPATIA MIKOPO WALENGWA WA TASAF WALIO KWENYE VIKUNDI KUPITIA MIKOPO YA ASILIMIA KUMI INAYOTENGWA KUVIKOPESHA VIKUNDI VYA WANAWAKE, VIJANA NA WENYE ULEMAVU

 Na. Veronica Mwafisi – Dar es salaam

Tarehe 17 Disemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo walengwa wa TASAF walio kwenye vikundi, kupitia fedha za asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili mikopo hiyo iboreshe maisha ya kaya maskini nchini kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia.

Mhe. Ndejembi ametoa rai hiyo, kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mhe. Ndejembi amesema, ameweza kutembelea vikundi mbalimbali vya walengwa wa TASAF katika Halmashauri zote zilizopo jijini Dar es salaam na kuona utekelezaji wa kazi za vikundi mbalimbali vinavyojumuisha Vijana, Wazee, Walemavu na Wanawake.

“Wilayani Kinondoni kuna vijana walio kwenye vikundi vya TASAF walipatiwa mikopo wa pikipiki ambapo wamemudu kurejesha, pia wanawake Temeke walio kwenye vikundi vya TASAF wamepatiwa mikopo ya shilingi milioni 10 na Ilala wamepatiwa milioni 30 ambayo imewawezesha kuboresha maisha yao na kujishughulisha na ujasiriamali,” Mhe. Ndejembi amefafanua.  

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bi. Salome Mwakigomba amesema TASAF imefanya jitihada kubwakuhamasisha uundaji wavikundi vya walengwa katika halmashauri zote ambazo Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unatekelezwa hivyo wakipatiwa mikopo hiyo ya asilimia 10 watendelea kuboresha maisha yao.

Bi. Mwakigomba amesema, TASAF itatekeleza maelekezo ya Ndejembi ya kuwahamasisha walengwa wa TASAF kuwa na miradi endelevu ili wajiongezee kipato kitakachowawezesha kuboresha maisha yao.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF wa Kikundi cha Twiyendage kilichopo Wilaya ya Ubungo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini Dar es salaam.

Sehemu ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Hapa Kazi tu na Umoja Group vya Wilaya ya Kigamboni wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Sehemu ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Jiwezeshe Women Group  Wilaya ya Temeke wakionesha baadhi ya bidhaa wanazotengeneza, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TASAF, Bi. Salome Mwakigomba akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi jijini Dar es Salaam, iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.





MHE. JENISTA AKEMEA TABIA YA WAAJIRI SERIKALINI KULIPA MADENI YA WAKUU WA IDARA PEKEE NA KUYAACHA YA WATUMISHI WENGINE

Na. James K. Mwanamyoto-Ikungi

Tarehe 17 Disemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amekemea tabia ya baadhi ya waajiri Serikalini kutoa kipaumbele cha kulipa madeni yasiyo ya mishahara kwa Wakuu wa Idara pekee na kuyaacha ya watumishi walio wengi, kitendo ambacho kinashusha ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma nchini.

Mhe. Jenista amekemea tabia hiyo wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.

Mhe. Jenista amesema, kama mwajiri amekusanya mapato na ana lengo la kulipa madeni yasiyotokana na mishahara, anapaswa kutenda haki kwa kuweka usawa katika kulipa madeni ya watumishi na Wakuu wa Idara badala ya kutoa kipaumbele kwa Wakuu wa Idara pekee.

“Si haki kwa Wakuu wa Idara kutengenezewa mkakati wa kulipwa peke yao na watumishi wengine kutolipwa na ikizingatiwa kuwa wanatoa mchango mkubwa katika kuwahudumia wananchi,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kitendo cha waajiri kulipa madeni ya Wakuu wa Idara pekee, amekuwa akikikemea mara kwa mara wakati wa vikao kazi vyake na waajiri kwani kinaathiri saikolojia ya utendaji kazi wa watumishi wa umma na kukwamisha lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Waajiri msijali sana maslahi ya Wakuu wa Idara na kusahau kuzingatia maslahi, haki na stahiki za watumishi wa umma ambao ni wengi kuliko Wakuu wa Idara hivyo, mnapaswa kuzingatia agizo hili,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Akizungumzia madeni ya malimbikizo ya mishahara, Mhe. Jenista amesema madeni hayo yamezingatiwa na Serikali kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza itengwe fedha jambo ambalo lilitekelezwa na katika mwaka wa fedha ujao itatengwa pia ili kuendelea kuwalipa watumishi wanaostahili, na kuongeza kuwa ofisi yake imejipanga kuhakiki madai yote yatakayowasilishwa ili yalipwe kwa wakati.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba ameunga mkono maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama, na kuwashauri waajiri kuanza kulipa madeni ya watumishi wa umma walio wengi kwani wakianza kuwalipa Wakuu wa Idara ambao kila mmoja anadai fedha nyingi, sehemu kubwa ya makusanyo itaishia kulipa madeni ya Wakuu wa Idara pekee.

“Watumishi walio wengi wanadai kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na Wakuu wa Idara, hivyo, wakilipwa hao kwanza, watabakia Wakuu wa Idara ambao wanadai fedha nyingi, na hata kama wakuu hao wakilipwa mmoja mmoja kiasi chote cha fedha wanachodai wataona thamani ya fedha waliyokuwa wakiidai,” Mhe. Serukamba amefafanua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Jerry Muro amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Ikungi, kitendo ambacho kimejenga morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma walio katika wilaya yake ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia kukusanya mapato yatakayoisaidia Serikali kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Singida, ambayo ililenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma, kukagua utekelezaji wa majukumu ya Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini mkoani humo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.

 

Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba akitoa salamu za mkoa wake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika halmashauri hiyo.

 

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Jerry Muro akieleza hali ya Utumishi wa Umma katika wilaya yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika Wilaya ya Ikungi.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Bi. Martha Mlata katika Ofisi za CCM mkoani humo, mara baada ya Waziri huyo kuwasili mkoani Singida kwa ajili ya ziara ya kikazi.