Na Antonia Mbwambo na Eric Amani-Dodoma
Tarehe 26 Mei, 2026
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, amewasisitiza Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kushiriki kikao kazi muhimu kilichopangwa kufanyika tarehe 1-3 Juni, 2026 katika ukumbi wa mabele hall jijini Dodoma.
Bw. Mkomi ametoa msisitizo huo Mei 26, 2026 wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI uliopo Mtumba jijini Dodoma
“Natoa wito kwa Wakuu wa Idara na vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kuhudhuria wao wenyewe katika kikao hicho bila kukosa kwakuwa kikao hiki kitakuwa na maelekezo mahususi ya kuboresha utendaji kazi.” Bw. Mkomi alisema.
Aidha, Bw. Mkomi amebainisha kuwa kikao hicho kitajadili na kufafanua kuhusu matumizi ya Mifumo mbalimbali ya kidijiti ikiwemo e-uhamisho, e-watumishi, e-utendaji, e-mrejesho na hr-assesment kwa kuzingatia shabaha za vipaumbele vya Taifa kuelekea dira 2050.
Ameongeza kuwa kikao hicho kitatoa nafasi ya kujadili kuhusu changamoto na mafanikio yaliyopo katika utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu na mapendekezo ya namna bora ya kuzishughulikia changamoto hizo. Pia washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuimarisha utendaji kazi katika Taasisi za Umma.
Bw. Mkomi amewataka washiriki kujisajili katika mfumo kupitia link ya tsms.gov.go.tz huku wakizingatia kwamba mwisho wa usajili ni tarehe 29 Juni, 2026.
Vile vile, Wakuu wa Idara na vitengo vya Usimamizi wa Rasilimaliwatu wamesisitizwa kufika katika ukumbi wa Mabele Hall uliopo jijini Dodoma tarehe 31 Mei, 2026 kuanzia saa 4 asubuhi kwa ajili ya kuchukua vitambulishi vyao vitakavyotumika katika kikao hicho.Kikao kazi hicho kitaongozwa na kauli mbiu isemayo; “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa ulio Sikivu,Jumuishi wenye Matokeo na Uwajibikaji kuelekea Dira 2050”.




No comments:
Post a Comment