Saturday, September 28, 2019

DKT. MWANJELWA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO LA KITUO CHA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA JIJINI MWANZA



Na Happiness Shayo – Mwanza
Tarehe 28 Septemba, 2019

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kilichopo eneo la Pasiansi jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa kituo hicho, Dkt. Mwanjelwa amesema ujenzi wa mradi huo uko katika hatua nzuri hivyo, ameipongeza Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa kufikia hatua hiyo.
 “Hakika jengo hili ni la viwango, linaridhisha na vifaa vya ujenzi vilivyotumika viko katika viwango bora” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutenga bajeti iliyowezesha ujenzi wa kituo hicho kwani mradi huo ulianza tangu mwaka 2008.
“Matumizi ya mkandarasi na mshauri binafsi yalisababisha kuwapo kwa gharama kubwa za ujenzi zilizosababisha kusimama kwa ujenzi katika hatua za awali, lakini mwaka 2017/2018 Serikali ya Awamu ya Tano ilithamini mradi na kutoa fedha zilizofanikisha mradi kama unavyoonekana sasa” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi amesema, Serikali iliamua kujenga kituo hicho cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa  kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka mbalimbali za ofisi za serikali zilizopo kanda ya ziwa.
Bw. Msiangi amesema, kituo kitakapokamilika kitatumika kama kituo mbadala cha kuhifadhi mifumo ya kumbukumbu na nyaraka iliyopo katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu cha jijini Dodoma.
Naye, Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mkoa wa Mwanza, Bw. Victor Baltazar amemthibitishia Dkt. Mwanjelwa kuwa, ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2019.
“Mpaka sasa tumejenga jengo la utawala, maghala ya kuhifadhia nyaraka kwa asilimia 95 na pia tumejenga uzio, eneo la kuegesha magari, eneo la bustani, banda la walinzi na madereva kwa asilimia 60” Bw. Baltazar amefafanua.

Ziara ya Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa ya kutembelea kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Mwanza ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake la kukagua utekelezaji wa miradi iliyo chini ya Ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza leo






Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza leo.




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firmin Msiangi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza leo.





Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mkoa wa Mwanza, Bw. Victor Baltazar akitoa ufafanuzi wa michoro ya ramani ya Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa kituo hicho.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (katikati) akielekeza jambo kwa Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Ziwa jijini Mwanza leo. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mkoa wa Mwanza, Bw. Victor Baltazar.

No comments:

Post a Comment