Thursday, June 17, 2021

AFISA MALALAMIKO ANAYETOA SIRI ZA MALALAMIKO ANAKOSA SIFA YA KUWA MTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 17 Juni, 2021

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema, Afisa Malalamiko yeyote katika Taasisi ya Umma ambaye anashindwa kutunza siri za malalamiko yanayowasiliswa kwenye dawati lake anapoteza sifa ya kuwa Mtumishi wa Umma muadilifu.

Dkt. Michael amezungumza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka zake za Serikali za Mitaa ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia malalamiko ya wananchi katika taasisi zao.

Dkt. Michael amesema Maafisa Malalamiko katika Taasisi za Umma wanapaswa kujenga imani kwa watumishi na wananchi wanaowasilisha malalamiko kwenye ofisi zao kwa kutunza siri zinazohusu malalamiko yanayowasilishwa.

Amefafanua kuwa, uvujishaji wa siri zinazohusu malalamiko yaliyowasilishwa ni ukiukwaji wa Kanuni Na. 8 ya Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005 ambayo inawataka Watumishi wa Umma kutunza siri zinazohusu utekelezaji wa majukumu yao.

Dkt. Francis ameongeza kuwa, Afisa Malalamiko hapaswi kuwa na upendeleo wakati wa kushughulikia malalamiko, na badala yake anapaswa kuwa mshauri kwa watumishi na wananchi wanaowasilisha malalamiko katika ofisi yake. 

Sanjari na hayo, Dkt. Michael ametoa wito kwa Maafisa Malalamiko kutoa namba za simu za kiganjani ili kutoa fursa kwa watumishi na wananchi wenye malalamiko kuyawasilisha na kufanyiwa kazi.

Aidha, ametoa maelekezo kwa waajiri wote nchini kusimamia Utekelezaji wa Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Malalamiko ya Wananchi katika Utumishi wa Umma wa Mwaka 2012 ili kuhakikisha ofisi au dawati la ushughulikiaji wa malalamiko linakuwepo kwenye taasisi zao, ikiwa ni pamoja na kuwateua watumishi wenye sifa stahiki kushughulikia malalamiko ya wananchi.

Awali akimkaribisha Dkt. Francis kufungua mafunzo hayo kwa Maafisa Malalamiko, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika alisema, mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji maafisa wanaoratibu ushughulikiaji wa malalamiko ili wafahamu namna wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao.

Bi. Leila ameongeza kuwa, maafisa hao watapata mafunzo kuhusu utekelezaji wa Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Malalamiko,uandaaji wa taarifa za malalamiko na watapewa elimu kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, haki na wajibu, dhana ya Utawala Bora, namna ya kuwahudumia na kuwadhibiti walalamikaji wa aina mbalimbali. 

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Ukuzaji Maadili inatoa mafunzo ya siku tatu ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi yanayohudhuriwa na Maafisa Malalamiko kutoka Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa na Mamlaka zake za Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kwa maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi na CBE.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa  ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa  yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.


Baadhi ya Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko kwa maafisa hao yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.


Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika akieleza lengo la mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya Wananchi katika Utumishi wa Umma yanayotolewa kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa. 


Mkurugenzi Idara ya Uratibu na Maboresho, Ofisi ya Rais-Ikulu Bw. Apolinary Tamayamali akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kufungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Malalamiko wa Sekretarieti za Mikoa  ya Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Singida, Morogoro na Iringa, mara baada ya kufungua mafunzo ya ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi kwa maafisa hao yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.



 

Wednesday, June 16, 2021

OFISI YA RAIS UTUMISHI YATOA ELIMU YA MASUALA YA KIUTUMISHI KWA MADIWANI ILI KUHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA UMMA

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 16 Juni, 2021

Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wametoa elimu ya masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Rufiji kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Akizungumzia ujio wa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi hao wa CCM, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mchengerwa amesema kwa kuwa viongozi hao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi ni vizuri wakayaelewa vema majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika maeneo yao ya utawala. 

“Nina imani mkitoka hapa mtakuwa ni chachu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kutoka kwa Watumishi wa Umma kwani Serikali imewaajiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza. 

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, hivyo  amewaomba viongozi hao ambao ni wasimamizi wa haki za watumishi na wananchi katika maeneo yao, wawahimize watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

“Dhamira ya Mhe. Rais ni kuhakikisha haki za msingi za Watumishi wa Umma zinatekelezwa ili kuwajengea ari ya kutoa huduma bora kwa umma,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa rai kwa viongozi hao kutumia elimu waliyoipata kuhamasisha watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Wilaya ya Rufiji, Bw. Hassan Makoba amesema, wakiwa wasimamizi wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 watawahamasisha Watumishi wa Umma kutimiza wajibu wao ili wananchi wapate huduma bora.

