Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameelekeza suala la
nidhamu katika Utumishi wa Umma ni namba moja na lipewe uzito unaostahili ili
kujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu.
Dkt. Ndumbaro aliyasema hayo
wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Umma mikoa ya Singida,
Shinyanga na Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
2017.
Alisema Watumishi wanaokiuka
maadili ya Utumishi wa Umma wasionewe aibu bali wachukuliwe hatua zinazostahili
haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo
katika Utumishi wa Umma.
“Ni lazima hatua za
kinidhamu zichukuliwe mapema kwa mtumishi asiye na maadili kwani bila kufanya
hivyo tutajenga Utumishi wa Umma usio na maadili kwa siku zijazo,” Dkt.
Ndumbaro alisema na kuongeza kuwa mtumishi wa Umma anapofanya kosa ni lazima
lifanyiwe kazi na mwajiri wake katika kituo cha kazi alichopo badala ya
kumhamishia katika kituo kingine.
Aidha, Dkt, Ndumbaro
amewataka waajiri kuwapongeza watumishi wanaofanya vizuri katika utumishi wao
ili kujenga nidhamu ya utendaji kazi.
“Tusifikirie kutoa adhabu tu
kwa Watumishi wa Umma wasio na maadili bali tunatakiwa kutambua mchango na ubunifu
wa wale wanaofanya vizuri kwa kuwapongeza. Tuelewe kuwa kuwapongeza watumishi
wa umma sio lazima tuwape fedha, bali kuwatambua kwa kuwapa vyeti vya utendaji
mzuri na kuwaandikia barua za pongezi kwa kutambua juhudi zao katika
kuwahudumia wateja hivyo kuwapa morali ya kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia
weledi na bidii zaidi, aliongeza.
Kwa upande mwingine Dkt.
Ndumbaro amewataka Waajiri kupitia taarifa za Watumishi mara kwa mara ili
kuweka kumbukumbu ya taarifa sahihi na safi katika Mfumo wa Taarifa za
Kiutumishi na Mishahara (HCIMS).
“Waajiri katika Utumishi wa
Umma ni jukumu lenu kuwakumbusha na kushirikiana na Maafisa Utumishi kupitia
taarifa za watumishi mara kwa mara na kuwaondoa katika mfumo wa HCIMS Watumishi
wa Umma ambao hawastahili kuwepo ili kuepukana na suala la watumishi hewa na
taarifa zisizo sahihi (chafu).” Dkt. Ndumbaro alisisitiza.
Wiki ya Utumishi wa Umma
huadhimishwa kila mwaka na kufikia kilele chake tarehe 23 Juni ambapo mwaka huu
inaadhimishwa kwa viongozi mbalimbali katika Utumishi wa Umma kukutana ili kufanyia
kazi masuala ya Menejimenti ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, pamoja
na wadau ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika huduma
wanazopokea, ndani na nje ya utumishi wa umma ili kuleta mabadiliko zaidi
katika Utoaji huduma na kufikia malengo ya nchi.
No comments:
Post a Comment