Tuesday, May 26, 2026

KATIBU MKUU MKOMI AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUWA NA UHUSIANO MZURI KAZINI NA NJE YA KAZI

 Na Eric Amani. Mtumba-Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka watumishi wa umma kujenga na kudumisha uhusiano mzuri katika maeneo yao ya kazi na nje ya kazi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuimarisha mshikamano na kujenga taswira nzuri ya Utumishi wa Umma kwa jamii.

Akizungumza leo Mei 25, 2026 wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Mkomi amesema kuwa mazingira mazuri ya kazi hujengwa kupitia ushirikiano, kuheshimiana, mawasiliano bora na kuthaminiana miongoni mwa watumishi.

“Watumishi wa Umma tunapaswa kuwa mfano mzuri kwa jamii kwa kuzingatia maadili, nidhamu na kujenga mahusiano chanya siyo tu ofisini bali hata nje ya maeneo ya kazi. Umoja wetu una mchango mkubwa katika kuongeza tija na ubora wa huduma tunazozitoa kwa Umma,” amesema Bw. Mkomi.

Aidha, amewapongeza watumishi kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ya kila Jumatatu ambayo yamekuwa yakisaidia kuongeza uelewa, kuimarisha utendaji kazi na kujenga ari mpya ya kuwahudumia wananchi kwa weledi na uwajibikaji mkubwa zaidi.

Katibu Mkuu Mkomi pia amewataka watumishi kuendelea kushikamana, kusaidiana na kudumisha heshima baina yao ili kuifanya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora Serikalini.

Mafunzo hayo hutolewa kila siku ya Jumatatu katika eneo la Ofisi hiyo Mtumba, jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji, maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi akitoa neno kwa watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao Mei 25, 2026 Mtumba, Jijini Dodoma.

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Ummma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi( Wa kwanza Kulia)  akiwa na Baadhi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mei 25, 2026 wakimsikiliza mwezeshaji SACP Ibrahim Mahumi (Hayupo kwenye Picha) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yanayofanyika kila jumatatu katika eneo la Ofisi hiyo Mtumba, Dodoma. 

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma SACP. Ibrahim Mahumi akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI Mei 25, 2025 Mtumba, Dodoma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi (Aliyevaa Suti ya Blue) akiwa pamoja na Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Ummma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi (watatu kutokea kushoto) wakimsikiliza mwezeshaji (hayupo pichani) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo. 

Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakisikiliza mafunzo kutoka kwa mwezeshaji (hayupo pichani) Mei 25, 2026 katika eneo la ofisi hiyo iliyopo mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.







No comments:

Post a Comment