Wednesday, May 19, 2021

MHE. MCHENGERWA AWATAKA MAAFISA WA TAKUKURU KUTUNZA SIRI ZA WANAOTOA TAARIFA ZA VITENDO VYA RUSHWA


 

MHE. MCHENGERWA AWATAKA MAAFISA WA TAKUKURU KUTUNZA SIRI ZA WANAOTOA TAARIFA ZA VITENDO VYA RUSHWA

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 19 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) kutotoa siri za wananchi wanaowasilisha taarifa za uwepo wa vitendo vya rushwa kwenye taasisi hiyo ili ziweze kufanyiwa kazi.

Akizungumza wakati wa kikao kazi chake na Viongozi wa TAKUKURU leo jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi (CP) Salum Hamduni kuhakikisha vyanzo vya taarifa za rushwa vinalindwa ili kuhamashisha wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazoiwezesha Serikali kulinda rasilimali za taifa.

Mhe. Mchengerwa amehimiza uadilifu kwa Watumishi wa TAKUKURU hususan kwenye eneo la utunzaji siri za watoa taarifa ili kuwajengea wananchi imani ya kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Utoaji wa siri za wanaowasilisha taarifa za vitendo vya rushwa, unahatarisha usalama wao, hivyo Mkurugenzi Mkuu uanze na suala hili ili tubaini watumishi wote wanaotoa siri za watoa taarifa na kuwachukulia hatua za kinidhamu.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewaasa watumishi hao kutenda haki wanaposhughulikia vitendo vya rushwa ili kutoitia dosari Ofisi hiyo inayoaminiwa na wananchi.

Kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais juu ya taasisi hiyo kujikita moja kwa moja katika majukumu yake, Mhe. Mchengerwa amewakumbusha Viongozi hao kutekeleza maelekezo hayo ipasavyo kwa kushughulikia masuala yanayohusiana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi na si vinginevyo.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali ina imani na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Hamduni na Naibu wake Bi. Neema Mwakalyelye walioapishwa leo na Mhe. Rais, na ndio maana wamepewa dhamana ya kuiongoza taasisi hiyo nyeti.

Akizungumza na viongozi wa TAKUKURU kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza watendaji wa TAKUKURU kutofanya kazi zisizoihusu TAKUKURU kama ambavyo Mhe. Rais na Waziri Mchengerwa wamekuwa wasisitiza.

Mhe. Ndejembi ameitaka TAKUKURU kuhakikisha inayakamilisha kwa wakati mashauri ya msingi yanayoihusu taasisi hiyo na kwa yale yasiyokuwa na msingi yafutwe ili kutoa fursa kwa taasisi hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yenye tija kwa taifa.

Kwa upande wake. Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amekiri kupokea maelekezo ya Mhe. Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi ndani ya muda aliolekeza.

Ili kutekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa wakati, CP Hamduni amewataka watumishi wake kujitoa kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU ili kufikia malengo ya taasisi hiyo.

Mhe. Mchengerwa amefanya kikao kazi na Viongozi wa TAKUKURU mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo na Naibu wake kuapishwa na Mhe. Rais-Ikulu Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuhimiza uwajibikaji na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais aliyedhamiria taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa weledi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akikaribishwa na Watumishi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam alipowasili kwa ajili ya kikao kazi chake na Viongozi wa TAKUKURU kilicholenga kuhimiza uwajibikaji. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Watumishi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam alipowasili kwa ajili ya kikao kazi chake na Viongozi wa TAKUKURU kilicholenga kuhimiza uwajibikaji. Kulia kwake Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na Viongozi Wakuu wa TAKUKURU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi chake na Viongozi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika kikao kazi na Viongozi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Viongozi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni akiahidi kutekeleza maelekezo aliyopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Viongozi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha nembo ya TAKUKURU aliyokabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni baada ya kikao kazi cha Waziri huyo na Viongozi wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa TAKUKURU mara baada ya kikao kazi cha Waziri huyo na Viongozi hao wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiagana na Viongozi Wakuu wa TAKUKURU mara baada ya kikao kazi cha Waziri huyo na Viongozi hao wa TAKUKURU leo Jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.

 


 

Wednesday, May 12, 2021

MHE. MCHENGERWA AZITAKA TAASISI ZA KIFEDHA KUTOA MIKOPO KUPITIA HATIMILIKI ZINAZOTOLEWA NA MKURABITA

 

Na. James K. Mwanamyoto-Zanzibar

Tarehe 12 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka taasisi za kifedha nchini kutoa mikopo kwa wananchi wenye hatimiliki za kimila zinazotolewa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ili kuwawezesha wananchi hao kuendesha shughuli zao na kuinua kipato.

Akikabidhi hatimiliki hizo kwa baadhi ya wananchi wa Shehia ya Welezo, Zanzibar, Mhe. Mchengerwa amesema, hatimiliki hizo zinalenga kutoa fursa kwa wananchi kupata mikopo itayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara ili kuboresha maisha yao.

“Taasisi za kifedha zitambue hatimiliki hizi na kupunguza masharti ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kukopa na kuongeza mtaji.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akiwa katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara, eneo la Darajani Wilaya ya Mjini, Mhe. Mchengerwa amezitaka pia taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wajasiriamali waliorasimisha biashara zao na kuongeza kuwa, mikopo hiyo itawaongezea mitaji ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.

Kutokana na uwepo wa kituo hicho, Mhe. Mchengerwa amehimiza zoezi la urasimishaji biashara lisichukue muda mrefu ili kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kurasimisha biashara zao.

Akieleza mchango wa ofisi yake katika zoezi la urasimishaji biashara, Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum amesema kituo hicho kimejengwa ili kuondoa changamoto za urasimishaji walizokuwa wakikutana nazo wafanyabiashara wadogo.

Dkt. Salum ameongeza kuwa kutokana na faida za uwepo wa kituo hiki, Serikali imedhamiria kujenga kituo kama hiki Pemba ili wananchi wa eneo hilo nao waweze kunufaika.

Naye Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe amesema utekelezaji wa MKURABITA Zanzibar umewanufaisha wananchi wa Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu za biashara ambapo hivi sasa wanazo takwimu sahihi za maendeleo ya biashara zao.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Ajira ofisi ya Zanzibar.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Shehia ya Welezo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya MKURABITA, Zanzibar.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa hatimiliki kwa mmoja wa wananchi wa Shehia ya Welezo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya MKURABITA, Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wajasiriamali (hawapo pichani) wanaopata huduma katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara, eneo la Darajani Wilaya ya Mjini wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya MKURABITA, Zanzibar. Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum.

Baadhi ya Wajasiriamali wa Zanzibar waliorasimisha biashara zao kupitia kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara, eneo la Darajani Wilaya ya Mjini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo Zanzibar.

Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akitoa taarifa ya utekelezaji ya kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara eneo la Darajani Wilaya ya Mjini, wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya MKURABITA, Zanzibar.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha moja ya hatimiliki alizozitoa kwa wananchi wa Shehia ya Welezo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya MKURABITA, Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akihimiza zoezi la urasimishaji wa biashara kufanyika kwa wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara, eneo la Darajani Wilaya ya Mjini. Wanaomsikiliza ni Watendaji wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar na Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe.