Saturday, May 6, 2023

VIONGOZI WANAWAKE WALIOHITIMU MAFUNZO YA UONGOZI WATAKIWA KUJIAMINI NA KUFANYA KAZI KWA UFANISI ILI KUWAHUDUMIA WANANCHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 06 Mei, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Watumishi wa Umma wanawake waliohitimu Programu ya Mafunzo kwa Viongozi Wanawake inayotolewa na Taasisi ya UONGOZI, kujiamini na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mhe. Simbachawene ametoa wito huo, kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu hao wa mafunzo ya uongozi kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa mahafali ya sita ya Programu za Uongozi inayotolewa na Taasisi ya UONGOZI.

Mhe. Simbachawene amewaasa watihimu hao wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake, kuhakikisha wanafanya kazi kwa kushirikiana na wanaume katika maeneo yao ya kazi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema ukiwa kiongozi mwanamke haimaanishi jukumu lako ni kuwasaidia wanawake wenzio bali ni kuutumikia umma bila kujali jinsia na kuongeza kuwa, hakuna mwanamke aliyefanikiwa bila mchango wa mwanaume na hakuna mwanaume aliyefanikiwa bila mchango wa mwanamke.

“Viongozi wanawake na wanaume mkishirikiana kiutendaji nina hakika mtatumia maarifa mliyoyapata katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yenu ya kazi na hatimaye kutoa mchango katika maendeleo ya taifa,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Mhe. Simbachawene ametoa rai kwa wahitimu hao wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake, kuwa kitendo cha Serikali kuwawezesha kielimu isiwe sababu ya kuibua jeuri na majivuno pindi wanapopewa nyadhifa za uongozi na kuongezewa kipato kwani watakuwa wameharibu dhana halisi ya kujengewa uwezo.

Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa, lengo la Serikali ni kuwa na viongozi wanawake watakaokuwa ni chachu ya kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa na kuongeza kuwa, Serikali inayo imani kwamba wanawake walioelimika ni chachu ya maendeleo yenye tija kwa jamii nzima.

“Ni matumaini yangu kwamba mafunzo mliyoyapata yatakuwa ni chachu ya mabadiliko chanya katika maeneo yenu ya kazi kwani mtakwenda kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizopo katika Utumishi wa Umma,” Mhe. Simbachawene amehimiza.

Sanjari na hilo, amewataka kuongeza ubunifu na kuimarisha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kuujenga Utumishi wa Umma utakaokuwa na tija na manufaa kwa wananchi na maendeleo ya taifa.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa Programu ya Uongozi kwa Wanawake, Bi. Mwanaani Mtoo, ameishukuru Menejimenti ya Taasisi ya UONGOZI kwa kuanzisha programu hiyo ya mafunzo ambayo imewawezesha kupata ujuzi na maarifa yatakaboresha utendaji kazi wao kama viongozi wanawake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya UONGOZI, Balozi Ombeni Sefue amewataka viongozi hao wanawake waliohitimu mafunzo ya uongozi kwenda katika maeneo yako ya kazi na kutatua changamoto zinazoikabili jamii hususani katika eneo la utoaji wa huduma kwani wameiva kiuongozi kupitia mafunzo waliyopatiwa na taasisi yake.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya uongozi (hawapo pichani) wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi zinazotolewa na Taasisi ya UONGOZI alipomuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika mahafali hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.


 

Sehemu ya wahitimu wa mafunzo ya uongozi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kabla ya Waziri huyo kuwatunuku vyeti wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi zinazotolewa na Taasisi ya UONGOZI.


 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI akitoa neno la utangulizi wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi yanayotolewa na taasisi yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) kuwatunuku vyeti wahitimu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya UONGOZI Balozi Ombeni Sefue akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) mara baada ya Waziri huyo kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi katika Mahafali ya Sita ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

 

Mwakilishi wa wahitimu wa programu ya mafunzo kwa viongozi wanawake Bi. Mwanaamani Mtoo, akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzie kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuwatunuku vyeti wahitimu katika Mahafali ya Sita ya Taasisi ya UONGOZI yaliyofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akimtunuku cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya uongozi wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya wahitimu wa Programu ya Mafunzo kwa Viongozi Wanawake inayotolewa na Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.  

 

 

Sehemu ya wahitimu wa mafunzo ya uongozi wakionesha vyeti walivyotunikiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa mahafali ya sita ya programu za mafunzo ya uongozi yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.  


No comments:

Post a Comment