Sunday, May 28, 2023

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YATEKELEZA MAELEKEZO YA MHE. RAIS YA KUHUISHA MIUNDO YA MAENDELEO YA UTUMISHI YA KADA ZA MAKATIBU MAHSUSI NA WATUNZA KUMBUKUBU NA NYARAKA ITAKAYOANZA KUTUMIKA MWEZI JULAI, 2023

 Na. Veronica E. Mwafisi-Zanzibar

Tarehe 28 Mei, 2023

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhuisha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada za Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka ambayo itaanza kutumika Julai 1, 2023.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akitoa maelezo mafupi kwa Mhe. Rais wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar tarehe 27/05/2023.

Mhe. Simbachawene amesema pamoja na maelekezo ya kuhuisha muundo huo, Mhe. Rais pia alielekeza kukiwezesha na kukipa hadhi Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Tabora kuzalisha Makatibu Mahususi wenye viwango na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa ambapo Chuo hicho kimeboresha mitaala yake ambayo imeshaidhinishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) ambao utaanza kutumika kuanzia mwaka wa masomo wa 2023/24 unaoanza mwezi Oktoba, 2023.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa katika kushughulikia uhaba wa watumishi wa kada hizi mbili ndani ya Utumishi wa Umma, Serikali imetoa vibali 512 vya ajira mpya wa kada za Makatibu Mahsusi na nafasi 443 na ajira mpya kwa kada za Watunza Kumbukumbu na Nyaraka katika mwaka wa fedha 2022/23.

Pia, katika mwaka wa fedha 2023/24, Ofisi ya Rais-UTUMISHI imeidhinisha jumla ya nafasi 775 za ajira mpya za kada ya Makatibu Mahsusi na nafasi 930 za ajira mpya za kada za Watunza Kumbukumbu na Nyaraka.

Mhe. Simbachawene amesema kwa kutambua mchango wa kada hizi mbili katika ustawi wa Utumishi wa Umma, jumla ya watumishi 450 wa kada za Makatibu Mahususi wamepandishwa vyeo na kuidhinishiwa mishahara mipya kuanzia mwezi Mei, 2023 na watumishi wengine 462 wanarajiwa kuidhinishiwa vyeo na mishahara mipya mwezi Juni, 2023. Hivyo kufanya idadi ya Watumishi waliopandishwa vyeo kufikia 912.

Aidha, jumla ya Watunza Kumbukumbu 394 waliokasimiwa katika Ikama na Bajeti ya mwaka 2022/23 wameshapandishwa vyeo na kuidhinishiwa mishahara ya vyeo vipya mwezi Mei, 2023 na watumishi wengine 255 wanatarajiwa kuidhinishiwa vyeo na mishahara mipya mwezi Juni, 2023. 

Katika mkutano huo, zaidi ya Wanachama 7,943 wa TAPSEA na TRAMPA walikula kiapo cha uadilifu na Utunzaji wa Siri mbele ya Mhe. Rais kutokana na unyeti na umuhimu wa majukumu wanayoyatekeleza.

Mhe. Simbachawene amemshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake ya kukutanisha vyama hivi pamoja na kufanyia Mkutano Zanzibar ambapo imeongeza undugu na mshikamano kwa kada hizi mbili na Wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Amemhakikishia kuwa, Serikali zote mbili kupitia Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora – Zanzibar na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ya JMT itaendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wa TRAMPA na TAPSEA, kusimamia utendaji kazi wa Watalaamu wa kada hizi mbili pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kisera, Kitaaluma na kiutendaji ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Mkutano huo wa pamoja umefanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya Vyama hivi viwili kwa lengo la kudumisha mshikamano wa kada hizi mbili kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akitoa maelezo mafupi kwa    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu mkutano wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.


Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wapili kutoka kushoto) akifurahia jambo kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhitimisha kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa utambulisho wa Viongozi na Watendaji wa Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.

 


Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakila kiapo cha Uadilifu mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar.

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (aliyenyoosha kidole) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Bw, Idrisa Mustafa (wapili kutoka kushoto) na Naibu Katibu Mkuu, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Bw. Omar Gora (wakwanza kulia) kabla ya kuhitimishwa kwa kilele cha Mafunzo ya Uadilifu kwa Wanachama wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika Zanzibar. Wakwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.



 

No comments:

Post a Comment