Tuesday, November 15, 2022

MHE. NDEJEMBI AKEMEA TABIA YA WAAJIRI SERIKALINI KUFICHA BARUA ZA UHAMISHO WA WATUMISHI WA UMMA ZILIZORIDHIWA NA MAMLAKA

Na. Veronica E. Mwafisi-Kigoma

Tarehe 15 Novemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya waajiri katika Taasisi za Umma kuficha barua za uhamisho wa watumishi wa umma ambao Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameridhia na kutoa kibali cha uhamisho ili wakautumikie umma katika maeneo mengine ya nchi ambayo mamlaka imeona kuna uhitaji.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ndejembi amesema, waajiri na Maafisa Utumishi wanapaswa kutenda haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya kupatiwa kibali cha uhamisho na mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, na si kufichiwa barua zao za uhamisho kwa lengo la kukwamisha mchakato wa uhamisho.

 “Waajiri na Maafisa Utumishi tendeni haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya uhamisho wao kuridhiwa na mamlaka, tusifiche barua zao kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na mamlaka na ni kinyume cha Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, wapo watumishi wa umma ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi, hivyo mamlaka kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu-UTUMISHI ikaamua kumpeleka mtumishi huyo katika eneo lingine la kazi ili abadili mazingira ya kazi ambayo yatamuongezea ufanisi kiutendaji, lakini baadhi ya waajiri hukwamisha uhamisho huo wakati mamlaka iliridhia baada ya kufanya uchambuzi yakinifu.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutopitisha barua za kuomba uhamisho za watumishi ambao ni ajira mpya, kwani ajira zao hazina muda mrefu na baadhi yao wanakuwa hawajathibitishwa kazini, hivyo kutotimiza kigezo cha kutumikia miaka mitatu tangu waajiriwe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.

Mhe. Mahawe, amewahimiza watumishi wa umma walio katika eneo lake la utawala, kufanya kazi kwa bidii na weledi kama alivyoelekeza Mhe. Ndejembi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya KAZI IENDELEE ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ujiji, ambaye ni Afisa Utumishi, Bw. Stafordi Bidebuye amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.

Mhe. Bidebuye amesema kupitia elimu ya masuala ya kiutumishi waliyoipata kutoka kwa Mhe. Ndejembi, anaamini Mkoa wa Kigoma utafunguka katika kila sekta na kupata maendeleo chini ya uongozi makini wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji (hawapo pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika halmashauri hizo.


Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hizo.


Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji (hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika halmashauri hizo.


Afisa Mifugo, Kilimo na Uvuvi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. Evans Mdee akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Manispaa ya Kigoma, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo. Kushoto kwake ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Bw. Ntime Mwalyambi na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Ester Mahawe.




 

  

Thursday, November 10, 2022

MHE.JENISTA NA MHE. KAIRUKI WAWEKA MKAKATI KUTEKELEZA MAELEKEZO YA MHE. RAIS YA KUIMARISHA MAADILI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 10 Novemba, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wamefanya kikao kazi cha kujadili namna ya kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha maadili katika utumishi wa umma aliyoyatoa wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 mkoani Kagera.

Akiongoza kikao kazi hicho, Mhe. Mhagama amesema, wameona ni vema wakakutana pamoja na watendaji wa ofisi zao ili kuwa na mtazamo wa pamoja na mkakati madhubuti utakaowezesha kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuimarisha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma ili uwe na tija katika usimamizi wa miradi ya maendeleo nchini. 

Mhe. Mhagama amesema, kikao kazi hicho kitatoa mwelekeo wa namna  TAKUKURU itakavyotekeleza jukumu la kuzuia  na kupambana na vitendo vya rushwa ili visiathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kutafuta fedha kwa wadau wa maendeleo ili ziwanufaishe wananchi. 

“Mhe. Rais amekuwa akitafuta fedha kwa hali na mali ili ziwanufaishe wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa ofisi yangu na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” Mhe. Mhagama amesisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki amesema kikao kazi hicho kitawezesha kuwa na Rasilimialiwatu yenye uwezo wa kusimamia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwa na mifumo imara ya usimamizi wa fedha hizo. 

Mhe. Kairuki ameongeza kuwa, Ofisi yake itashirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kusimamia maadili ya watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo. 

Akiwasilisha mpango kazi wa namna ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais katika mapambano dhidi ya rushwa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Neema Mwakalyelye amesema TAKUKURU imeandaa programu ya TAKUKURU RAFIKI inatakayowawezesha wananchi kushiriki katika kuzuia vitendo vya rushwa.

