Wednesday, June 22, 2016

WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2016:MATUKIO KATIKA PICHA MKOANI ARUSHA

Mwakilishi wa chama cha wafanyakazi akiuliza swali wakati wa kikao mkoani Arusha.
Watumishi waliohudhuria mkutano kazi wa Wiki ya Utumishi wa Umma 2016 mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri wa Nchi-Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb) hayupo pichani
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akitoa maelekezo kwa watendaji wa mkoa wa Arusha wakati wa kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma 2016, mjini Arusha. 

Mmoja wa Watumishi akiwasilisha kero kuhusu hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Katibu Tawala, mkoa wa Arusha Bw. Richard Kwitega akiwakaribisha watumishi wa umma mkoani Arusha katika kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma 2016, lengo likiwa kuwasilisha kero na maoni kuhusu Utumishi wa Umma.
“Fursa za Mafunzo Zisiwe Siri” MHE. KAIRUKI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewaelekeza waajiri kuhakikisha kuwa fursa za mafunzo zinakuwa wazi na kujulikana kwa Watumishi wa Umma ili kuepuka malalamiko.
Waziri Kairuki alisema hayo wakati wa kikao kazi cha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2016 kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha katika muda tofauti. Kikao kilihusisha watumishi wa umma katika mikoa hiyo, ikiwa ni pamoja na kusikiliza maoni na kero zinazowakabili.
“Fursa za mafunzo zikijulikana kwa kila mtu zitaepusha malalamiko ya baadhi ya watu kurudia kwenda katika mafunzo wakati wengine bado” Mhe. Kairuki alisema na kuongeza, lazima mpango wa mafunzo kwa kila taasisi uzingatiwe ipasavyo.
Waziri Kairuki aliongeza, Maofisa Rasilimaliwatu wanalo jukumu la kuhakikisha wanawahudumia watumishi wa umma ipasavyo, kwa kusikiliza changamoto wanazozipata katika maeneo ya kazi na kuzitatua kama mikataba ya huduma kwa mteja na mwongozo wa kushughulikia malalamiko ulivyoelekeza.
Aidha, aliwaelekeza Maofisa utumishi  kuhakikisha wanamaliza zoezi la kusafisha taarifa chafu katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) ili kubaki na majina ya watumishi wanaostahili wakiwa na takwimu safi, zisizo na shaka.
Alisema kwa wale ambao watabainika kucheza na mfumo ili kudanganya au kuzembea hatua za kinidhamu zitachukuliwa mara moja dhidi yao.
Waziri Kairuki aliwahakikishia watumishi kuwa ajira zao ni salama, na wale wanaoenda kinyume na maadili watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu zilizopo.
Kuhusu vitambulisho na fomu za wazi za mapitio na tathmini ya kazi (OPRAS) Waziri Kairuki alielekeza kila mwajiri kuhakikisha anawahudumia watumishi na sio kuuza nyaraka hizo. Kila mwajiri ahakikishe watumishi katika eneo lake wanapata vitambulisho na fomu za OPRAS bila usumbufu au kuingia gharama yoyote.
Waziri Kairuki anaendelea na vikao kazi na Watumishi wa Umma katika mkoa wa Manyara kusikiliza kero na maoni kuhusu Utumishi, ikiwa ni moja ya matukio katika Wiki ya Utumishi wa Umma 2016.

***********************************MWISHO***************************************




No comments:

Post a Comment