Tarehe 23 Juni, 2022
Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wamefanya usafi katika Kituo Kikuu cha Mabasi jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, 2022 pamoja na kutekeleza kwa vitendo Kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE ambayo imekuwa ni chachu ya kuleta maendeleo katika taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akiwa katika eneo
la Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma ambapo amewaongoza watumishi wa idara yake
kufanya usafi katika kituo hicho.
Bw. Msiangi amesema kuwa, idara yake
imeshiriki kufanya usafi katika eneo hilo kuungana na wananchi katika shughuli
za kijamii kwani usafi ni muhimu na ni sehemu ya utekelezaji wa Kaulimbiu ya
Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE ambayo ni dira ya mafanikio katika sekta zote.
“Leo tumekuja hapa kufanya usafi
katika stendi hii kuu ya Mabasi Dodoma ili kuliweka jiji la Dodoma katika hali
ya usafi kwani mazingira ni afya, na ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya
KAZI IENDELEE,” Bw. Msiangi amesisitiza.
Aidha, Bw. Msiangi amesema, shughuli
hiyo ya usafi waliyoifanya ni utekelezaji wa maelekezo ya Katibu Mkuu-UTUMISHI,
Dkt. Laurean Ndumbaro aliyezitaka taasisi zote za umma nchini kuadhimisha Wiki
ya Utumishi wa Umma, 2022 kwa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ili
kujenga mahusiano mazuri na umma.
“Pamoja na kufanya kazi zetu za msingi maofisini, Katibu Mkuu-UTUMISHI alitutaka tushirikiane na wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii ili kuleta tija kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuendeleza jitihada za Mhe. Rais za kuijali jamii,” Bw. Msiangi amefafanua.
Kwa upande wake, mmoja wa watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bi. Joyce Maro amesema, wamefanya usafi katika stendi kuu ya mabasi Dodoma ili kuweka mazingira safi yatakayowaepusha wananchi na magonjwa mbalimbali, kama ambavyo Mhe. Rais amekuwa akisisitiza usafi wa mazingira ili kuwa na taifa la watu wenye afya bora watakaoshiriki shughuli za maendeleo.
Naye, Afisa Habari wa Kituo Kikuu
cha Mabasi Dodoma, Bi. Qeen Mwasunga amesema, menejimenti ya kituo chake
imefurahishwa na kitendo cha watumishi wa Idara ya Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa kufanya usafi kwenye eneo la kituo hicho jambo ambalo
limemkumbusha ushiriki wa usafi wa mazingira, hivyo ametoa wito kwa taasisi
nyingine kushiriki shughuli za mbalimbali za kijamii.
Mkurugenzi wa
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi akieleza azma ya
idara yake kufanya usafi eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma kama sehemu ya
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, 2022.
Baadhi ya
watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa wakifanya usafi eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma ikiwa ni
sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, 2022.
Mtumishi wa Idara
ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bi. Joyce Maro katika kufanya usafi eneo la
Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma, 2022.
Afisa Habari wa Kituo Kikuu cha
Mabasi Dodoma, Bi. Qeen Mwasunga akiwashukuru watumishi wa Idara ya Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa kwa kufanya usafi kwenye eneo la kituo hicho ikiwa ni sehemu
ya mchango wao katika jamii.
No comments:
Post a Comment