Sunday, May 7, 2023

WATUMISHI HOUSING YAPONGEZWA KUJENGA NYUMBA ZA BEI NAFUU ZAIDI YA 900 KWA AJILI YA KUWAUZIA NA KUWAPANGISHA WATUMISHI WA UMMA

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 07 Mei, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameipongeza Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kujenga nyumba za gharama nafuu zaidi ya 900 nchini kwa ajili ya kuwauzia na kuwapangisha Watumishi wa Umma na wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata makazi bora ya kuishi yatakayowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Simbachawene ametoa pongezi hizo alipoitembelea Watumishi Housing Investments jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuihimiza taasisi hiyo kuendelea kujenga nyumba za gharama nafuu ili watumishi wa umma nchini waondokane na changamoto ya kukosa nyumba za kuishi karibu na vituo vyao vya kazi jambo ambalo limekuwa likikwamisha azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa, pamoja na Watumishi Housing kukabiliana na changamoto ya kukosa mtaji unaokidhi mahitaji ya nyumba za watumishi nchini lakini wameweza kujenga nyumba zaidi ya 900 ambazo zinaendana na lengo la Serikali la kuianzisha Watumishi Housing ili kuwawezesha watumishi wa umma nchini kupata nyumba za kuishi kwa gharama nafuu.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, Watumishi Housing wamejitahidi kutekeleza jukumu la kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma, japo bado wana jukumu kubwa la kujenga katika maeneo mengine nchini kwani watumishi wa umma hawapo Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza pekee bali wapo hadi vijijini,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema Watumishi Housing imeanzisha Mfuko wa Pamoja (FAIDA FUND) ambao umetoa fursa kwa wadau na wananchi kununua vipande ili kuwekeza kwenye mfuko huo ambao mpaka hivi sasa una mtaji wa bilioni 12.7 na thamani ya bilioni 15 na kuongeza kuwa, uanzishwaji wa mfuko huu ni sehemu ya kuiongezea nguvu Watumishi Housing katika kutekeleza jukumu lake la msingi la kuendelea kujenga nyumba za gharama nafuu zitakazoweza kupangishwa au kununuliwa na watumishi wa umma.

Akizungumzia changamoto ya bajeti katika utekelezaji wa jukumu la kujenga nyumba za gharama nafuu, Mhe. Simbachawene amesema Serikali ndio yenye watumishi hivyo, itafanya linalowezekana kuiongezea WHI fedha za maendeleo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa makazi ya watumishi wa umma.

“Mtumishi wa umma akiwa anaishi katika makazi yaliyo bora na jirani ya kituo cha kazi itamsaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,” Mhe. Simbachawene amefafanua.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing Investments, Dkt. Fred Msemwa amesema wamepokea maelekezo ya Mhe. Simbachawene ya kuongeza wigo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini ili kuwafikia watumishi wengi zaidi, hivyo wamejipanga kutekeleza agizo hilo ikizingatiwa kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua stahiki kuiwezesha taasisi yake kuwa na mtaji mkubwa utakaowezesha kujenga nyumba nyingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, akizungumza na Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) jijini Dar es Salaam alipotembelea taasisi hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing (WHI) akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, wakati Waziri huyo alipotembelea taasisi hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

                                                

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing (hayupo pichani) alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Waziri huyo alipofanya ziara ya kuhimiza uwajibikaji kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisisitiza jambo kwa Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) jijini Dar es Salaam, alipotembelea taasisi hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akielekeza jambo kwa Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt. Fredy Msemwa, alipotembelea mradi wa nyumba ya ghorofa iliyojengwa na taasisi hiyo kwa ajili ya kuwauzia na kuwapangisha watumishi wa umma.

 

 

Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing (WHI) Dkt. Fredy Msemwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, kuhitimisha ziara ya kuitembelea taasisi hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment