Friday, September 29, 2023

MHE. SIMBACHAWENE: UONGOZI SIO KUBADILISHA WATU BALI NI KUBALISHA MITIZAMO YA UNAOWAONGOZA

 Na.Lusungu Helela-DSM

29 Septemba, 2023

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Uongozi sio kubadilisha watu uliowakuta badala yake ni kujenga ushawishi wa kubadili mitazamo ya wale unaowaongoza kwa kuonesha njia ili kufikia malengo makubwa ya kuwahudumia wananchi.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Njia ya Mtandao Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne inayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto, cha nchini Finland.

 

Mhe. Simbachawene amesema kuna tabia imejengeka kwa baadhi ya Viongozi  mbalimbali nchini  pindi wanapopewa uongozi huanza  kuwaondoa baadhi ya  Watumishi waliowakuta katika Ofisi za Umma kwa kisingizio kuwa hawaendani na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Amesisitiza kuwa, Kiongozi bora hahitaji kujitambulisha kuwa yeye ni nani bali hutambuliwa kwa jinsi anavyojiweka na anavyoendesha mambo yake kwa wale anaowaongoza.

 

''Ukiona Kiongozi anajitambulisha kuwa yeye ni nani tambua kuwa hapo kuna walakini, Kiongozi hutambuliwa na watu kwa jinsi anavyojiweka katika jamii kwa matendo yake mema yanayozingatia maadili'' amesisitiza Mhe. Simbachawene.

 

Akizungumzia Programu hiyo ya uongozi ngazi ya cheti, Mhe. Simbachawene amewataka washiriki kusoma kwa bidii kwani Programu hiyo ni muhimu kwa vile inalenga kuisaidia Serikali katika kuimarisha utendaji kazi na hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo.

 

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utawala bora, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika kada zote za uongozi.

 

Amesema  mafunzo  hayo  yamehusisha washiriki kutoka  sekta ya umma na sekta binafsi ambao kimsingi jukumu lao kuu ni moja ambalo ni kuhudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki.

 

Mhe. Simbachawene amewahimiza washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili yakawe nyenzo muhimu ya kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi wao na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na hatimaye kuwa na utawala bora wenye kuzingatia sheria, maadili na haki.

 

Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting ameisifu Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kwenye suala la Uongozi hususan, kwenye idadi kubwa ya wanawake ambao ni viongozi wakubwa kwenye sekta ya umma na binafsi.

 

''Kwa mwelekeo huu, Mimi kama Balozi nitaendelea kuishawishi nchi yangu kuendelea kufadhili Taasisi ya UONGOZI ili kuibua wanawake wengi zaidi katika ngazi za juu za maamuzi'' amesema Mhe. Balozi.

 

Awali, Mtendaji Mkuu, Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema Taasisi yake imejielekeza kuandaa Viongozi wenye maarifa na wanaojua wajibu wao kwa wanaowangoza na wananchi na sio wanaotaka kupata vyeti tu. 

 

Jumla ya washiriki takriban 70 kutoka sekta ya umma na sekta binafsi wanashiriki programu ya mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa miezi sita.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya washiriki wa Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati akifungua Programu ya Mafunzo hayo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting, akiwasilisha salamu za nchi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya Mhe. Simbachawene kufungua Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa kuhusu Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kabla ya kumkaribisha Mhe. Simbachawene kufungua mafunzo hayo leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akitia baraka matarajio ya washiriki wa Programu ya Mafunzo ya Uongozi ya Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne kwa kuweka saini kwenye ubao unaoonyesha matarajio hayo 


Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting akitia baraka matarajio ya washiriki wa Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne kwa kuweka saini kwenye ubao unaoonyesha matarajio hayo. Anayeshuhudia nyuma yake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Programu ya Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne. Waliokaa wa pili kushoto ni Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting na wa pili kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo


Thursday, September 28, 2023

MHE. KIKWETE ASISITIZA UTUMISHI WA UMMA NI POPOTE, AWAASA WAZAZI

 


Na. Lusungu Helela-Chalinze

28 Septemba, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Watumishi wa Umma kuwa tayari kufanya kazi sehemu yoyote watakayopangiwa kwani Utumishi wa Umma ni utayari wa kukubali kufanya kazi mahali popote.

 

Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, ikiwa ni ziara yake ya kimkakati ya kusikiliza na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili Watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Amesema Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wazazi wakiomba kuwabadilishia watoto wao vituo vya kazi pindi wanapopangiwa mikoa ya pembezoni, wakiomba wapangiwe mijini hususan Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.

