Monday, June 17, 2019

MHE. MKUCHIKA AWAHIMIZA WAUMINI WA KIKRISTO KUCHANGIA HUDUMA ZA KIJAMII KWA MAENDELEO YA TAIFA

Waumini wa dini ya kikristo nchini wamehimizwa kutoa mchango kwenye maeneo mbalimbali  hususan katika kujenga makanisa, shule na hospitali ambazo zitatumika kutoa huduma za kijamii kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa   Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.
Mhe. Mkuchika amewataka waumini wa kanisa hilo kuchangia maendeleo ya kanisa, kwani mafundisho ya kanisa yanawataka waumini kutoa kwa hiyari ili kuisaidia Serikali kuboresha huduma za kijamii ambazo ndio chachu ya maendeleo ya taifa.
 “Kanisa linatufundisha ni heri kutoa kuliko kupokea kwa kuwa tukitoa tunapata thawabu kwa Mungu” Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa, Kanisa la Anglikana Tanzania ni Kanisa la tatu kuwa na wafuasi wengi lakini katika shughuli za maendeleo limekuwa nyuma sana.
“Kanisa letu limekuwa nyuma katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo hususan kujenga makanisa mengine, shule na hospitali. Ni lazima tubadilike kwa sababu Wamissionari wa Kigeni tuliowategemea sasa hawapo” Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika alihamasisha uchangiaji wa ujenzi wa Kanisa ambapo takribani milioni nne zilipatikana.
Naye, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Given Gaula amemshukuru Mhe. Mkuchika kwa kujitoa katika kuhamasisha uchangiaji wa maendeleo ya kanisa na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuleta  maendeleo katika Taifa.
“Pamoja na masuala ya kiimani na kiroho, Kanisa la Anglikana limejipanga kutoa elimu katika jamii kwa kujenga shule ya sekondari na ufundi katika Wilaya ya Chemba na shule ya awali katika eneo la Bicha” Dkt. Gaula amesema na kuongeza kuwa, kanisa hilo lina miradi mingine kama mradi wa hosteli na vikundi vya kijamii vya kujikwamua kiuchumi vinavyojulikana kama Church Community Mobilization Process.
Ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi imehudhuriwa na viongozi wa serikali wa wilaya ya Kondoa, washirika wa Kanisa Anglikana kutoka Marekani, Uingereza na vikundi mbalimbali vya dini kutoka kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akizungumza wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.



Baadhi ya Mashemasi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) wakati wa ibada ya kuwawekea mikono iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.



Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Rochester, Uingereza, James Langstaff na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula, wakiwawekea mikono Mashemasi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa wakati wa ibada iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Dkt. Given Gaula akizungumza wakati wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemashi na Makasisi wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.





Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga kabla ya kuanza kwa  wa ibada ya kuwawekea mikono Mashemasi na Makasisi wa  Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kondoa iliyofanyika katika kanisa la Mchungaji Mwema, Wilayani Kondoa.



No comments:

Post a Comment