Na. Lusungu
Helela-Dodoma
Tarehe 14 Juni, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewapongeza Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika maendeleo ya kidijitali huku akiwataka Watumishi hao kujiimarisha zaidi kwenye ubunifu.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amewaeleza watumishi hao kuwa Serikali inawategemea sana katika kipindi hiki cha uvumbuzi wa mifumo ya kidigitali ya kimkakati itakayosaidia katika utoaji huduma kwa wananchi wa ndani na nje ya nchi.
"Katika dunia ya sasa maendeleo ya nchi yamekuwa yakipimwa kwa kuangalia endapo nchi inatumia mifumo ya kidigitali katika kuendesha mambo yake" amesema Mhe.Simbachawene.
Aidha, Mhe.Simbachawene ameutaka uongozi wa eGa kuendelea kuwekeza kimkakati kwa watumishi kwa kuwawezesha kwenda kusoma katika nchi zilizopiga hatua zaidi kwenye masuala ya kidijitali.
"Nimeambiwa kuna baadhi ya watumishi wanasoma hapa nchini, natamani kuona idadi kubwa zaidi ya watumishi wanawake na wanaume wanakwenda kusoma nchi za nje hususani katika nchi zilizotuzidi kwenye masuala haya" amesisitiza Mhe.Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameitaka Mamlaka hiyo kujitangaza ipasavyo ambapo amesema, licha ya mifumo mingi ya kidigitali inayotumiwa na Taasisi za Serikali kubuniwa na Mamlaka hiyo na kupelekea kuokoa fedha nyingi za Serikali lakini Mamlaka hiyo haiyatangazi mafanikio hayo kwa Umma.
"Nataka mtoke muwaeleze Watanzania mmetekeleza kwa kiasi gani Ilani ya CCM (2020 - 2025) na pia mmeisaidia kwa kiasi gani Serikali katika kutumia mifumo ya kidigitali hususan katika kuwahudumia wananchi" Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza watumishi wa eGA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kubuni mifumo mbalimbali ya kidigitali yenye tija kwa taifa na kuwasisitiza kujitangaza zaidi ili wananchi wajue kwa kina shughuli zinazofanywa na Mamlaka hiyo.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utendaji katika utumishi wa umma huku akiwasisitiza kutunza siri katika mifumo ya kidigitali ambayo Serikali inaitumia katika kuwahudumia wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene
akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kikao kazi
kilichofayika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika kutekeleza
majukumu yao ambapo amewataka kujikita kwenye ubunifu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana
na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) mara baada ya kuwasili katika
kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji
katika kutekeleza majukumu yao.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza kabla
ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na watumishi wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao wakati wa kikao kazi kilichofayika jijini Dodoma kwa lengo la
kuhimiza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) katika kikao kazi kilichofayika jijini Dodoma kwa lengo
la kuhimiza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali
Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya taasisi yake kwa
viongozi wakuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora wakiongozwa na Waziri Mhe. George Simbachawene.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw.Juma Mkomi (katikati)
wakiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi
Benedict Ndomba mara baada ya kuwasili katika ofisi za eGA zilizopo jijini
Dodoma kwa ajili ya kikao kazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene (katikati) akiwa
kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao mara baada
ya kikao kazi huku akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa
pili kulia) pamoja na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Bw.Juma Mkomi (wa pili kushoto).
Sehemu ya watumishi wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene wakati wa kikao kazi
kilichofayika jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika kutekeleza
majukumu yao.
No comments:
Post a Comment