Bw. Makoba ameongeza kuwa, wameona nia ya dhati ya Serikali katika kusimamia upatikanaji wa haki za Watumishi wa Umma hususan upandishwaji vyeo na malipo ya madai yao mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara, hivyo watakuwa ni mabalozi wazuri wa kuelezea nia njema ya serikali ili watumishi wawajibike ipasavyo.

Viongozi hao wamepata elimu kuhusiana na usimamizi wa Sera na Miongozo katika Utumishi wa Umma, utaratibu wa upandishwaji madaraja, taratibu za uhamisho, stahili za watumishi (Madai ya malimbikizo ya mishahara na stahili nyinginezo) Uhamasishaji wa ujumuishwaji wa masuala ya Anuai za Jamii (Jinsia, Ulemavu, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa) pamoja na uzingatiaji wa Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2005.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake Mhe. Deogratius Ndejembi.


Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao katika Ofisi yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea masuala ya kiutumishi na utawala bora kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya Rais-UTUMISHI   kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa elimu ya masuala ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.


Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Bi. Mwanaamani Mtoo akitoa elimu ya masuala ya Sera na Miongozo mbalimbali ya kiutumishi kwa Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliotembelea Ofisi Rais-UTUMISHI iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI baada ya kikao na  Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Rufiji waliofika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi .

Thursday, June 10, 2021

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA MAAFISA UTUMISHI WANAODANGANYA KUWASILISHA MADAI YA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA OFISI YA RAIS-UTUMISHI

 Na. Veronica Mwafisi-Kondoa

Tarehe 10 Juni, 2021

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu Maafisa Utumishi wote watakaobainika kuwadanganya Watumishi wa Umma wenye madai ya malimbikizo ya mishahara kuwa wamewasilisha madai yao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kufanyiwa kazi wakati sio kweli.

Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa leo Wilayani Kondoa, Mhe. Ndejembi amesema kuna baadhi ya Maafisa Utumishi hawatekelezi wajibu wao kikamilifu na kusababisha Ofisi ya Rais Utumishi kutupiwa lawama na Watumishi.

Amewaelekeza Wakurugenzi kuwasimamia Maafisa Utumishi wao ili watekeleze majukumu yao ipasavyo ikiwemo la kushughulikia fomu za madai ya malimbikizo ya watumishi hao ili yafanyiwe kazi kwa haraka kwa lengo la kupunguza malalamiko ya watumishi ambayo yanashusha ari ya kutekeleza majukumu yao kikamifu.

“Madai ya Watumishi yakichelewa kulipwa, mnasingizia fomu ziko UTUMISHI wakati sio kweli, mara nyingi fomu hizi zinakuwa ziko kwenu Wakurugenzi sababu Maafisa Utumishi wenu kujifanya miungu watu,’” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Mhe. Ndejembi amesema madai ya Watumishi ni haki yao ya msingi  kwani wanatumia jasho lao kulitumikia taifa, hivyo wanastahili kulipwa na si hisani.

Akizungumzia changamoto ya upandishwaji madaraja kwa watumishi, Mhe. Ndejembi amewaelekeza Maafisa Utumishi nchini kuhakikisha wanatenda haki kwa wanaostahili kupandishwa madaraja kama Mhe. Rais Samia Suhuhu Hassan alivyoelekeza.

“Tujitume kwa bidii tusimuangushe Mhe. Rais ambaye ameonyesha nia thabiti ya kuwajali Watumishi wa Umma katika kulinda maslahi na haki zao za msingi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi kuwa makini katika mchakato wa kuwapandisha madaraja watumishi wanaostahili kupanda na kuongeza kuwa Afisa Utumishi yeyote atakayebainika kusababisha mtumishi kutopata haki hiyo atachukuliwa hatua.

Mhe. Ndejembi amewasisitiza Watumishi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika Utumishi wa Umma ili kuboresha utendaji kazi utakaowezesha utoaji wa huduma bora kwa umma.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Sezaria Makota, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kufika Wilayani humo na kuzungumza na Watumishi ambapo pia amesisitiza uwajibikaji kwa watumishi hao.

Mhe. Makota amesema hapendezwi kuwepo kwa madai ya malimbikizo ya mishahara na ya upandishwaji vyeo ambayo hayajafanyiwa kazi na Maafisa Utumishi katika Wilaya yake na kuongeza kuwa hatosita kuwachukulia hatua watakaoshindwa kutekeleza maelekezo.

Mhe. Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Wilayani Kondoa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.  

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao leo wilayani Kondoa chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi leo wilayani Kondoa yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo. 

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Mji Kondoa Bw. Msoleni Dakawa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Mustapha Semwaiko akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na Watumishi wa Wilaya hiyo leo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wilayani humo.