Tuesday, May 16, 2023

MAAFISA UCHUNGUZI WANAFUNZI WA TAKUKURU WAASWA KUPAMBANA NA WATU WANAOIUMIZA JAMII KWA VITENDO VYA RUSHWA ILI KULINDA MASLAHI YA NCHI


Na. Veronica E. Mwafisi-Moshi

Tarehe 16 Mei, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewaasa Maafisa Uchunguzi Wanafunzi wa TAKUKURU kuichukia rushwa na kupambana na watu wanaoiumiza jamii kwa vitendo vya rushwa ili kulinda maslahi ya nchi kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Simbachawene amesema hayo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati akifungua mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi na wanaotarajiwa kuanza mafunzo hayo ya TAKUKURU katika Shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi yenye lengo la kuwajengea uwezo washiriki hao kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Mhe. Simbachawene amesema Maafisa hao wanafunzi wa TAKURURU wanatakiwa kujua kazi waliyoichagua kuwa ni ya kupambana na vitendo vya rushwa na kutokomeza kabisa vitendo hivyo bila woga.

Mhe. Simbachawene amewasisitiza maafisa hao, kufanya kazi mahali popote katika vituo vya kazi watakavyopangiwa mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo kwani huo ndio uzalendo.

Kafanyeni kazi popote mtakapopangiwa ni kazi inayohitaji uzalendo wa hali ya juu, nendeni mkawe mfano wa kuigwa kutokana na tabia njema na kutetea maslahi ya watu wanyonge kwa maslahi ya nchi yetu ili tujenge amani na utulivu,” Mhe. Simbachawene amesema.

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajali wananchi wake, hivyo hakuna budi kumuunga mkono katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bila kunyanyasika na pasipo mianya  yoyote ya rushwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amesema mafunzo hayo ya Maafisa Uchunguzi yamegawanyika katika sehemu kuu mbili yakiwemo mafunzo ya vitendo na nadharia ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Mkurugenzi Hamduni amesema, mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi hao yatahusu zaidi katika kutoa mbinu mbalimbali za ulinzi, ukakamavu, uzalendo, utii na nidhamu.

Naye, Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania, SACP Ramadhani Mungi, amewashukuru wakufunzi wote kwa kushirikiana na shule hiyo kwani wanategemea wanafunzi hao wakimaliza mafunzo hayo wataitumikia nchi kwa kiwango cha hali ya juu kutokana na elimu watakayoipata shuleni hapo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Maafisa Uchunguzi wanafunzi wa TAKUKURU (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo ya awali kwa Maafisa hao katika Shule ya Polisi Tanzania, mjini Moshi.


Sehemu ya wanafunzi wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi wa TAKUKURU wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akifungua mafunzo hayo mjini Moshi katika Shule ya Polisi Tanzania.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipokea salamu kutoka kwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati alipowasili katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi kwa lemgo la kufungua mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi wa TAKUKURU.


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni akielezea lengo la mafunzo ya Maafisa Uchunguzi wa TAKUKURU wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua mafunzo hayo.


Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania SACP Ramadhani Mungi akitoa salamu za shule hiyo kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa TAKUKURU mjini Moshi. 


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu akitoa salamu za mkoa wake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wa TAKUKURU mjini Moshi katika Shule ya Polisi Tanzania


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja baada ya kufungua mafunzo ya awali kwa Maafisa Uchunguzi wa TAKUKURU katika Shule ya Polisi Tanzania, mjini Moshi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni na kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu.


 

No comments:

Post a Comment