Tuesday, June 29, 2021

MFUMO WA KIDIGITALI WA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO UJULIKANAO KWA JINA LA SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI WAZINDULIWA RASMI

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 29 Juni, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI.

Akizindua mfumo huo leo ofisini kwake jijini Dodoma, Mhe Mchengerwa amesema, uzinduzi wa mfumo huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma na wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huo utamuwezesha yeye na wasaidizi wake kupata taarifa za malalamiko yanayohusu huduma zinazotolewa katika taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na kupokea maoni, pongezi kwa Mhe. Rais na Ofisi yake.

Amefafanua kuwa, mfumo huo pia utawawezesha kufanya ufuatiliaji wa namna malalamiko yanavyopokelewa na kufanyiwa kazi na kuongeza kuwa, mfumo unampa nafasi ya kutoa maelekezo ya ushughulikiwaji wa malalamiko hayo pale anapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo.

“Popote nitakapokuwa, iwe safarini, ofisini au nyumbani, nitaweza kuona malalamiko yote yanayowasilishwa ofisini kwangu na namna yanavyofanyiwa kazi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema mfumo huo ni rafiki kwa watumiaji, hivyo kila mtumishi na mwananchi mwenye hoja ataweza kuutumia bila changamoto yoyote kwa njia ya tovuti kwa anuani ya www.swu.utumishi.go.tz, simu janja kwa kupakua SWU kutoka kwenye play store, na simu ya kawaida kwa kutumia msimbo wa *152*00# na kuchagua namba 9 na baadae namba 2 ili kuwasilisha malalamiko.

Aidha, katika kuadhimisha siku 100 za utendaji kazi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mhe. Mchengerwa amezindua Jarida la Utumishi la Habari na Matukio ili kuuhabarisha umma namna Ofisi yake inavyomsaidia Mhe. Rais kutekeleza jukumu la usimamizi wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, jarida hilo litauhabarisha umma juu ya mafanikio ya Serikali yanayopatikani na utekezaji wa majukumu kwenye eneo la Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Jarida hili litakuwa linatoka kila baada ya miezi mitatu na litakuwa na maudhui ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa na matukio mbalimbali ambayo ofisi imekuwa ikiyafanya kwa masilahi ya umma hapa nchini,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Mhe. Mchengewa ametoa wito kwa watumishi wenye habari za kiutumishi na utawala bora zenye manufaa kwenye utumishi wa umma na umma kwa ujumla kuwasilisha taarifa hizo ili ziweze kuchapishwa kwenye jarida hilo.

Awali akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzindua mfumo huo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, amefarijika kuona utekelezaji wa maelekezo ya kuanzishwa kwa mfumo wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi na wananchi umekamilika.

Mhe. Ndejembi amesema, anakumbuka siku ya kwanza ya Mhe. Mchengerwa kuripoti kazini, alitoa maelekezo ya kufanya kazi kidigitali katika kusikiliza kero, kupokea malalamiko na maoni ambayo yatatumika kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, hivyo amefurahi kuona mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI kuzinduliwa rasmi.

Akitoa neno la utangulizi kabla ya uzinduzi, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amempongeza Mhe. Mchengewa kwa kuwahamasisha watendaji wake kutekeleza majukumu kwa njia ya kidijitali ili kurahisiha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma na wananchi.

“Mfumo huu wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ni zao la hamasa yako ya utatuzi wa changamoto za watumishi na wananchi zitakazowasilishwa kupitia mfumo huo”, Dkt. Ndumbaro ameeleza.

Mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI uliobuniwa na wataalam wa ndani wa TEHAMA umelenga kupunguza au kuondoa kabisa kero na malalamiko ya Watumishi wa Umma na wananchi kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani ameazimia katika utawala wake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi, ujulikananao kama SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) aliouzindua leo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kushoto kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijiandaa kubonyeza kitufe leo jijini Dodoma ili kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU). Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa    kuzungumza na vyombo vya habari kabla ya kuzindua rasmi mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.


Mwonekano wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) uliozinduliwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waandishi wa Habari kwenye uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumishi na wananchi ujulikanao kwa jina la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (SWU) leo jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akionyesha jarida la Utumishi Habari na Matukio mara baada ya kuzindua jarida hilo leo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi akishiriki uzinduzi wa jarida hilo na kushoto kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.

