Saturday, June 18, 2022

VIONGOZI TAKUKURU WEKENI JITIHADA KUBWA KUZUIA NA KUDHIBITI VITENDO VYA RUSHWA NCHINI – Mhe. Ndejembi


Na. James K. Mwanamyoto-Kibaha

Tarehe 18 Juni, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuweka jitihada kubwa na madhubuti katika kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa nchini kwa manufaa na maendeleo ya taifa.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo wilayani Kibaha, wakati akifunga mafunzo ya uchunguzi kwa viongozi waandamizi wa TAKUKURU yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo wilayani humo.

Mhe. Ndejembi amewataka viongozi hao wa TAKUKURU kuwa na jicho la ziada litakalobaini viashiria vya uwepo wa vitendo vya rushwa katika jamii, ili kuzuia rushwa isitokee kwani rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Ni muhimu kwenu nyote kuwa na jicho la ziada katika kupambana na rushwa kwani kuna maeneo kwa mfano juzi nilikuwa Geita, nimekuta kuna hosteli moja imejengwa kwa shilingi 150,000,000/= lakini ndani ya mkoa huo huo kuna nyingine imejengwa kwa shilingi 128,000,000/= hivyo mkifuatilia na kuwa karibu na miradi inayotelelezwa na Serikali mnaweza kuzuia ubadhirifu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Sanjari na hilo, amewata viongozi hao wa TAKUKURU kusimamia ipasavyo uzingatiaji wa sheria za nchi, taratibu za utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU na kanuni zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa, hatarajii kuona viongozi hao wakiiacha TAKUKURU iende kinyume na maelekezo ya kuzuia vitendo vya rushwa yanayotolewa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Jenista Mhagama, yeye mwenyewe pamoja Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ambao Mhe. Rais amewapa dhamana ya kumsaidia kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi Salum Hamduni amesema mafunzo hayo ya uchunguzi kwa viongozi waandamizi wa TAKUKURU (Senior Investigation Course) ni ya kimuundo na yamefanyika kwa viongozi 40 kwa muda wa wiki mbili. 

Kamishna Hamduni amesema kuwa, mafunzo hayo ya kimuundo ni muhimu kwa viongozi hao kwani yatawasaidia kuhakikisha wanatekeleza jukumu la kuwasimamia watumishi walio chini yao ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu yao kama viongozi wenye dhamana ya kuhakikisha TAKUKURU inatekeleza jukumu lake la msingi ambalo ni kuzuia vitendo vya rushwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na viongozi waandamizi wa TAKUKURU wakati akifunga mafunzo ya uchunguzi kwa viongozi hao yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

 

Viongozi waandamizi wa TAKUKURU wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga mafunzo ya uchunguzi kwa viongozi hao yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamisha wa Polisi, Salum Hamduni akitoa taarifa ya mafunzo ya uchunguzi yaliyowashirikisha viongozi waandamizi wa TAKUKURU kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga mafunzo hayo kwa viongozi hao katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

 

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimkabidhi cheti mmoja wa viongozi wa TAKUKURU aliyeshiriki mafunzo ya uchunguzi yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TAKUKURU walioshiriki mafunzo ya uchunguzi kwa viongozi waandamizi yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

 

 

No comments:

Post a Comment