 

Mhe. Kikwete amewasihi wazazi hao kuwaacha watoto wao wakafanye kazi katika vituo walivyopangiwa kwani katika mikoa hiyo ya pembezoni wanaoishi pia ni Watanzania sawa na wale wanaoishi mijini na kwamba nao pia wanahitaji kuhudumiwa kama wengine.

 

"Watumishi wenzangu hakuna Watumishi ambao ni maalum kwa ajili ya kufanya kazi mikoa ya pembezoni hivyo nawasihi mtulie kwenye vituo vya kazi mlivyopangiwa na kuendelea kuwahudumia wananchi" Mhe. Kikwete amesisitiza.

 

Naibu Waziri Kikwete ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada za kuweka mazingira mazuri ya watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi katika vituo vyao vya kazi.

 

Katika hatua nyingine Mhe. Kikwete ameahidi kuendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo huku akiahidi kuzichukua baadhi ya changamoto za kimuundo ambazo zimekuwa zikipunguza morali ya utendaji kazi kwa baadhi ya Wakuu wa vitengo vya Halmashauri hiyo.

 


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao 



Kaimu wa  Idara ya Elimu Msingi, Warda Hussein akizungumza mbele Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete changamoto zinazokikabali Kitengo hicho katika kutimiza majukumu yake wakati  kikao na watmishi wa Halmashauri hiyo.



Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe.  Halima Okashi   akizungumza kabla ya kumkaribisha  Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzungumza na Watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao

Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhan Possi  akizungumza na Watumishi wa Halmashauri hiyo kabala ya kumkaribisha  Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete kuzumgmza na watumishi hao, ikiwa ni ziara yake ya  kikazi mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza changamoto  zinazowakabili watumishi hao 


Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na leo wilayani  hapo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji

 


SIKUKUU NJEMA YA MAULID

 


Monday, September 25, 2023

TIMU YA OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAPEWA KIBARUA CHA KURUDI NA UBINGWA SHIMIWI

 

Na. Mwandishi wetu-Dodoma

25 Septemba, 2023

 Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika ameisisitiza timu ya Ofisi hiyo inayokwenda kushiriki kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu kuhakikisha inashindana ili kuibuka kidedea.

 

Katika michezo hiyo ya kusisimua iliyopangwa kufanyika Mkoani Iringa, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora imepeleka wachezaji 46 ambao watashindana katika michezo ya mpira wa miguu, netiboli, baiskeli, pamoja na riadha.

 

Mwaka 2014, Ofisi hiyo ilishiriki katika michezo hiyo na kufanikiwa kunyakua ubingwa, ambapo tangu mwaka huo haikuweza kushiriki tena hadi mwaka huu.

 

Akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao 46 waliochaguliwa kwa ajili ya kuipeperusha bendera ya Ofisi hiyo katika michezo ya mwaka huu, Bi. Mavika amewahimiza wawakilishi hao kuhakikisha wanakwenda kupambana kikamilifu ili kurejesha heshima ya Ofisi hiyo katika michezo hiyo.

 

“Kwanza kabisa napenda kuwapongeza kwa kuchaguliwa kuiwakilisha Ofisi katika michezo ya SHIMIWI ya mwaka huu, kwani Ofisi hii ina watumishi wengi lakini mmechaguliwa nyinyi, hivyo ni lazima mjue mmepewa heshima kubwa sana ya kutuwakilisha,” amesema.

 

Pamoja na kuwataka wakacheze kikamilifu na kurudi na ubingwa, Bi Mavika amewaasa watumishi hao kuonyesha nidhamu ya hali ya juu, ndani na nje ya uwanja.

 

“Lazime mkumbuke mnakwenda kuiwakilisha Ofisi yenye heshima ya juu sana katika Serikali yetu, hivyo mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wengine,” ameongeza.

 

Hata hivyo, amewatia moyo kwamba uongozi wa Ofisi hiyo utasimama bega kwa bega na wachezaji hao katika kipindi chote cha mashindano, na kuwataka wasisite kuwasiliana na uongozi wa Ofisi pale watakapokutana na changamoto yeyote.

 

Kwa upande wake, mwakilishi wa timu hiyo, Bw. Charles Shija, ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kuwaamini na kuwapatia huduma nzuri katika kipindi chote cha maandalizi.

 

“Tunajua Ofisi kwa sasa ina vipaumbele vingi na vya muhimu sana vya kutekeleza, lakini pamoja na hayo mmeona umuhimu wa kuturuhusu na kutuwezesha kushiriki katika mashindano ya mwaka huu, tunaahidi hatutawaangusha,” amesisitiza Bw. Shija.

 

Aidha, amesema wachezaji wote wana afya nzuri na wamepata muda mzuri wa kufanya mazoezi chini ya makocha hodari hivyo wana uhakika wa ushindi na kurudi na ubingwa.




