Wednesday, May 17, 2023

WAAJIRI WATAKIWA KUWARUHUSU MAKATIBU MUHSUSI NA WATUNZA KUMBUKUMBU KUSHIRIKI MKUTANO UTAKAOWAJENGEA UWEZO KIUTENDAJI KUTIMIZA DHAMIRA YA MHE. RAIS YA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 16 Mei, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka waajiri katika Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuwaruhusu na kuwawezesha Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma Zanzibar uliolenga kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa watanzania pamoja na kuleta maendeleo katika taifa.

Mhe. Simbachawene ametoa wito huo Jijini Dodoma, wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari wenye lengo la kuwahimiza waajiri nchini kuwaruhusu Makatibu Muhsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza ufanyike Zanzibar.

Mhe. Simbachawene amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi unakuwa uliotukuka na wenye lengo la kuwahudumia wananchi, hivyo amewahimiza waajiri kuwaruhusu Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano huo wa kitaaluma ili wapate ujuzi na maarifa ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

“Mheshimiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa kada hizi za Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu katika utendaji wa shughuli za Serikali na Sekta Binafsi, alielekeza ufanyike mkutano mkubwa wa kitaaluma Zanzibar ili wapate fursa ya kula kiapo cha uadilifu na kujadili namna ya kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Mhe. Simbachawene amewahimiza waajiri katika sekta ya umma kuhakikisha idadi kubwa ya Makatibu Mahususi na Watunza Kumbukumbu wanashiriki mkutano huo na kugharamiwa, ili ushiriki wao uwe na tija kiutendaji pindi watakaprejea katika maeneo yao ya kazi.

Mhe. Simbachawene amesema mkutano huo utafanyika katika Viwanja vya Mao Tse Tung Zanzibar katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kaulimbiu ya mkutano huo ni Nidhamu, Uadilifu na Utunzaji Siri Sehemu za Kazi ni Chachu ya Maendeleo Kitaaluma” ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema kuwa, maandalizi ya mkutano huo kwa kiasi kikubwa yamekamilika kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hivisasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha maandalizi ili washiriki wote wanaokadiriwa kuwa 8000 wawe na ukakika wa kupata huduma za malazi na usafiri pindi watakapokuwa wakishiriki mkutano huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka (TRAMPA) uliofanyika  tarehe 27/11/2022      Jijini Arusha, alielekeza ufanyike mkutano wa pamoja Zanzibar wa TAPSEA na TRAMPA  utakaowawezesha kubadilishana uzoefu kiutendaji na kuweka mikakati endelevu na madhubuti ya kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) na Watendaji wa ofisi yake jijini Dodoma kuhusu Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma Zanzibar.


Sehemu ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma Zanzibar.



Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu Makatibu Mahsusi na Watunza Kumbukumbu kushiriki mkutano wa kitaaluma Zanzibar.



No comments:

Post a Comment