 

 


 



WAZIRI MCHENGERWA AITAKA WHC KUJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU NA SI ZA KIBIASHARA ILI KUWASAIDIA WATUMISHI WA UMMA

 

Na. Veronica Mwafisi-Dar es Salaam

Tarehe 29 Juni, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameutaka uongozi wa Watumishi Housing Company (WHC) iliyo chini ya ofisi yake kutokuwa na mlengo wa kibiashara kwa kujenga nyumba za gharama nafuu za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma wa kada za chini ili kutatua changamoto ya makazi inayowakabili.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo kwa Mkurugenzi Mtendaji Watumishi Housing Dkt. Fredy Msemwa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, Watumishi Housing itaendelea kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo Watumishi wa Umma nchini wenye kipato cha kawaida watamudu kuzinunua.

Mhe. Mchengerwa ameuhimiza uongozi wa Watumishi Housing kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba kwenye maeneo mbalimbali ili kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ya kutatua changamoto zote zinazowakabili Watumishi wa Umma nchini. 

“Jengeni nyumba za kutosha zenye gharama nafuu katika miji mikubwa, Makao Makuu ya nchi Dodoma na maeneo ambayo yana changamoto ya miundombinu na uhaba mkubwa wa makazi ya watumishi”, Mhe. Mchengerwa amehimiza.

Ameongeza kuwa, dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi ikiwemo uhaba wa nyumba za kuishi imelenga kujenga ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma na hatimaye wajivunie kuwa Watumishi wa Umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Dkt. Fred Msemwa amesema ofisi yake itatekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa kuongeza ubunifu ili kujenga nyumba za gharama nafuu kwa watumishi kwenye majiji na maeneo yenye uhaba wa nyumba hususani vijijini na kwenye maeneo yenye huduma za shule na afya. 

Dkt. Msemwa ameahidi kuwa, ofisi yake itaendelea kubuni miradi itakayowahakikishia Watumishi wa Umma pamoja na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu kwa kuzingatia kipato chao. 

Aidha, amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuipongeza ofisi yake kwa ubunifu wa miradi ya nyumba ambazo zimewawezesha Watumishi wa Umma katika maeneo yenye miradi ya nyumba za Watumishi Housing kupata nyumba za kupanga na kuishi.

Watumishi Housing Company (WHC) ilianzishwa na Serikali mwezi Februari 2013 na kuanza kufanya kazi kama Mfuko wa Nyumba za Watumishi na Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii mwaka 2014 na mpaka hivi sasa imefanikiwa kujenga nyumba 917 katika mikoa 19.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na watumishi wa Watumishi Housing Company (WHC) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya Watumishi wa WHC wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing (WHC) Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ofisi yake kwa Mhe. Mchengerwa (wa kwanza kulia) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Gezaulole Kigamboni na Magomeni jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mradi wa WHC wa Gezaulole Kigamboni wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Watumishi Housing Company jijini Dar es Salaam.


Mwonekano wa baadhi ya nyumba za Mradi wa Gezaulole uliopo Kigamboni jijini Dar es Salaam unaomilikiwa na Watumishi Housing Company (WHC).


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa sehemu ya juu ya wazi ya mradi wa nyumba Magomeni na Mtendaji Mkuu wa WHC Dkt. Fred Msemwa wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.


Mwonekano wa Mradi wa nyumba wa Magomeni House unaomilikiwa na Watumishi Housing Company (WHC) eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.



Saturday, June 26, 2021

MWANAHABARI RIZIKI ABRAHAM AAGWA JIJINI DODOMA KWA KUPONGEZWA KWA UCHAPAKAZI WAKE ENZI ZA UHAI WAKE

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 26 Juni, 2021

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bi. Mary Mwakapenda kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro, amepongeza utendaji kazi wa marehemu Riziki Abraham wa kuitekeleza vema kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE wakati wa uhai wake kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, maarifa na weledi.

Bi. Mary Mwakapenda ametoa pongezi hizo, wakati wa Misa Takatifu ya kumuombea marehemu Riziki Abraham iliyofanyika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma.

Bi. Mary amefafanua kuwa, marehemu Riziki alikuwa ni mtumishi mwema aliyetekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kuongeza kuwa, alikuwa akishirikiana vema na wanatasnia wenzie kutekeleza majukumu ya kitaifa, hivyo anapaswa kuenziwa na wanahabari kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mhe. Rais ya KAZI IENDELEE. 

Naye, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Habari - MAELEZO Bw. Rodney Thadeus akizungumza kwa niaba ya Mkutugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, amesema, Bi. Riziki alikuwa ni mwepesi wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Ajira hivyo, taifa limempoteza mtu muhimu ambaye bado alikuwa akihitajika kuuhabarisha umma. 

