Saturday, October 29, 2022

MHE. JENISTA NA MHE. SULEIMAN WAFANYA KIKAO KAZI KUJADILI NAMNA YA KUBORESHA UTENDAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA

Na. James K. Mwanamyoto-Zanzibar

Tarehe 29 Oktoba, 2022

Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia masuala ya utumishi wa umma na utawala bora wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jenista Mhagama na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Haroun Suleiman wamefanya kikao kazi cha kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuweka msingi bora wa watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuleta tija katika mandeleo ya taifa. 

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi hicho kilichofanyika Unguja Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, wamekubaliana kubadilishana maarifa na uzoefu kwa pande zote mbili za muungano katika eneo la utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA ya usimamizi wa utendaji kazi na tathmini ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma na taasisi za umma. 

Mhe. Jenista amesema, kupitia kikao kazi hicho imesisitizwa uzingatiaji wa taratibu za ajira Serikalini, uzingatiaji wa maadili kwa viongozi na watumishi wa umma, usimamizi wa rasilimaliwatu, kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja vyuo vya utumishi wa umma kufanya tafiti zitakazosaidia kutoa mwongozo wa namna sekta ya utumishi wa umma nchini itakuwa na tija kwa maendeleo ya taifa. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman amesema kikao kazi hicho kimekuwa na faida kubwa katika kujenga ushirikiano wa kiutendaji kwenye masuala ya muungano na yasiyo ya muungano, kati ya ofisi yake na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inayosimamiwa na Mhe. Jenista Mhagama. 

Kutokana na uwepo wa ushirikiano huo kiutendaji, Mhe. Suleiman amesema kikao kazi hicho kimetoa tamko la kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa namna wanavyohimiza ushirikiano pamoja na kusimamia masuala ya utumishi wa umma na utawala bora. 

Mhe. Suleiman ameongeza kuwa, anaamini kasi ya ushirikiano waliyonayo viongozi hao itaendelezwa pia na watumishi na watendaji walio chini yao, ili kufanikisha azma ya kuujenga utumishi wa umma na utawala bora wenye tija katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuleta maendeleo nchini. 

Awali akisoma maazimio ya kikao kazi hicho, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kikao kimeazimia kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wao katika kusimamia vizuri masuala ya utumishi wa umma na utawala bora. 

Bw. Daudi ameyataja maazimio mengine kuwa ni kuwekwa kwa asilimia ya utekelezaji wa masuala ya utumishi wa umma na utawala bora yaliyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, taasisi zote zilizoweka saini ya makubaliano ya masuala ya kutekeleza ziendelee kufanya hivyo na wakauu wa taasisi na watendaji waendelee kukutana kwa mujibu wa ratiba ya vikao.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari Unguja Zanzibar, mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi chake na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman kilicholenga kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman akiongoza kikao kazi cha kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwasilisha kwa Mhe. Jenista Mhagama na Mhe. Haroun Suleiman maazimio ya kikao kazi kilichojadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Baadhi ya maafisa na watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia kikao kazi cha kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman na watendaji wao wakiwa katika kikao kazi kilicholenga kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman wakisaini masuala waliyokubaliana kuyatekeleza kupitia kikao kazi chao kilichojadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haroun Suleiman wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Serikali, mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi kilicholenga kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 


 

Friday, October 28, 2022

MAKTABA YA UONGOZI KUCHOCHEA UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI KATIKA KULITUMIKIA TAIFA - Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 28 Oktoba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema viongozi walio katika Taasisi za Umma na Sekta Binafsi wakijenga utamaduni wa kusoma vitabu mbalimbali watapata elimu na maarifa yatakayowawezesha kuwajibika kikamilifu katika kuwahudumia wananchi na kulitumikia taifa. 

Mhe. Jenisa amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Maktaba ya Uongozi iliyoanzishwa na Taasisi ya UONGOZI kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi walio katika sekta ya umma na sekta binafsi nchini. 

Mhe. Jenista amesema kuwa, maktaba hiyo ya uongozi ikitumiwa vizuri itakuwa ni kituo muhimu cha kuchochea uwajibikaji wa viongozi katika taifa kwani maudhui watakayoyasoma kupitia vitabu mbalimbali yatawapatia maarifa yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. 

“Ninakubaliana na wale wanaoamini kwamba msomaji wa vitabu akipata fursa ya kusoma vitabu anaongeza wigo wa kujielimisha, hivyo viongozi wanapaswa kuitumia maktaba hii kuongeza maarifa,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, maktaba hiyo itakuwa ni msaada kwa viongozi katika kuwaongezea maarifa yatakayowawezesha kutekeleza jukumu la kuwaongoza wananchi kuutekeleza mpango wa taifa wa kujenga uchumi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na kutekeleza Dira ya Taifa ya mwaka 2025. 

Mhe. Jenista amesema, Serikali inaamini kupitia machapisho na vitabu vilivyopo katika maktaba ya uongozi au maktaba nyingine zilizopo nchini, viongozi watasoma tafiti nyingi ambazo zitawajengea uwezo wa kufanya uchambuzi na upembuzi yakinifu kuhusu namna bora ya kutekeleza mipango ya maendeleo katika taifa. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema taasisi yake iliona umuhimu wa kuanzisha Maktaba ya Uongozi yenye machapisho, vitabu na taarifa mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya viongozi na wadau wengine kitaifa na kimataifa ambayo yamejikita kwenye maeneo ya uongozi, maendeleo endelevu, utawala bora, tawasifu za viongozi, historia, siasa na uchumi. 

Akitoa takwimu za idadi ya wanachama wa maktaba ya uongozi, Bw. Singo amesema kuwa, hadi kufikia Julai mwaka huu, maktaba hiyo ina wanachama hai zaidi ya 800 tofauti na wale wanaokuja kuitumia mara moja moja kulingana mahitaji yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisoma moja ya kitabu katika Maktaba ya Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI mara baada ya kuizindua rasmi maktaba hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Waliokaa kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka na kushoto kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wadau wa Taasisi ya UONGOZI mara baada ya kuzindua rasmi maktaba ya Uongozi na toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa “Maisha Yangu, Kusudi Langu” katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya wadau wa Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuzindua rasmi maktaba ya Uongozi na toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa “Maisha Yangu, Kusudi Langu” katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa uzinduzi wa maktaba ya Uongozi na toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa “Maisha Yangu, Kusudi Langu” katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizindua maktaba ya Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiangalia moja ya kitabu katika Maktaba ya Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI mara baada ya kuzindua rasmi maktaba hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifurahia maudhui yaliyomo katika moja ya kitabu kwenye Maktaba ya Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI mara baada ya kuzindua rasmi maktaba hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.  Kushoto kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizindua toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa “Maisha Yangu, Kusudi Langu” katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Anayeshiriki nae ni Mke wa Hayati Benjamin William Mkapa, Mama Anna. Wanaoshuhudia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka (kulia) na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue (kushoto) ambaye ameshiriki kutafsiri kitabu hicho.


 

Thursday, October 27, 2022

VIONGOZI MANISPAA YA IRINGA WATAKIWA KUZINGATIA MASLAHI YA WATUMISHI ILI KUWAJENGEA MORALI YA UTENDAJI KAZI

 Na. Veronica E. Mwafisi-Iringa

Tarehe 27 Oktoba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameutaka uongozi wa Manispaa ya Iringa kuzingatia mahitaji na maslahi ya watumishi ili kuwajengea ari na morali ya utendaji kazi katika kuwahudumia wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa viongozi wa Manispaa ya Iringa, wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa hiyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamozo zinazowakabili watumishi hao.

 "Mimi naomba sana viongozi mbadilike katika suala zima la kusimamia rasilimaliwatu, tuzingatie maslahi na mahitaji ya watumishi wetu ili kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii, weledi na morali ya hali ya juu," Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka wakuu wa idara katika Manispaa ya Iringa kuwa na utaratibu wa vikao vya mara kwa mara na watumishi wanaowasimamia ili kusikiliza kero zao na kuzitatua kwa wakati.

“Si jukumu la Mkurugenzi au Afisa Utumishi pekee kuzungumza na watumishi, wakuu wa idara mnawajibu wa kuwa na vikao vya kuzisikiliza kero na changamoto zinazowakabili watumishi mnaowaongoza ili kuzitatua," Mhe. Ndejembi amehimiza.

Kuhusiana na wingi wa malalamiko kutoka kwa watumishi, Mhe. Ndejembi amesema, uongozi wa Manispaa ya Iringa unapaswa kufanya tathmini ya hali ya utendaji kazi kwani idadi kubwa ya watumishi imewasilisha malalamiko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Mohammed Moyo amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutenga muda wa kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi katika wilaya yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi Mkoani Iringa iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao wa umma.


Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao wa umma.


Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Mohammed Moyo akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa yake, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo.

 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Mohammed Moyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya Naibu Waziri huyo katika halmashauri hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao wa umma.

Mtumishi wa Iringa Manispaa, Bi. Jamila Mwindi, akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo.


Katibu wa Naibu Waziri, Bw. Philemon Mmbaga (Wakwanza kulia) akichukua taarifa za mtumishi aliyewasilisha changamoto yake wakati wa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi aliyoifanya katika halmashauri hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo.