Wednesday, November 30, 2022
Tuesday, November 29, 2022
MHE. NDEJEMBI AWAASA WATUNZA KUMBUKUMBU SERIKALINI KUTUNZA SIRI KAMA MHE. RAIS ALIVYOELEKEZA
Na. James K. Mwanamyoto-Arusha
Tarehe 29 Novemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amekemea kitendo cha baadhi ya Watunza Kumbukumbu Serikalini kuvujisha siri katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kutunza siri kama Mhe. Rais alivyowaelekeza wakati akifungua mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Watunza Kumbukumbu hao.
Mhe. Ndejembi amewaasa Watunza Kumbukumbu hao jijini Arusha, wakati akifunga mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA).
Mhe. Ndejembi amesema, sababu ya msingi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwahimiza wanataaluma ya utunzaji wa kumbukumbu kutunza siri, inatokana na unyeti wa kazi yao kwani kumbukumbu na nyaraka wanazotakiwa kuzitunza zinatumika kuendesha shughuli za Serikali za kila siku, ikiwa ni pamoja na kufanyia maamuzi yenye maslahi kwa taifa.
“Niwaombe sana mzingatie utunzaji wa siri kwani kumekuwa na matukio ya barua za vibali vya uhamisho kuvuja kupitia masijala kabla ya kuifikia taasisi husika na mlengwa au taarifa za mtumishi anayepata uhamisho wa ndani kuvuja katika taasisi yake kabla ya yeye mwenyewe kupata barua ya uhamisho wake hivyo, muache tabia hiyo ambayo ni kinyume na taratibu za kiutumishi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa, ofisi yake imeshatoa maelekezo kwa waajiri na mamlaka husika kuboresha mazingira ya kazi ya Watunza Kumbukumbu, hivyo ana imani kwamba watumishi hao katika utendaji kazi wao wa kila siku watazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utunzaji siri katika maeneo yao ya kazi.
Mhe. Ndejembi amemtaka kila Mtunza Kumbukumbu Serikalini kuendelea kuwa muadilifu katika eneo la utunzaji wa siri hata ikitokea ni jambo linalomhusu rafiki, ndugu au mtu wake wa karibu.
Akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Ndejembi, Mlezi wa TRAMPA Bw. Charles Magaya ameahidi kuwa chama hicho kitasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa ili siri za utendaji kazi serikalini zisivuje, na kuongeza kuwa TRAMPA inaishukuru Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa kutoa msaada wa kitaalam kwa Watunza Kumbukumbu ili kuwajengea uwezo kiutendaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi amesema idara yake pamoja na TRAMPA imepokea maelekezo ya Mhe. Rais ya uzingatiaji wa maadili pindi wanapotoa huduma kwa wananchi na kumuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, watahakikisha wanayatekeleza kwa vitendo maelekezo hayo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofungwa na Mhe. Ndejembi umefanyika jijini Arusha kwa siku 3 ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa kwa wanataaluma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi katika utendaji kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watunza Kumbukumbu wakati akifunga mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Arusha.
Sehemu ya washiriki wa mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akifunga mkutano wao jijini Arusha.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi kabla ya Mhe. Ndejembi kuufunga mkutano mkuu wa 10 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Arusha.