“Tangu nimfahamu marehemu Riziki sijawahi kusikia juu ya taarifa yoyote ambayo aliitoa na ikaleta sintofahamu katika jamii, huu ni uthibitisho tosha wa umahiri wake”, alisisitiza Bw. Thadeus. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini Tanzania (TAGCO) Bw. Abdul Njaidi, amesema marehemu Riziki, alifanikiwa kutekeleza jukumu kubwa la kutangaza shughuli zinazotelelezwa na taasisi zote alizozitumikia  ikiwa ni pamoja na mafanikio yaliyopatikana.

Bw. Njaidi ameeleza kuwa, marehemu Riziki alikuwa hawezi kufanya jambo la kitaaluma bila kuuliza au kuomba ushauri wa kitaaluma hivyo ameacha mfano mzuri wa kuigwa.

Bw. James Mkuwa, aliyekuwa akishirikiana na marehemu Riziki kutunza nyumba ya mapradri “Betania House” iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam amesema, marehemu alikuwa ni mtu asiyejikweza kwani baada ya kifo chake ndio amefahamu marehemu alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Amesema, marehemu Riziki mpaka mauti yanamkuta amekuwa akitekeleza jukumu lake la kutoa habari kwani muda wote alikuwa akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake tangu aanze kuumwa na kuongeza kuwa, hakika amefia taaluma yake ya habari.

Kwa niaba ya Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Mhandisi Samweli Tanguye amesema, marehemu Riziki ameifanya kazi ya kuitangaza taasisi kwa kiwango cha kutukuka kwa kipindi cha miaka 10.

Mhandisi Tanguye ameeleza kuwa, marehemu amezunguka nchi nzima bara na visiwani kuitangaza taasisi, hivyo ameingia katika historia kwa kuwa msemaji wa kwanza wa Sekretarieti ya Ajira ambaye alitekeleza majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio makubwa.

Kutokana na maelezo kuhusu umahiri wa marehemu Riziki Abraham enzi za uhai wake, Padri Gaetano Maswenya ametoa pole kwa mume wa marehemu na familia ya wanahabari kwa kuondokewa na mtu makini na shabiki mwenzie wa yanga, hivyo ametoa wito kwa wanatasnia na  waumini kuendelea kumuombea.

Marehemu Riziki Veneranda Abraham amefanya kazi Ofisi ya Makamu wa Rais Mwaka 2005 hadi 2010 na mwezi Novemba 2011, alihamishiwa Ofisi ya Rais - Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Cheo ambacho amekitumikia  hadi umauti ulipomfika tarehe 22 Juni, 2021. 


Mume wa marehemu Riziki Abraham, Ndugu Joseph Michael Kiringo (wa kwanza kulia) na mwanae wa kike (wa pili kulia kwake) wakiwa na waombolezaji wengine kwenye ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Mwili wa marehemu Riziki Veneranda Abraham ukiwa mbele ya madhabahu ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma kwa ajili ya ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu huyo iliyofanyika katika kanisa hilo. 



Padri Gaetano Maswenya akihubiri wakati wa misa ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bi. Mary Mwakapenda akiwasilisha salamu za rambirambi za Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 


Katibu Mkuu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Tanzania (TAGCO) Bw. Abdul Njaidi salamu za rambirambi kwenye ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma.

 


Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Habari - MAELEZO Bw. Rodney Thadeus akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 


Mhandisi Samweli Tanguye akielezea namna walivyofanya kazi na marehemu Riziki Abraham wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu huyo, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 


Afisa Utumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bi. Neema Kivugo akisoma wasifu wa marehemu Riziki Veneranda Abraham wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu Riziki Veneranda Abraham iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma. 


Jeneza lenye Mwili wa marehemu Riziki Veneranda Abraham likiwa mbele ya madhabahu ya Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Gaspar De Buffalo lililopo Makole jijini Dodoma wakati wa ibada takatifu ya kumuombea na kumuaga marehemu huyo iliyofanyika katika kanisa hilo.



Wednesday, June 23, 2021

VIONGOZI TOENI MOTISHA KWA WATUMISHI WA UMMA ILI WAONGEZE UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI WAO

 Na. James Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 23 Juni, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu, amewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kujenga utamaduni wa kuwapatia motisha Watumishi wa Umma ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao kwa lengo la kuwajengea ari ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na Serikali kupitia taasisi zake.

Mhe. Ummy ametoa wito huo wakati akifunga kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Mhe. Ummy amefafanua kuwa, kutoa motisha kwa Watumishi wa Umma ni mojawapo ya jitihada za kuboresha utendaji kazi wa Watumishi wa Umma, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuzingatia hilo. 

“Motisha si lazima iwe fedha au kitu kikubwa, yaweza kuwa ni kutambua juhudi za Mtumishi wa Umma hata kwa kumpatia cheti ili mtumishi huyo aendelee kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa,” Mhe. Ummy amesisitiza.

Amewaasa viongozi hao, kuwapatia motisha watumishi walio chini yao na wale ambao majukumu yao hayatoi fursa ya kusafiri kikazi mara kwa mara, hivyo amewataka kutojiangalia wenyewe. 

Aidha, Mhe. Ummy amewataka viongozi hao, kuwa na utamaduni wa kurekebisha mienendo mibaya ya Watumishi wa Umma wanaowasimamia ili watumishi hao waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi.

Amesema ni wazi kuwa, binadamu wanatofautiana kitabia na kimaadili na ikumbukwe kuwa, mtumishi anaweza kuwa anakabiliwa na changamoto za kifamilia ambazo zinakwamisha utendaji kazi wake, hivyo ni wajibu wa viongozi kutatua changamoto hizo ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Sanjari na hilo, amewataka viongozi hao ambao ni wasimamizi wa rasilimaliwatu kuwa na utaratibu wa kuwasikiliza Watumishi wa Umma ili kujenga mahusiano mazuri mahala pa kazi.

“Ninyi ni wasimamizi wa rasilimaliwatu, licha ya kusimamia kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo, mnapaswa kuzingatia utu kwa kuwasikiliza watumishi ikiwa ni pamoja na kufahamu mapungufu yao ili kuyarekebisha,” Mhe. Ummy amehimiza. 

Awali akimkaribisha Mhe. Ummy kuzungumza na viongozi hao, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi hao wakirejea kwenye maeneo yao ya kazi kubuni mikakati ya namna ya kutoa motisha kwa watumishi wanaowasimamia ili kuwajengea ari ya utendaji kazi. 

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, motisha si lazima iwe fedha, wanaweza kutengeneza vyeti au kuwaandikia barua ikiwa ni sehemu ya kutambua utendaji kazi wa watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa bidii, maarifa, ufanisi na weledi.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kilihudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kutoka kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretariti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, na kaulimbiu ya kikao hicho ilikuwa ni: “Utumishi wa Umma unaozingatia Haki na Wajibu kwa Maendeleo ya Taifa”.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kabla ya kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu – UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.


Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akikabidhi cheti cha utendaji kazi mzuri kwa mmoja wa wakilishi wa taasisi iliyoshinda, kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini kabla ya Waziri huyo kufunga rasmi kikao kazi cha mwaka cha viongozi hao kilichofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

 



Monday, June 21, 2021

SERIKALI HAITOMVUMILIA KIONGOZI ATAKAYESABABISHA WATUMISHI NA WANANCHI KUKOSA HAKI ZA MSINGI


Na. James Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 21 Juni, 2021

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali haitomvumilia Mkuu wa Idara yeyote katika taasisi ya umma atakayesababisha mtumishi kukosa stahili yake na mwananchi kukosa huduma bora. 

Mhe. Mchegerwa ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma. 

Mhe. Mchengerwa amewataka wakuu hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza viongozi katika taasisi za umma kutenda haki kwa watumishi walio chini yao na kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Amewaasa viongozi hao kutatua kero za watumishi na wananchi pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi na kuongeza kuwa, pindi atakapofanya ziara katika maeneo yao hategemei kukuta foleni kubwa ya wananchi wakisubiri huduma pasipokuwa na sababu ya msingi. 

“Mimi, Naibu Waziri wangu na Watendaji wa Ofisi yangu tukifanya ziara katika taasisi yako, hatutegemei kukuta mlolongo wa foleni ya wanananchi wakisubiri huduma pasipo na matumaini yoyote,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza. 

Katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi na wananchi wanapohitaji huduma katika taasisi za umma, Mhe. Mchengerwa ameanzisha mfumo wa kielektroniki unaoitwa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ambao unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni ili kutoa fursa kwa watumishi na wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kufanyiwa kazi. 

“Kupitia mfumo huu, nitakuwa na uwezo wa kuona malalamiko yanayowasilishwa popote nitakapokuwa na kufanya ufuatiliaji wa namna yalivyofanyiwa kazi na ofisi yangu,” Mhe. Mchengerwa ameongeza. 

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Festo Dugange amesema Mhe. Rais Samia amekuwa akisisitiza mara kwa mara matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi kwenye maeneo yao ya kazi. 

