Wednesday, January 13, 2021

MAAFISA UGANI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA KILIMO BORA CHA MAZAO YA BIASHARA KWA WANUFAIKA WA TASAF

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 13 Januari, 2021

 Maafisa Ugani wametakiwa kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya biashara  kwa kaya zote maskini nchini zinazonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  ili kaya hizo ziweze kupata mavuno bora yatakayoziwezesha kuboresha maisha yao na kuondokana umaskini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa Maafisa Ugani akiwa kijiji cha Mtinko Wilayani Singida katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.

Mhe. Ndejembi amewahimiza Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Ugani katika Halmashauri zote kutoa maelekezo kwa kaya maskini juu ya namna bora ya kulima mazao yanayostahimili ukame na kuendana na mazingira halisi ya maeneo husika ili kaya maskini ziweze kunufaika na kilimo.

“Maafisa Ugani katika ngazi ya kata na vijiji waanze kuzitembelea kaya maskini na kuzisaidia namna ya kulima kitaalamu ili ziweze kupata mavuno ya kutosha na kuongeza kuwa, Maafisa Ugani waache kwenda kwenye miradi ya nyama pekee ambayo inawanufaisha kwa kujipatia fedha”, Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amepokea shuhuda mbalimbali za mafanikio waliyoyapata wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Mtinko wilayani Singida.

Mmoja wa wanufaika, Bi. Leah Ibrahimu Shila amesema, ameitumia fedha ya ruzuku aliyoipokea kujiwekea akiba kidogo kidogo na hatimaye kupata mtaji wa shilingi 200,000/= uliomuwezesha kufungua mgahawa wa kuuza chakula.

Bi. Shila ameeleza kuwa, kabla ya kuwa mnufaika wa TASAF alikuwa akiishi maisha magumu yaliyomsababishia kula mlo mmoja kwa siku lakini hivi sasa anakula milo mitatu na anasomesha watoto wake katika shule za msingi na sekondari.

Naye, Bi. Zena Ramadhani Igwe amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ametumia vizuri ruzuku aliyoipokea toka TASAF kwa kujenga nyumba bora ya bati kwani aliweza kuwekeza fedha kidogo kidogo ambazo zilimuwezesha kununua saruji na bati.

Ameongeza kuwa, fedha hizo zimemsaidia pia kuanza shughuli ya ufugaji wa kuku ambao wamefikia 30 na ameweza kujishughulisha na kilimo cha bustani, ikiwa ni pamoja na kumsomesha mtoto wake elimu ya sekondari.

Mhe. Ndenjembi ameridhishwa na mafanikio waliyoyapata wanufaika wa TASAF, Bi. Lea Ibrahimu Shila na Bi. Zena Ramadhani Igwe wa Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida na kutoa wito kwa wanufaika wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, kuzitumia vema fedha za ruzuku katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao na kuondokana na umaskini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Mtinko wilayani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.


Baadhi ya wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida wakisikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Hayupo pichani) wakati wa ziara kikazi ya Naibu Waziri huyo wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.


Mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko wilayani Singida, Bi. Leah Ibrahimu Shila akieleza mafanikio aliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kushoto) akila chakula kwenye mgahawa wa mnufaika wa TASAF kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, Bi. Leah Ibrahimu Shila (wa kwanza kulia) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.


Mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, Bi. Zena Ramadhani Igwe akieleza mafanikio aliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo mbele ya nyumba ya mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.



 

 

Tuesday, January 12, 2021

WAAJIRI WAHIMIZWA KUKITUMIA IPASAVYO CHUO CHA UTUMISHI

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 12 Januari, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza Waajiri katika Taasisi za Umma nchini kuwapeleka watumishi wao katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kupatiwa mafunzo bora yatakayowajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Singida.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, kuna tabia ya baadhi ya Watumishi wa Umma kulewa madaraka ambayo mara kadhaa imekemewa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika inatokana na watumishi hao kukosa maadili ya kiutumishi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma ndicho pekee kina uwezo wa kutoa mafunzo yatakayojenga maadili bora kwa Watumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, lengo kuu la kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma lilikuwa ni kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao, hivyo ni wajibu wa waajiri wote kukitumia ipasavyo ili kuondokana na changamoto za kiutendaji na kimaadili zinazowakabili Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Mhe. Ndejembi amekanusha dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu wakidhani Chuo cha Utumishi wa Umma kipo kiushindani dhidi ya Vyuo Vikuu kama UDSM, UDOM, SAUT na Mzumbe na kuongeza kuwa, chuo hicho pia kina jukumu la kutoa mafunzo ya maadili na masuala kiutumishi kwa watumishi walioajiriwa na vyuo vikuu nchini ili vyuo hivyo viweze kuwaandaa wahitimu watakaotoa mchango katika maendeleo ya Taifa.

