Na. Veronica E. Mwafisi-Arusha
Tarehe 30 Novemba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewataka Watumishi wa Umma nchini kuacha kiburi na majivuno pindi wanapotoa huduma kwa wananchi kwani mishahara wanayolipwa na Serikali inatokana na kodi za wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo kwa Watumishi wa Umma nchini, wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri inayofanyika jijini Arusha.
Mhe. Mchengerwa amesema, Watumishi wa Umma wanapaswa kuwahudumia wananchi ipasavyo kama ambavyo wao wanatamani kuhudumiwa na Serikali.
“Baadhi yetu, kuna vitendo tunavifanya ambavyo haviwapendezi wananchi tunapowahudumia, hivyo tuhakikishe tunatoa huduma bora kama ambavyo sisi tunavyoitaka Serikali ituhudumie,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Akihimiza Watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao pasipo kushurutishwa, Mhe. Mchengerwa amenukuu maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyowahi kusema kwamba, si jambo jema kwa mtu mzima kuwekewa mnyampara ili aweze kumfunza nidhamu ya utendaji kazi hivyo, Watumishi wanapaswa kutimiza wajibu wao bila kushurutishwa.
Akisisitiza dhana ya kujisimamia kiutendaji, Waziri Mchengerwa amemnukuu Rais wa Awamu wa Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye aliwahi kusema kuwa, hajaumbwa kufokafoka, ataangalia utendaji kazi wa kila mtumishi kwa nafasi aliyonayo kwani wote ni watu wazima ambao wanatambua mazuri na mabaya, na ikitokea wakifanya mabaya basi inakuwa ni kwa makusudi hivyo yeye ataongea kwa kalamu.
Kwa Muktadha huo, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, fikra na maono ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ndio fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo Watumishi wa Umma tunapaswa kuishi kwa vitendo fikra na maono hayo ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika kuunga mkono fikra na maono ya viongozi hao kuhusu uwajibikaji, Mhe. Mchengerwa amewataka Watumishi wote wa Umma nchini kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi aliyonayo anafanya kazi kwa bidii na weledi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Awali, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kufungua Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri, Mwenyekiti wa TUGHE taifa Bw. Joel Kaminyoge amempongeza Waziri Mchengerwa kwa utendaji kazi mzuri hususani katika kusimamia masilahi ya Watumishi wa Umma nchini.
Bw. Kaminyoge amesema kuwa, utendaji kazi wa Waziri Mchengerwa unadhihirisha kuwa, katika historia ya Utumishi wa Umma amekuwa ni miongoni mwa Mawaziri bora kabisa waliowahi kutokea kushika wadhifa huo wa kumsaidia Mhe. Rais kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Semina hiyo yenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji viongozi hao wa TUGHE na Waajiri inafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 29 Novemba, 2021 hadi tarehe 03 Disemba, 2021.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi wa Matawi wa TUGHE (hawapo pichani) walioshiriki Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri kabla ya Waziri huyo kufungua Semina hiyo iliofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri iliofanyika jijini Arusha.
Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Bw. Joel Kaminyoge akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kufungua Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri iliofanyika jijini Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki kuimba wimbo wa kuhamasisha mshikamano kwa Watumishi wa Umma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Bw. Joel Kaminyoge na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini –UTUMISHI, ACP Ibrahim Mahumi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Semina ya Viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri mara baada ya Waziri huyo kufungua Semina hiyo iliofanyika jijini Arusha.