Thursday, June 10, 2021

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA MAAFISA UTUMISHI WANAODANGANYA KUWASILISHA MADAI YA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA OFISI YA RAIS-UTUMISHI

 Na. Veronica Mwafisi-Kondoa

Tarehe 10 Juni, 2021

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu Maafisa Utumishi wote watakaobainika kuwadanganya Watumishi wa Umma wenye madai ya malimbikizo ya mishahara kuwa wamewasilisha madai yao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kufanyiwa kazi wakati sio kweli.

Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa leo Wilayani Kondoa, Mhe. Ndejembi amesema kuna baadhi ya Maafisa Utumishi hawatekelezi wajibu wao kikamilifu na kusababisha Ofisi ya Rais Utumishi kutupiwa lawama na Watumishi.

Amewaelekeza Wakurugenzi kuwasimamia Maafisa Utumishi wao ili watekeleze majukumu yao ipasavyo ikiwemo la kushughulikia fomu za madai ya malimbikizo ya watumishi hao ili yafanyiwe kazi kwa haraka kwa lengo la kupunguza malalamiko ya watumishi ambayo yanashusha ari ya kutekeleza majukumu yao kikamifu.

“Madai ya Watumishi yakichelewa kulipwa, mnasingizia fomu ziko UTUMISHI wakati sio kweli, mara nyingi fomu hizi zinakuwa ziko kwenu Wakurugenzi sababu Maafisa Utumishi wenu kujifanya miungu watu,’” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Mhe. Ndejembi amesema madai ya Watumishi ni haki yao ya msingi  kwani wanatumia jasho lao kulitumikia taifa, hivyo wanastahili kulipwa na si hisani.

Akizungumzia changamoto ya upandishwaji madaraja kwa watumishi, Mhe. Ndejembi amewaelekeza Maafisa Utumishi nchini kuhakikisha wanatenda haki kwa wanaostahili kupandishwa madaraja kama Mhe. Rais Samia Suhuhu Hassan alivyoelekeza.

“Tujitume kwa bidii tusimuangushe Mhe. Rais ambaye ameonyesha nia thabiti ya kuwajali Watumishi wa Umma katika kulinda maslahi na haki zao za msingi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi kuwa makini katika mchakato wa kuwapandisha madaraja watumishi wanaostahili kupanda na kuongeza kuwa Afisa Utumishi yeyote atakayebainika kusababisha mtumishi kutopata haki hiyo atachukuliwa hatua.

Mhe. Ndejembi amewasisitiza Watumishi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika Utumishi wa Umma ili kuboresha utendaji kazi utakaowezesha utoaji wa huduma bora kwa umma.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Sezaria Makota, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufika Wilayani humo na kuzungumza na Watumishi ambapo pia amesisitiza uwajibikaji kwa watumishi hao.

Mhe. Makota amesema hapendezwi kuwepo kwa madai ya malimbikizo ya mishahara na ya upandishwaji vyeo ambayo hayajafanyiwa kazi na Maafisa Utumishi katika Wilaya yake na kuongeza kuwa hatosita kuwachukulia hatua watakaoshindwa kutekeleza maelekezo.

Mhe. Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Wilayani Kondoa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.  

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi leo wilayani Kondoa yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo. 

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji Kondoa Bw. Msoleni Dakawa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Mustapha Semwaiko akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.

Friday, June 4, 2021

MHE. MCHENGERWA AIELEKEZA TPSC KUTOA MAFUNZO YATAKAYOIMARISHA UZALENDO KWA WATUMISHI NA WATANZANIA

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 04 Juni, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutoa mafunzo yatakayoimarisha Uzalendo na Utaifa ili kuzalisha Watumishi wa Umma na Watanzania wazalendo watakaoshiriki vema katika kujenga uchumi wa taifa.

Akizungumza katika mahafali ya 33 ya chuo hicho yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema kutokana na changamoto ya uzalendo kwa baadhi ya Watanzania, ni muda muafaka sasa kwa kila mtanzania kuwa mzalendo kwa taifa lake kwa lengo la kulinda rasilimali za taifa hivyo ni vema chuo kikajikita pia katika mafunzo ya uzalendo na utaifa.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa wahitimu wakiwa na uzalendo watatumia vema mafunzo waliyoyapata ili kuleta tija hususan katika kukuza uchumi wa taifa letu.

“Mafunzo mliyoyapata yasiishie hapa bali yawe ni nyenzo na mkawe mabalozi wazuri kwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi mkubwa na uadilifu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Katika kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa Viongozi wa taasisi za Umma na Halmashauri mbalimbali nchini kutenga bajeti itakayowawezesha watumishi wao kushiriki mafunzo katika chuo cha utumishi wa umma yatakayowajengea uwezo kiutendaji.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma ni mojawapo ya utekelezaji wa Ilani cha Chama cha Mapinduzi ya 2020, hivyo ameiagiza Bodi ya Ushauri na Uongozi wa Chuo kufanya mawasiliano kwa lengo la kuzihimiza wizara na taasisi zote za serikali ili watumishi wanaostahili kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wapate fursa hiyo.

