Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene ametoa rai kwa wahitimu kutambua kuwa kwenye utumishi wa
umma sio sehemu ya kuvuna utajiri na kujilimbikizia mali bali ni sehemu ya
kujitoa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa umma.
Mhe.
Simbachawene ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 38 ya Chuo cha Utumishi wa
umma Tanzania yaliyofanyika katika Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Mkoani
Tabora.
“Naomba kila mmoja wenu awe na moyo wa
kujitoa kwa maendeleo ya taifa na kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana katika
mazingira yenu na zile zinazotolewa na Serikali katika kujiletea maendeleo na
kuhakikisha mnatatua changamoto zinazokabili jamii zinazowazunguka wakati mkidumisha
amani, upendo na mshikamano” amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Aidha,
Mhe. Simbachawene ametumia fursa ya mahafali hayo kutoa wito kwa waajiri wote
wa Taasisi za Umma nchini kukitumia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika kuboresha
utendaji kazi wa watumishi na Taasisi zao kupitia mafunzo mbalimbali
yanayotolewa na Chuo hicho.
Mhe.
Simbachawene amesema kuwa baadhi ya taasisi za umma zimekuwa zikisuasua katika kuwapatia
waajiriwa wapya Mafunzo Elekezi ya Awali (Induction Training) jambo ambalo
linasababisha watumishi hao kushindwa kutambua misingi ya Utumishi wa Umma, Sheria,
Kanuni, Miongozo na Taratibu za utendaji kazi na uwajibikaji Serikalini.
Aidha,
amewasisitiza Maafisa Masuuli wote katika taasisi za umma kutumia muda wao
kufanya uchunguzi kwa makini ili kuona namna wajiriwa hao wapya wanavyopata
shida katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kukwamisha
jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Napenda
ifahamimike kuwa suala la kuwapatia watumishi wapya mafunzo sio hiari bali ni matakwa
ya kisheria na hii ni kwa mujibu wa waraka wa Utumishi Na. 5 wa mwaka 2011. Kwa
hiyo ninaelekeza watumishi wote wapya katika utumishi wa umma wapewe mafunzo
mara tu wanaporipoti katika vituo vyao vya kazi” amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Vilevile, Mhe. Simbachawene Mhe.
Simbachawene ameipongeza Bodi, Menejimenti na watumishi wote wa Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwa matunda ya kazi
yao njema yanaonekana wazi. Vilevile
amewahakikishia kuwa Serikali hii ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua juhudi wanazofanya na hivyo, Wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano
ili kufanikisha malengo ya chuo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akihutubia wahitimu na wageni waalikwa wakati wa mahafali
ya 38 ya Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania yaliyofanyika katika Kampasi ya
Chuo hicho Mkoani Tabora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wakati
wa mahafali ya 38 ya Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania yaliyofanyika katika
Kampasi ya Chuo hicho Mkoani Tabora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo
cha Utumishi wa umma Tanzania Dkt. Florens Turuka wakati wa mahafali ya 38 ya Chuo
hicho yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora Mkoani Tabora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahitimu wa Chuo
cha Utumishi wa umma Tanzania wakati wa mahafali ya 38 yaliyofanyika katika
Kampasi ya Chuo hicho Mkoani Tabora.