Saturday, June 17, 2023

SERIKALI YATOA RAI KWA WATUMISHI WA UMMA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Na. Lusungu Helela-Dodoma

Tarehe 17 Juni, 2023 

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetoa rai kwa Taasisi Simamizi na Vyama vya Kitaaluma kuhimiza na kuwasimamia watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.                     

Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha Watalaamu Waandamizi wa Taasisi Simamizi na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi. 

Bi. Shuli amesema kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi katika sekta ya afya, manunuzi, ujenzi pamoja na elimu ambayo yanahusu uvunjifu wa maadili, hivyo anaamini mafunzo hayo waliyoyapata kwa muda wa siku mbili yatasaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kufuatia hatua hiyo, Bi. Shuli amezitaka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma kujenga imani kwa wananchi na kuonesha thamani ya fedha zinazowekezwa na serikali katika miradi mbalimbali kwa kuwasimamia ipasavyo wataalamu wao katika utendaji kazi wao wa kila siku

‘’Ni matarajio yetu kupitia mafunzo haya tutakuwa na utumishi uliotukuka kwa kuwa na Watumishi wa Umma wenye kuzingatia weledi na wachapa kazi ili kuendelea kulinda taswira nzuri ya serikali ’’ amesema Mwakilishi wa Katibu Mkuu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Madilli kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika amesema kikao kazi hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja ya usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma pamoja na kujadili mikakati mbalimbali itakayowasaidia kusimamia suala la maadili kwa watumishi wa umma.

"Katika kuhakikisha suala hili linakuwa endelevu tumeweka mikakati ya pamoja kwa lengo la kuhakikisha suala la maadili katika utumishi wa umma linasimamiwa ipasavyo" amesisitiza Bi. Mavika.  

Naye Afisa Muuguzi kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Rehema Msanjila amesema mafunzo aliyoyapata yataenda kuleta mapinduzi makubwa katika eneo analolifanyika kazi ikizingatiwa sekta ya afya imekuwa ikilalamikiwa sana katika uvunjifu wa maadili.

“Nina imani kubwa kutokana na mikakati mikubwa tuliyojiwekea katika kikao hiki, tunakwenda kuwa na wauguzi na madaktari wenye kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali zetu hapa nchini’ amesema Bi. Msanjila.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli akizungumza Jijini Dodoma na Maafisa Waandamizi wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichozikutanisha Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma kwa lengo la kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.


Mkurugenzi  wa Usimamizi wa Madilli kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma , Bi.Leila Mavika akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Waandamizi kutoka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma kwa lengo la kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.

Sehemu ya Maafisa Waandamizi kutoka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma wakiwa katika kikao kazi kilichofanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dodoma kwa lengo la kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Usajili, Maadili na Leseni kutoka Baraza la Ukunga na Maadili Tanzania, Bi. Jane Mazigo akitoa neno la shukrani kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli baada ya kufunga kikao kazi cha Maafisa Waandamizi kutoka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.


Afisa Muuguzi kutoka Baraza la Ukunga na Maadili Tanzania, Bi. Rehema Msanjila akielezea faida walizozipata katika kikao kazi cha kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi na jinsi kitakavyoenda kuleta mapinduzi ya kimkakati.

 


 

No comments:

Post a Comment