Ameongeza kuwa ili matokeo hayo yaonekane, Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu hawana budi kusimamia utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma kwa ufanisi. 

Kikao kazi hicho cha siku mbili kinahudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kutoka kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretariti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

Mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo Miundo ya Maendeleo ya Utumishi wenye Vyeo Tisa (9), Masuala Muhimu ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma, Utekelezaji wa Mfumo Mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara, Usimamizi wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na mafunzo kuhusu uongozi. 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma alipokuwa akifungua kikao kazi cha wakuu hao kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Baadhi ya Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akifungua kikao kazi cha wakuu hao kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Festo Dugange akitoa salam za ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kufungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Festo Dugange na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro wakiwa katika kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitambulisha washiriki wa kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi wakati wa kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na TAMISEMI mara baada ya kufungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa J.K. Nyerere, Chuo cha Mipango jijini Dodoma.


 

Friday, June 18, 2021

TAASISI YA UONGOZI KUTOA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO KIUTENDAJI VIONGOZI WOTE KUANZIA WIKI IJAYO

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 18 Juni, 2021

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute) imeandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Viongozi wa Kisiasa na Viongozi Watendaji katika Utumishi wa Umma yatakayotolewa kuanzia wiki ijayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka viongozi kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo, mapema leo mara baada ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, wajumbe wa bodi hiyo waliteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, miongoni mwa viongozi watakaopatiwa mafunzo ni Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya,  Wakurugenzi Wasaidizi na  Wakurugezi wa Idara katika Taasisi za Umma.

Ameongea kuwa, mafunzo hayo elekezi yatakayotolewa yatawaandaa viongozi hao kutambua majukumu yao na kutekeleza kikamilifu wajibu wao, kwa mujibu wa Viapo vya Ahadi ya Uadilifu katika Utumishi wa Umma walivyovitoa.

Mhe. Mchengerwa amesema, ukienda katika mataifa mengine ya Afrika Taasisi ya UONGOZI inasifika kwa kuwaandaa viongozi mbalimbali na imekuwa ni tegemezi katika kujenga uwezo wa viongozi barani Afrika, hivyo Serikali imeona ni vema taasisi hii itumike ipasavyo kutoa mafunzo kwa viongozi nchini ili waweze kuzingatia Miiko ya Uongozi na Maadili ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewakumbusha viongozi wote kuwa, cheo ni dhamana hivyo kila kiongozi anaowajibu wa kuhakikisha anakitumia cheo chake kwa uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya taifa.

“Viongozi tambueni uongozi ni dhamana hivyo mnapaswa kuongeza ufanisi kiutendaji kwa kushiriki mafunzo yatakayotolewa na Taasisi ya UONGOZI hivi karibuni” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inatarajia kuwa, baada ya viongozi kupata mafunzo haya ya kuwajengea uwezo, hakutakuwa na kiongozi yeyote atakayekwenda kinyume na Kanuni za Maadili ya Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005.

Mara baada ya Mhe. Mchengerwa kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI, Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt. Stergomena Tax amemshukuru Mhe. Rais kwa kumteua yeye pamoja na wajumbe wengine wa bodi hiyo na kuahidi kuwa, watahakikisha wanatekeleza jukumu kubwa la Taasisi ya UONGOZI la kuwajenga viongozi ambao wataleta maendeleo endelevu katika taifa.

Dkt. Tax amesema, wao kama bodi wanatambua umuhimu wa kuwa na viongozi mahiri wenye uwezo wa kuiwezesha nchi kupata maendeleo katika sekta mbalimbali nchini, hivyo watatekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kutumia uwezo na uzoefu walionao.

Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI iliyozinduliwa leo inaundwa na Mwenyekiti Dkt. Stergomena Tax, Makamu Mwenyekiti Dkt. Laurean Ndumbaro na wajumbe wengine ni Prof. Penina Mlama, Prof. Samuel Wangwe, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mhe. Ritta Swan, Bi. Susan Mlawi, Bi. Lina Soiri na Bw. David Walker.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI na wageni waalikwa wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Bw. Kadari Singo akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) kabla ya waziri huyo kuzindua Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI uliofanyika leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na  Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI  wakionyesha vitendea kazi alivyowakabidhi leo kwa ajili ya  kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI,  Dkt. Stergomena Tax akitoa shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa mara baada ya Waziri huyo kuzindua bodi hiyo leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI na watumishi wa taasisi hiyo mara baada ya  kuzindua bodi hiyo leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya UONGOZI leo katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.