Kuhusiana na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma wanaopatiwa mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Mhe. Ndejembi amehuzunishwa na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma 86 tu wa mkoa wa Singida waliopata fursa ya mafunzo katika Kampasi ya Singida wakati chuo kina uwezo wa kutoa mafunzo kwa watumishi wote mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amesema, waajiri wakishirikiana vema na Chuo cha Utumishi wa Umma katika kutoa mafunzo kwa watumishi watakuwa wametekeleza wajibu wa kujenga taifa lenye Watumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa chuo, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema, Chuo kilianzishwa kwa lengo la kuboresha Utumishi wa Umma nchini licha ya kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya cheti, diploma na shahada.

Dkt. Shindika amefafanua kuwa, Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kama zilivyo kampasi nyingine kina majukumu makubwa matatu ambayo ni kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kutoa shauri za kitaalam na kufanya tafiti zenye tija ambazo zinatumiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.

Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kilianza kutoa huduma rasmi mwaka 2011 na kilisajiriwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) mwezi Novemba 2014, hivyo kimeweza kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika ngazi  nne ambazo ni fani Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka, Uhazili na Utawala wa Umma na Rasilimaliwatu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


Baadhi ya Watumishi wa Umma Kampasi ya Singida wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao.


Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Kampasi ya Singida.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


 

Saturday, January 9, 2021

TASAF YABORESHA MAISHA YA WANANCHI KIJIJI CHA BWITI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Mkinga

Tarehe 09 Januari, 2021

Wananchi wanaoishi katika kaya maskini Kijiji cha Bwiti, wilayani Mkinga wanaonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamewezeshwa kuboresha makazi yao, kufanya shughuli za ufugaji, ujasiliamali, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, kujishughulisha na kilimo ikiwa ni pamoja na kumudu gharama za mahitaji ya shule kwa watoto wao.

Wananchi hao wametoa shuhuda za mafanikio waliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Tanga.

Mmoja wa wanufaika Bi. Fatuma Mohamed Hamza amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ruzuku aliyoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemuwezesha kununua bati 40 alizoziezeka katika nyumba yake na hatimaye kuondokana na adha ya kunyeshewa na mvua aliyokuwa akikabiliana nayo kwa kipindi kirefu.

Naye, mjane Bi. Mwajuma Ayubu Bakari amesema, baada ya kupokea ruzuku yake kwa vipindi vitatu mfululizo aliwekeza kidogo kidogo na hatimaye kuweza nununua mbuzi ambapo mpaka hivi sasa amefanikiwa kuwa na mbuzi wapatao 14 na kuongeza kuwa, ruzuku pia inamuwezesha kugharamia mahitaji ya watoto shuleni.

Mnufaika mwingine, Bi. Mwajuma Said Kidevu amemthibitishia Mhe. Ndejembi kuwa, kabla ya kupokea ruzuku alikuwa na mbuzi 6 lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kuongeza idadi ya mbuzi anaowafuga hadi kufikia 12.

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, kupitia ruzuku anayoipata ameweza kujenga nyumba bora yenye choo bora, anajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na ameweka umeme nyumbani kwake, hivyo anaishukuru Serikali kwa kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa umeboresha maisha yake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) mara baada ya kupokea shuhuda hizo, amewataka walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vema ruzuku wanazozipata kujikwamua katika umaskini ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, matumizi mazuri ya ruzuku ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Mhe. Rais ya kuuendeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha ya wanyonge nchini.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya namna bora ya kutumia ruzuku wanazopatiwa walengwa wa TASAF na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha ruzuku wanazopatiwa zinatumika kuboresha maisha yao na kuweza kuhitimu kwa lengo la kutoa fursa kwa kaya nyingine kunufaika na ruzuku inayotolewa na TASAF.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) akiwasisitiza wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti (hawapo pichani) kutumia vizuri ruzuku wanayoipata ili kuboresha maisha yao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga. 


Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga.


Mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti, Bi. Fatuma Mohamed Hamza akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata baada ya kunufaika na ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa TASAF Bw. Oscar Maduhu akifafanua malengo ya TASAF kwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wilayani Mkinga.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza ushuhuda wa mafanikio aliyoyapa Bi. Mwajuma Ayubu Bakari baada ya kupokea ruzuku yake toka TASAF.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza kwa makini ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata Bi. Mwajuma Said Kidevu mara baada ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF.


Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata kupitia ruzuku anayoipata toka TASAF.