Na. James K. Mwanamyoto-Kondoa
Tarehe 14 Juni, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ametoa siku moja kwa Mtendaji wa Kijiji cha Bukulu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha mlengwa wa TASAF kijijini humo, Bw. Laurent Chebu anapewa ruzuku yake na kumpatia taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo
wakati akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Bukulu
wilayani Kondoa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo.
Mhe. Jenista amesema akiwa katika
ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya TASAF hupenda kusikiliza shuhuda za
walengwa pamoja na changamoto zinazowakabili, hivyo baada ya kusikia changamoto
ya Bw. Laurent Chibu kutopata ruzuku ameamua kutoa maelekezo kwa Mtendaji wa Kijiji
ili mlengwa huyo apate haki yake.
“Mtendaji nimekuuliza hapa na
umekiri kwamba Bw. Laurent Kibu hajapata ruzuku yake kwasababu yeye na mwenzeke
walikuwa safarini, hivyo nikupa muda wa kushughulikia suala hili mpaka kesho
jioni na unipigie simu wewe mwenyewe kunieleza kuwa mlengwa huyu ameshapewa na
wengine ambao bado wapewe ruzuku zao,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Waziri Jenista amewataka watendaji
na waratibu wa TASAF kote nchini kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa
ajili ya walengwa wa TASAF zinawafikia walengwa kwa wakati, kama ambavyo
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
ilivyokusudia.
Katika kuhakikisha ruzuku inawafikia
walengwa kwa wakati, Mhe. Jenista amewataka walengwa wa TASAF kujisajili kwenye
mfumo wa kidigitali wa simu ili waweze kuhawilishiwa ruzuku zao kupitia
mitandao ya simu, na hatimaye kuondokana na changamoto ya kutopokea ruzuku zao
kwa wakati.
“Watendaji na waratibu wa TASAF nisingependa
kusikia mlengwa wa TASAF hajapewa ruzuku yake, iwe kwasababu ya kutokuwepo
wakati wa dirisha au sababu nyingine yoyote ile kwani lengo la TASAF ni
kuwawezesha walengwa kuboresha maisha yao,” Mhe. Jenista amefafanua.
Akieleza namna TASAF ilivyoboresha
maisha yake, mlengwa wa TASAF wa Kijiji cha Bukulu, Bi. Rukia Kasi amesema
ruzuku aliyoipata imemuwezesha kununua mbuzi na kuku wa kufuga, kusomesha
watoto pamoja na kukarabati nyumba anayoishi na mme wake ambaye ni mlemavu wa
macho.
Mlengwa mwingine wa TASAF wa Kijiji
cha Bukulu, Bi. Mwanaidi Dohu amesema kuwa TASAF imemuwezesha kununua ng’ombe,
kujenga nyumba ya kuishi, kuchimba kisima cha maji na kujishughulisha na kilimo
cha migomba.
Naye, Bw. Abdilahi Ally ambaye ni
mlengwa wa TASAF Kijiji cha Bukulu amesema licha ya ulemavu wake TASAF
imemuwezesha kusomesha watoto wanne waliohitimu kidato cha nne na mmoja
amemaliza kidato cha sita hivyo anaishukuru Serikali kupitia TASAF kwa
kumuwezesha kumudu gharama za kuwasomesha watoto wake.
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii (TASAF) katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetoa kiasi cha shilingi
bilioni 2.6 katika Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru
Kaya Maskini wilayani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Bukulu wilayani Kondoa wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani
humo.
Walengwa wa TASAF na wananchi wa
Kijiji cha Bukulu wilayani Kondoa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani
humo.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Hamis
Mkanachi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama
kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Bukulu wilayani humo
wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani humo.
Mlengwa wa TASAF Kijiji cha Bukulu,
Bw. Laurent Chebu akiwasilisha hoja yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wakati
akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Bukulu wilayani
Kondoa wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani humo.
Mlengwa wa TASAF wa Kijiji cha Bukulu
wilayani Kondoa, Bi. Rukia Kasi akieleza namna TASAF ilivyomuwezesha kuboresha
maisha yake.
Mlengwa wa TASAF wa Kijiji cha
Bukulu wilayani Kondoa, Bw. Abdilahi Ally akieleza namna TASAF ilivyomuwezesha
kuboresha maisha yake.
No comments:
Post a Comment