Friday, August 4, 2023

WANANCHI 72,000 KUNUFAIKA NA KITUO CHA AFYA KINACHOJENGWA KUPITIA MIRADI YA TASAF WILAYANI KWIMBA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Kwimba

Tarehe 04 Agosti, 2023.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema wananchi zaidi ya 72,000 wa Kata tano za Sumve, Mantare, Ngula, Wela na Mwabomba Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza watanufaika na kituo cha afya kinachojengwa kupitia Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara baada ya kituo hicho kukamilika.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Budushi, Kata ya Sumve, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF. 

Waziri Simbachawene amesema lengo la Miradi ya TASAF ni kupambana na umaskini na kuboresha Maisha ya Watanzania kwani taifa lolote linahitaji nguvukazi ya watu wenye afya ili waweze kufanya kazi bila kuwa na changamoto za kiafya.

Waziri Simbachawene amesema pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia TASAF kushughulika na miradi ya kupambana na umaskini lakini inatambua juhudi zinazofanywa na halmashauri kupitia fedha za mapato ya ndani katika kuendeleza miradi hiyo.

“Kama Ofisi, tumeona juhudi zenu, hivyo tuendelee kushirikiana katika kukamilisha majengo haya na kusimamia miradi hiyo kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali kwani uhitaji wa kituo cha afya katika halmashauri hii ni muhimu sana ili tuwe na wananchi wenye afya njema watakaoweza kutekeleza majukumu yao pasipo kuwa na changamoto yoyote ya kiafya,’’ Mhe. Simbachawene amesema.

Aidha, Waziri Simbachawene amewasihi wananchi kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuwa na afya njema na kutafuta fedha nyingi za miradi kwa ajili ya kuleta maendeleo katika taifa letu.

Akitoa salamu za TASAF, Meneja Mradi wa TASAF, Bw. John Stephen amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ni moja kati ya halmashauri zenye walengwa wengi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini na wamefanikiwa kujengewa majengo mengi hivyo amewasisitiza kufanya kazi kwa bidii.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Mhe. Lameck Hole ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kwa kutimiza ahadi ya kuwajengea Kituo cha Afya.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Budushi, Kata ya Sumve, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mara baada ya kukagua majengo ya afya ya uzazi na maabara yanayoendelea kujengwa kwa ufadhili wa TASAF na fedha za mapato ya ndani za Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo.


Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kukagua majengo ya afya ya uzazi na maabara yanayoendelea kujengwa kwa ufadhili wa TASAF na fedha za mapato ya ndani za Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ndatwa Ludigija (kushoto) katika Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Simbachawene iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Mkurugenzi wa Miradi  ya Jamii-TASAF, Bw. John Stephen akitoa salamu za TASAF kwa wananchi na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (aliyenyoosha kidole) akikagua jengo la afya ya uzazi (marternity Ward) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (watatu kutoka kulia) akitoka kukagua jengo la afya ya uzazi (marternity Ward) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo. Wengine ni watendaji wa TASAF na viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.


Mwonekano wa jengo la afya ya uzazi (marternity Ward) linalojengwa kupitia mradi wa TASAF katika Kijiji cha Budushi, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.



No comments:

Post a Comment