1.    Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,UTUMISHI, Bi. Leila Mavika akizungumza  wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo 46  waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

1.    Mwakilishi wa timu ya Wanamichezo kutoka Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Charles Shija akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo 46 waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa ambapo ametumia fursa hiyo kuishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa imani kubwa waliyonayo kwao.

 

1.    Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utawala kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Nyasinde Mukono akizungumza wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo 46  waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

1.    Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na wanamichezo 46  wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

 

 

1.    Sehemu ya wanamichezo wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao 46 waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

1.    Sehemu ya wanamichezo wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Leila Mavika wakati wa hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga wanamichezo hao 46 waliochaguliwa kushiriki kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Iringa.


Saturday, September 23, 2023

MHE. KIKWETE ASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUSHUGHULIKIA HOJA NA MALALAMIKO YA WANANCHI KWA WAKATI

Na. Rainer Budodi-Dodoma

Tarehe 22 Septemba, 2023


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasisitiza watumishi wa umma kushughulikia hoja na malalamiko ya wananchi kwa wakati  ili kuwapunguzia Viongozi wa Kitaifa adha ya kushughulikia masuala ambayo yangeweza kumalizwa katika vituo vya kutolea huduma.

“Sote tumeshuhudia namna ambavyo kunakuwa na mabango yenye malalamiko wakati wa ziara za Viongozi wa Kitaifa. Hii inaashiria kuwa watendaji wetu katika vituo vya kazi hawatekelezi majukumu yao ipasavyo na hivyo kusababisha wateja kutafuta suluhisho sehemu nyingine” amesisitiza

Mhe. Ridhiwani amesema hayo wakati akifunga kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kilichowashirikisha wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma katika ukumbi wa PSSSF-Makole Dodoma.

Aidha, Mhe.Ridhiwani ametoa rai kwa washiriki hao kufanyia kazi kwa vitendo masuala waliyojifunza katika siku hizo mbili ili kuendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Watumishi wa Umma ambao ni Waadilifu na wenye kuwajibika kwa hiari.

Ameongeza kuwa wataalamu wa ofisi yake kwa kushirikiana na Taasisi Simamizi za Maadili katika Utumishi wa Umma wanafanyia kazi hoja na changamoto mbalimbali kuhusu usimamizi wa maadili, nidhamu na michakato ya ajira ili kuondoa malalamiko yaliyopo na kuleta ufanisi zaidi.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu Bi. Leila Mavika amesema Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma kutoa ushauri wa kitaalamu pale itakapohitajika, kujenga uelewa kuhusu maadili ya Utumishi wa Umma na kushirikiana na wadau hao kuleta mabadiliko ya fikra miongoni mwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma Bi. Jane Mazigo ameishukuru ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora kwa kuandaa mafunzo haya muhimu kwa wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma.

“Mhe. Naibu waziri tumejifunza mambo mengi na tuko tayari kuelimisha kundi kubwa la watumishi wa umma kuzingatia masuala ya nidhamu na Uadilifu kazini. Kundi hili limejifunza masuala muhimu na kwa watu muhimu na sisi hatutokuangusha” alisisitiza.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akifunga kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kilichowashirikisha wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma tarehe 22 Septemba, 2023.


Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma tarehe 22 Septemba, 2023.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais- UTUMISHI Bi. Leila Mavika wakifuatilia kwa makini salamu za shukurani kutoka kwa Mwakilishi wa Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma Bi. Jane Mazigo katika Ukumbi wa PSSSF Jijini Dodoma tarehe 22 Septemba, 2023.


Mwakilishi wa Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma Bi. Jane Mazigo akitoa salaamu za shukurani kwa niaba ya washiriki kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa kufunga kikao kazi cha Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma kilichofanyika Jijini Dodoma tarehe 22 Septemba, 2023.


 

Thursday, September 21, 2023

MHE. SIMBACHAWENE ASISITIZA MATUMIZI YA SERIKALI MTANDAO KWA TAASISI ZA UMMA ILI KUEPUSHA MALALAMIKO YA WANANCHI

Na. Rainer Budodi-Dodoma

Tarehe 21 Septemba, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amesisitiza matumizi ya Serikali Mtandao katika kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa Maadili katika Utumishi wa Umma ambavyo vinaleta malalamiko Serikalini.

Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 21 Septemba, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kilichowashirikisha wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma katika ukumbi wa PSSSF-Makole Dodoma.

Ni matarajio yangu kuwa mikakati itakayofikiwa katika kikao hiki itasaidia kuondoa malalamiko kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa watumishi na Taasisi za Umma zinazosimamia upatikanaji wa haki” amesisitiza.

