Mwandishi Wetu
Tarehe 08 Mei, 2024
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi, amewataka Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika
Utumishi wa Umma PEPMIS kujitoa wakati wote kuwaelekeza watumishi wengine katika
maeneo yao ya kazi ili Serikali iweze kubaini mwenendo halisi wa utendaji kazi
wa watumishi wa umma.
Bw. Daudi, amesema hayo leo Mei 8, 2024 wakati akifungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara takribani 110 wa Mfumo wa Usimamizi wa
Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma kutoka katika taasisi mbalimbali za umma
zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Mafunzo hayo yanayofanyika katika
ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Aidha, amewapongeza Vinara hao kwa kuchaguliwa na
kupata fursa ya kujengewa uwezo ili kwenda kuwasaidia watumishi wengine katika
taasisi mbalimbali zilizopo katika mikoa yao.
Pia, amewasisitiza Vinara hao kutambua kuwa Serikali kupitia
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaamini na
kuwapa dhamana kubwa ya kutoa msaada wa kiufundi kwa watumishi wengine katika
masuala ya matumizi ya mfumo wa PEPMIS. Hivyo, wanatakiwa kutumia dhamana hiyo
kwa ufanisi.
“Ninatambua mafunzo kama haya yalitolewa kwa watumishi
wote katika kipindi cha mafunzo ya awali na ninyi mkiwa ni sehemu ya washiriki
hao, sasa mumechaguliwa kuwa vinara kutokana na uwezo wenu, shauku na mapokeo
chanya ya matumizi ya mifumo hii, hivyo jitoeni zaidi na muwe sehemu ya
watumishi watakaotambuliwa na Serikali na
vizazi vijavyo kuwa sehemu ya waliofanya mageuzi katika utumishi wa umma”
amesisitiza Bw. Daudi.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya
Utendaji Kazi, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Elizabeth Makyao amesema Mifumo ya
PEPMIS na PIPMIS ni mipya na inahitaji wataalamu wengi ambao wanauwezo wa kutoa
msaada wa kiufundi kwa ukaribu, haraka na ufanisi ili kuondoa changamoto ya
kutafuta msaada huo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora.
Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora iko tayari kupokea jambo ambalo litakuwa nje ya uwezo
wao na kusaidia kupata ufumbuzi wa haraka kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, mafunzo hayo ya siku tatu ni matokeo ya mapendekezo ya Timu ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora walioshiriki kutoa na kusimamia mafunzo ya PIPMIS na PEPMIS kuanzia Novemba 23, 2023 hadi Februari 15, 2024 katika taasisi zote za umma zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi akitoa hotuba wakati wa kufungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi
katika Utumishi wa Umma yanayofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya Utendaji Kazi, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Elizabeth Makyao akizungumzaa jambo na Mgeni Rasmi Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi kabla ya kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma yanayofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mikataba ya Utendaji
Kazi, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Elizabeth Makyao akitoa maelezo mafupi kabla
ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Vinara wa Mfumo
wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma yanayofanyika katika
ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Baadhi ya Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji
Kazi katika Utumishi wa Umma (PIPMIS) kutoka katika taasisi mbalimbali za umma
zilizopo katika mikoa 26 ya Tanzania Bara wakiwa kwenye mafunzo ya PEPMIS yanayofanyika
katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma leo tarehe 8 Mei, 2024
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo
ya kuwajengea uwezo Vinara wa Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi katika
Utumishi wa Umma yanayofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment