Friday, May 3, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE AWATAKA WATUMISHI WENYE DHAMANA YA KUINGA KWENYE MIFUMO YA KIUTUMISHI KUTENDA HAKI

 Na. Rainer Budodi-Arusha

Tarehe 02 Mei, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka Maafisa Utumishi waliopewa dhamana ya kuingia kwenye mifumo ya usimamizi wa rasilimaliwatu kutumia dhamana hiyo kutochezea mifumo hiyo na kuwaonea watumishi wengine na badala yake watumie dhamana hiyo kutenda haki.

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Amesema kuwa yapo malalamiko yanayoonesha uvunjifu wa Maadili na ukiukwaji wa taratibu za kiutendaji ikiwemo, baadhi ya Maafisa Utumishi ambao wanaingia katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (New HCMIS) kusimamisha mishahara au makato ya mishahara bila kufuata taratibu zilizowekwa na wakati mwingine kutumia nafasi zao kukomoa watumishi wengine, lakini pia wamekuwa wakitoa taarifa ambazo wanakutana nazo katika mifumo hiyo kwa watu wasiohusika.

“Tumebaini baadhi mnafanya hivyo kwa sababu tu mna dhamana ya kuingia kwenye mifumo, hili limejitokeza sana, tufahamu kuwa Sheria zetu za TEHAMA na za kiutumishi zinatambua kuwa hayo ni makosa makubwa ya Kimenejimenti na sehemu kubwa ni makosa ya jinai, hivyo tutachukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kufanya hivyo,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Mhe. Simbachawene ametumia fursa kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya kusimamia mifumo hiyo ya serikali ili isichezewe kwani imekuwa msaada mkubwa katika kuboresha ufanisi wa utendaji kazi katika utumishi wa umma nchini.

“Wenzetu Viongozi mlioko kwenye mikoa na Wilaya mtusaidie kusimamia hili  kwani masuala ya utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu ni ya wote na sio ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora pekee,  hivyo tukiruhusu mifumo hii kuchezewa tutashindwa kufikia malengo ya serikali ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi,  tushirikiane kuwabaini wale wanaoihujumu ili hatua kali zichukuliwe kwa masilahi mapana ya taifa,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Ameongeza kuwa mifumo hiyo imeisaidia Serikali kudhibiti baadhi ya mambo ya hovyo ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya watu, hivyo wale wote wanaopenda mambo ya hovyo wanaihujumu ili isifanye kazi na kurudisha nyumba maendeleo ya nchi.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kufungua mkutano huo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rai-UTUMISHI, Bi. Felister Shuli amesema mkutano huo wa 11 umelenga kutoa fursa kwa wataalam na wasimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma kujifunza; kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu; na kubaini changamoto zinazojitokeza katika kusimamia rasilimaliwatu na namna ya kukabiliana nazo.  

Aidha, umelenga kuweka mikakati ya kuendeleza Utawala na Rasilimaliwatu kwa kuzingatia makubaliano ambayo yamefikiwa na nchi wanachama wa AAPAM Afrika ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Serikali kwa umma.

Mkutano huo wa siku tatu unaoratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora-Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu unaongozwa na Kaulimbi isemayo ‘Usimamizi wa Utendaji Kazi katika Utoaji wa Huduma: Nafasi ya TEHAMA katika kuimarisha Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma.’

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).



Rais wa AAPAM Afrika, Dkt. John Nakabago akitoa salam wakati wa Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Mwenyekiti wa AAAPM Tawi la Tanzania, Bi. Leila Mavika akitoa utambulisho na maelezo kuhusu AAPAM Tawi la Tanzania kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya Waziri huyo kufungua Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Felister Shuli akitoa maelezo ya awali kuhusu Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua Mkutano huo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Washiriki wa Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).



 

 

No comments:

Post a Comment