Saturday, May 4, 2024

NAIBU WAZIRI KIKWETE ASISITIZA MATUMIZI YA MIFUMO YA TEHAMA ILI KUIMARISHA HAKI NA WAJIBU

 Na Mwandishi Wetu

Tarehe 04 Mei, 2024

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi kutumia mifumo ya usimamizi wa rasilimaliwatu iliyosanifiwa na kutengenezwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi na kuleta uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo Mei 4, 2024 wakati akifunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Amesema kuwa, Serikali imetengeneza mifumo mbalimbali akitolea mfano wa Mfumo wa Employment Self Service (ESS) ambao moja ya lengo lake ni kuwawezesha watumishi wa umma kupata huduma kwa urahisi na kupunguza mlolongo na ukiritimba uliokuwepo katika taratibu za kupata huduma za mikopo katika taasisi za umma na taasisi za fedha. 

“Serikali imelenga kutengeneza mazingira rafiki na kuwafanya watumishi wa umma kutumia muda wa kazi katika kuwahudumia wananchi kwa haraka na wakati, hivyo, waelimisheni watumishi walio katika sehemu zenu za kazi ili kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi” amesisitiza Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetafsiri kwa ufanisi na kutekeleza azma na maagizo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa na nia ya kuifanya Serikali kuwa ya kidijitali kwa kuandaa mifumo inayorahisisha utendaji kazi.

“Rais wetu amelenga kubadilisha mfumo wa utumishi wa umma ili uendane na Tanzania anayoitaka, hivyo, sisi tukiwa ndio wasaidizi wake na watumishi wa umma kwa jumla hatuna budi kuhakikisha azma yake inatekelezwa ipasavyo kwa kutumia mifumo hiyo” ameongeza Mhe. Kikwete. 

Mhe. Kikwete ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimawatu kuhakikisha wanasimamia mifumo hiyo ya Serikali na kuwahimiza watumishi katika taasisi zao kuitumia kwa lengo lililokusudiwa na Serikali.

“Iwapo kutatokea kushindwa kutumika ipasavyo itakuwa ni sehemu ya kushindwa katika uongozi wenu na shughulikieni kero za wananchi ili Tanzania anayoitaka Rais, Mhe. Samia iweze kupatikana” ameongeza Mhe. Kikwete.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Kikwete kufunga mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi amesema washiriki wa mkutano huo wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yatakayoboresha utendaji kazi na kuongeza tija na ufanisi.

Mkutano huo wa siku tatu unaoratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, umehitishwa leo kwa kufanya uchaguzi na kuwapata viongozi wa Jumuiya ya Maafisa Tawala na RasilimawatuTanzania (TAPAHR)

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa hatuba ya kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiteta jambo na Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi yake Bw. Xavier Daudi kabla ya kutoa hatuba ya kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Mwenyekiti wa AAAPM Tawi la Tanzania, Bi. Leila Mavika akitoa maelezo mafupi kuhusu AAPAM Tawi la Tanzania kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kabla ya kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Rais wa AAPAM Afrika, Dkt. John Nakabago akitoa kitambulisho cha uanachama wa AAPAMA Tawi la Tanzania kwa Makamu wa Rais wa AAPAM, ukanda wa Afrika Mashariki Bw. Ayoub J. Kilabuka wakati wa kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisisitiza jambo wakati wa akitoa hatuba ya kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania wakifuatilia wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).


Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi wakati wa kufunga Mkutano wa 11 wa Wanachama wa AAPAM Tawi la Tanzania leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).



No comments:

Post a Comment