Bi. Mwakalyelye ameongeza kuwa, programu hiyo shirikishi ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni itawajengea uwezo wananchi katika kutambua miradi ya maendeleo iliyopo, kubaini mianya ya rushwa ili kuhakikisha fedha za umma hazipotea na zinatumika katika kuleta maendeleo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiongoza kikao kazi leo jijini Dodoma kilichowakutanisha watendaji wa Ofisi yake na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki akizungumza kwenye kikao kazi leo jijini Dodoma kilichowakutanisha watendaji wa Ofisi yake na Ofisi ya Rais-UTUMISHI ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakiwa katika kikao kazi na watendaji wa ofisi zao leo jijini Dodoma ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akiwasilisha mpango kazi wa namna Taasisi yake itakavyotekeleza maelekezo ya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Neema Mwakalyelye akiwasilisha mpango kazi wa namna ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa kikao kazi leo jijini Dodoma cha kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakifuatilia taarifa ya mpango kazi iliyokuwa ikiwasilishwa na Watendaji wa Ofisi zao leo jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakichukua kumbukumbu ya taarifa ya mpango kazi iliyokuwa ikiwasilishwa na Watendaji wa Ofisi zao leo jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.

 



 

Wednesday, November 2, 2022

UANZISHWAJI WA MFUKO WA UWEKEZAJI WA PAMOJA WA ‘FAIDA FUND’ NI MATOKEO YA UTAWALA BORA WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 02 Novemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Serikali kupitia Watumishi Housing Investments (WHI), ni matokeo ya utawala bora wa Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kuwekeza ili kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.

Mhe. Ndejembi amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) iliyo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mhe. Ndejembi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaongoza kwa kusimamia misingi ya utawala bora na ndio maana kupitia Watumishi Housing Investments (WHI) imekuja na mfuko huu wa FAIDA FUND ambao ni wa uhakika zaidi kwa wananchi kuwekeza kwani fedha yao inakuwa kwenye mikono salama.

“Tumeoneshwa mfumo hapa ambao umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambao unamuwezesha mwananchi kufuatialia fedha yake na kuona faida atakayoipata, hivyo unamhakikishia mwananchi usalama wa vipande alivyonunua ili kuwekeza,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, uwepo wa Benki ya CRDB kama msimamizi wa masuala yote ya uwekezaji wa fedha kwenye mfuko huo wa FAIDA FUND unaondoa mashaka na hofu ya wananchi wenye kipato cha chini wenye nia ya kuwekeza kwenye mfuko huo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa FAIDA FUND ni fursa kubwa sana kwa watumishi wa umma wanaotamani kuingia katika uwekezaji kwani siku za nyuma uwekezaji ulikuwa ukitafsiriwa ni kwa watu wenye kipato kikubwa, lakini kupitia kiwango rafiki cha uwekezaji kilichowekwa na FAIDA FUND kinafungua milango ya watumishi wa umma kuwekeza.

“Kiwango cha awali cha uwekezaji kuanzia shilingi 10,000/= ambacho FAIDA FUND imekuja nacho kinamuwezesha mtumishi wa umma kufungua akaunti na kuendelea kuwekeza kwa shilingi 5,000/=, pia kinayawezesha kuwekeza makundi mengine yanayofanya kazi katika sekta isiyo rasmi yakiwemo ya bodaboda, mama lishe na mengineyo,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Charles Shirima amesema mfuko wa FAIDA FUND umepata idhini ya mamlaka hiyo kuendeshwa na kuongeza kuwa, ni mmoja wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaowezesha wawekezaji wa aina zote wakiwemo wadogo, wa kati na wakubwa kuwekeza kwa lengo la kupata faida na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa ambaye taasisi yake imeanzisha mfuko huo wa FAIDA FUND amesema kuwa, FAIDA FUND itawawezesha watu wenye kipato kidogo kuweka akiba itakayozaa na baadae kuuza vipande vyake na kununua kiwanja au nyumba au kufanya shughuli nyingine ya kiuchumi kadiri atakavyoona yafaa.

Mfuko wa FAIDA FUND ni mpango ulio wazi ambao unatoa fursa ya uwekezaji kwa Watanzania hasa wa kipato cha chini kupitia uwekezaji katika vipande ili kupata mapato shindani kupitia ukuaji wa mitaji na kutengeneza utamaduni wa kuwekeza katika Masoko ya Mitaji na Fedha. 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wadau jijini Dar es salaam wakati akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.

Baadhi ya wadau wa Watumishi Housing Investments (WHI) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Watumishi Housing Investments (WHI) CPA Hosea Kashimba akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.


Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa akieleza manufaa ya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzindua mauzo ya vipande vya mfuko huo jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.


Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Charles Shirima akiwasilisha salamu za Mtendaji Mkuu wa CMSA wakati wa  uzinduzi wa mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifuatilia maelezo ya namna mfumo wa FAIDA FUND unavyofanya kazi.