Aidha, Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa malalamiko yanayotolewa na wananchi yanapaswa kufanyiwa kazi kwa kutoa elimu kwa wanataaluma na watumishi wa umma wote ili wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia maadili ya utendaji kazi na miiko ya taaluma zao.

Vilevile, ameelekeza viongozi katika Ofisi yake kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu. Pia, Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma zinapaswa kusimamia na kuchukua hatua stahiki kwa wakati kwa wale wanaokiuka maadili ya taaluma zao kwa lengo la kuendelea kujenga imani kwa wananchi na kuongeza uwajibikaji na usikivu.

Ofisi yangu itaendelea kushirikiana na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma kutoa ushauri wa kitaalamu pale itakapohitajika; kutoa ushauri katika mapitio na maboresho ya Kanuni za Maadili za Kitaaluma; kujenga uelewa kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma; na kushirikiana nanyi katika kuleta mabadiliko ya fikra miongoni mwa watumishi wa umma ambao nao ni wanataaluma katika Taasisi mnazoziwakilisha” amesema.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu – UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi amesena lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu, kutambua changamoto zilizopo, mafanikio na masuala mapya yanayojitokeza katika utumishi wa umma kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na kuwahudumia wananchi vizuri zaidi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua kikao kazi leo jijini Dodoma cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kilichowashirikisha wadau kutoka Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji, Taasisi Simamizi za Maadili ya Kitaaluma na watumishi kutoka kwenye Wizara mbalimbali na taasisi za kitaaluma. 


Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza alipokuwa akifungua kikao kazi hicho leo jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi leo jijini Dodoma cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora.


Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika akitoa utambulisho wa washiriki wa kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi hicho.


Sehemu ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo jijini Dodoma.


Sehemu ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na  Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akisisitiza jambo kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi leo jijini Dodoma cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akimkabidhi Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama Mwongozo wa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2023 na Mwongozo wa Kushughulikia Mrejesho wa Wananchi wa mwaka 2023 mara baada ya kufungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo jijini Dodoma. 


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwa na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakisubiri kumpokea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ili akifungue kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akimpokea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipowasili kufungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora leo katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.


 

Sunday, September 17, 2023

MHE KIKWETE: WATUMISHI WA UMMA JIEPUSHENI NA MIKOPO KAUSHA DAMU

              




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa  Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwani Kikwete (Mb) amewatahadharisha Watumishi wa Umma kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la " Kausha Damu" huku akisisitiza kuwa mikopo ya aina  hiyo imekuwa ikidhalilisha na kutweza utu wa Watumishi katika Jamii.

 

Mhe.Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Busega Mkoani Simiyu wakati akihitimisha ziara yake aliyoianza mapema wiki hii Mkoani Mara.

 

Amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya watumishi wa umma   kuathirika kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri  utoaji wa  huduma bora kwa wananchi. 

 

Amefafanua kuwa mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye Taasisi za Kifedha  zisizotambulika imekuwa na  riba kubwa ambayo huwapelekea Watumishi wengi kushindwa kuwasilisha  marejesho na hivyo kupelekea kuuzwa kwa  nyumba au vitu vya thamani  wanavyo vimiliki.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kikwete amewataka Watumishi kuanza kutumia Mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans)  ulioanza kutumika kuanzia Septemba 1, 2023  ambao unamuwezesha Mtumishi wa Umma kuomba mkopo pasipo kufika kwenye Taasisi ya Kifedha au Tawi la Benki.

 

Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais -  UTUMISHI na Utawala Bora ili kumsaidia Mtumishi wa Umma  kupata mikopo katika Taasisi za Kifedha zinazotambulika na Mwajiri ili kumuepusha  Mtumishi  kukopa sehemu ambazo humpeleka Mtumishi   kunyang'anywa kadi ya Benki.

 

Aidha, Mhe.Kikwete amewataka watumishi hao kujenga nidhamu ya matumizi ya pesa wanazopata kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya  baadaye baada ya kustaafu.

 

Amewasihi kujiwekea malengo ya kujiandaa kustaafu kuanzia leo ili wasije kuwa wateja wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Kuendeleza Jamii ( TASAF ).

 

"Hakikisheni hata hela mnazozikopa mnafanya uwekezaji wa kimkakati kwa ajili ya kujitegemea kiuchumi katika siku za mbeleni" amesisitiza Mhe.Kikwete

 

Katika ziara hiyo Mhe.Kikwete mbali ya kuzungumza na watumishi wa umma katika mikoa ya Mara na Simiyu pia  amekagua miradi mbalimbali 

inayotekelezwa na TASAF pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF

 


 Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa  na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega mara baada ya kukagua zahanati iliyotekelezewa na mradi wa TASAF