 “Pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM, dunia inabadilika kutokana na kukua kwa teknolojia, hivyo ni lazima watumishi washiriki mafunzo mara kwa mara kuendana na mabadiliko hayo.” Mhe. Mchengerwa amesema.

Sanjari na hayo, Mhe. Mchengerwa ameupongeza uongozi wa chuo na Wakufunzi kwa kutekeleza majukumu yao ya msingi ya chuo na kuaigiza Bodi na uongozi kutekeleza maelekezo ya viongozi mbalimbali ya kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuanzisha matawi mengi zaidi ya chuo na kubuni mikakati mbalimbali itakayosaidia chuo hiki kuwa chuo cha mfano ndani na nje ya nchi.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri Mchengerwa kuzungumza na wahitimu, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florence Turuka amesema wahitimu wamepata mafunzo mazuri yenye weledi mkubwa na kuwasihi wahitimu hao kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kwa maslahi mapana ya taifa.

“Kutokana na mafunzo mliyoyapata hapa naamini mtakuwa ni chachu ya maendeleo na mabalozi wazuri wa chuo chetu huko muendako,” Dkt. Turuka amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Selemani Shindika amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 2000 chini ya Sheria ya Wakala Na. 30 ya mwaka 1997 kupitia Mpango wa Uboreshaji Utumishi wa Umma (PSRP) kwa lengo la kubadilisha na kuboresha Utumishi wa Umma pamoja na kutoa mafunzo kuhusu Utumishi wa Umma, kuratibu na kujenga utamaduni mpya wa Watumishi na Watumishi wa Umma watarajiwa kujiendeleza ili kutoa huduma kwa weledi na ufanisi zaidi.

Dkt. Shindika amesisitiza umuhimu watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza kushiriki mafunzo elekezi katika Chuo cha Utumishi wa Umma ili kuwawezesha watumishi hao kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.

Jumla ya wahitimu 7136 kutoka kwenye kozi 12 zinazotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wametunukiwa Astashahada ya Awali, Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani mbalimbali.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiongoza maandamano wakati mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wahitimu wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wahitimu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florence Turuka akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na wahitimu wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

 


Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akielezea lengo la kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakati wa mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitunuku cheti kwa mmoja wa wahitimu kwenye mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

 

Wahitimu na wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali ya 33 ya chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


 

Tuesday, June 1, 2021

WATUMISHI WA OFISI YA RAIS - UTUMISHI WAPATIWA MAFUNZO YA NAMNA BORA YA KUTOA HUDUMA KWA UMMA

Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 01 Juni, 2021

Watumishi watakaokuwa wakitoa huduma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wanashiriki mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia kituo hicho kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Akifungua mafunzo hayo Jijini Dodoma leo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji amesema, kituo hicho kitasaidia wadau kupewa mrejesho wa masuala ya kiutumishi kwa wakati tofauti na ilivyo sasa ambapo wanalazimika kusubiri wajibiwe kwa barua.

Bw. Ngangaji amesema, utoaji wa huduma kupitia kituo hicho utapunguza adha ya wanaohitaji huduma na kuongeza kuwa, utajenga mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora kwani utarahisisha upokeaji wa maoni na malalamiko ya kiutumishi yanayowasilishwa na kuyashughulikia kwa wakati.

“Ifahamike kuwa, uanzishwaji wa kituo hicho hauondoi mifumo rasmi ya utoaji huduma na ushughulikiaji wa malalamiko, bali ni moja ya utaratibu wa kisasa wa utoaji huduma kwa njia ya TEHAMA.” Bw. Ngangaji amesisitiza.

Amefafanua kuwa, Kituo hicho kitaunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Malalamiko (e-malalamiko) ambao umesanifiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Mafunzo hayo ya siku tatu yana lengo la kujenga uelewa wa watumishi juu ya namna bora ya kuendesha kituo hicho na kubadilishana uzoefu wa  ushughulikiaji wa malalamiko na maoni ya wadau ambayo yatakayoboresha uendeshaji wa Kituo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amemshukuru Bw. Ngangaji kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kuwa kituo hicho kitatumika kujenga taswira nzuri ya Ofisi na Serikali kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji akifungua mafunzo Jijini Dodoma leo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI juu ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji alipokuwa akifungua mafunzo hayo Jijini Dodoma leo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, akitoa neno la shukurani kwa Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Ngangaji baada ya Mkurugenzi huyo kufungua mafunzo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI ya kutoa huduma kwa umma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

 

Mwezeshaji wa mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni, Bw. James Sweke akitoa mafunzo kwa washiriki wa mafunzo hayo leo Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni baada ya Mkurugenzi huyo kufungua mafunzo hayo Jijini Dodoma leo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI.