Wednesday, August 9, 2023

SERIKALI YAJA NA MFUMO WA KUONDOKANA NA SUALA LA UPUNGUFU WA WATUMISHI - WADAU WASISITIZWA KUTOA MAONI KUUBORESHA

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 9 Agosti, 2023

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi amewataka washiriki katika kikao kazi cha kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu kushiriki kikamilifu katika kikao hicho ili kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo huo utakaowezesha kubaini mahitaji halisi ya watumishi katika Taasisi za Umma.

Bw. Mkomi ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi hicho kwa Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote, Baadhi ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti za Mikoa, Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri na Manipaa, Wakurugenzi na Maofisa kutoka OR -TAMISEMI, Wataalam kutoka Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri za Manispaa.

Bw. Mkomi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais- UTUMISHI baada ya kuona tatizo la upungufu wa watumishi  katika maeneo mengi iliona kuna haja ya kutafuta suluhu kwa kutengeneza Mifumo ya kisayansi itakayosaidia katika uchambuzi wa mahitaji ya watumishi ili kutatua changamoto hiyo.

Amesema Mfumo mmojawapo uliotengenezwa ni huo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ambao ndio unawasilishwa kwa wadau kwa lengo la kupata maoni na mapendekezo  ya kuboresha ili uwe na tija kwa ustawi wa taifa, hivyo amewasisitiza kuhakikisha wanajadili kwa umakini ili Serikali iweze kuondokana na changamoto hii.

Amesema kuwa, kila mwaka Serikali imekuwa ikiandaa ikama lakini haitoshi kwasababu utaratibu unaotumika ni wa kawaida wa kuajiri tukifikiri ndio suluhu pekee na kuongeza kuwa ni wakati sasa wa kuangalia namna ya kufanya, kwani inatakiwa kujua watumishi wangapi wanahitajika wapi, wakafanye nini na baada ya kujua hayo itapatikana nafasi nzuri ya kuboresha.

“Kila Mkurugenzi utakayemuuliza atakwambia watumishi hawatoshi, Mfumo huu wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu utatupa kujua idadi ya watumishi walioko katika kila kituo cha kazi na upungufu au ziada iliyopo ili kuwa na idadi ya watumishi sahihi katika sehemu sahihi za utekelezaji wa majukumu yao.” Bw. Mkomi amesisitiza.

Akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda ameelezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kupata maoni toka kwa wadau hao ili kuboresha mfumo huo katika Utumishi wa Umma kwa masilahi mapana ya taifa.

Kikao kazi hicho kilichoanza leo kinafanyika kwa muda wa siku nne ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa ili kuwezesha wadau kuwasilisha maoni sahihi. Mada hizo ni pamoja na Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu kwa nadharia na vitendo, Uchambuzi wa Mahitaji ya Watumishi kwa Kuzingatia Uzito wa Majukumu na Namna ya Kuandaa Majukumu na Viwango vya Kazi.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akifungua kikao kazi leo jijini Dodoma cha wadau kutoka Serikalini kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.


Sehemu ya wadau kutoka Serikalini wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi wakati akifungua kikao kazi cha wadau hao jijini Dodoma kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.


Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi kufungua kikao kazi cha wadau kutoka Serikalini kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau kutoka Serikalini mara baada ya kufungua kikao kazi cha wadau ha oleo jijini Dodoma kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akiagana na Wakurugenzi wa Ofisi yake mara baada ya kufungua kikao kazi cha wadau kutoka Serikalini kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.


Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Miundo na Wakala za Serikali, Bi. Jane Kaji akiwasilisha mada ya Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu kwa nadharia leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha wadau kutoka Serikalini kilicholenga kupata maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu ili kuondokana na suala la upungufu wa watumishi serikalini.

 




No comments:

Post a Comment