Thursday, January 30, 2025

Wednesday, January 29, 2025

SERIKALI YAZIDI KUWAPANDISHA VYEO MAELFU YA WATUMISHI

Na Lusungu Helela-Dodoma 

Serikali imesema kwamba katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 imewapandisha vyeo watumishi 180,000 wakiwemo watumishi walioathirika na mwongozo wa upandaji madaraja wa miaka minne.

Mhe. Sangu amesema hayo  wakati akijibu swali la  Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Janejelly Ntate aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukwamua watumishi walioathiriwa na mwongozo wa upandaji madaraja wa miaka minne.

Aidha, katika utekelezaji wa Ikama na Bajeti ya Mwaka 2023/2024, Serikali imewapandisha vyeo watumishi zaidi ya 232,530 wakiwemo walioathirika na zoezi hilo, uhakiki wa vyeti feki na watumishi hewa



NAIBU WAZIRI MHE. SANGU:MFUMO WA UPIMAJI UTENDAJI KAZI KUJAZWA KILA WIKI NA WATUMISHI NA SIO VINGINEVYO

 Lusungu Helela-Dodoma 

Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe. Deus Sangu amesema Mfumo  wa upimaji wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma ujulikanao kama PEPMIS utaendelea kujazwa kwa wiki kama ilivyopangwa.

Mhe. Deus Sangu amesema hayo Bungeni leo Jummane Januari 29, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Sophia Mwakagenda aliyetaka kujua kwa nini watumishi wa afya wasijaze ripoti za utendaji kila mwezi badala ya kila wiki ili wapate muda zaidi kuhudumia wagonjwa




Monday, January 27, 2025

WATUMISHI WA OFISI YA RAIS-UTUMISHI WASISITIZWA KUZINGATIA ITIFAKI NA DIPLOMASIA KATIKA UTENDAJI KAZI

Na. Mwandishi Wetu

Tarehe 27 Januari, 2025.

Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wamesisitizwa kuzingatia Itifaki na Diplomasia katika utendaji kazi Ili kujenga heshima ya ofisi kwa manufaa ya nchi.

Wito huo umetolewa leo Januari 27, 2025 na Balozi Nelson Lyimo (mstaafu) wakati akifanya wasilisho kuhusu Itifaki na Diplomasia kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Balozi Lyimo amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ni muhimu kwa Taifa la Tanzania kwa kuwa inasimamia rasilimaliwatu, hivyo Watumishi wake wanatakiwa kuzingatia Itifaki na Diplomasia wakati wote wanapotekeleza majukumu yao katika ofisi hiyo.

Amewasisitiza Watumishi kuwa wasikivu kwa wateja wanaowahudumia na kuona namna ya kuwasaidia kupata majibu au suluhisho la suala ambalo mteja husika ameliwasilisha.

“Niwaombe kila mtumishi wa ofisi hii ajipime namna anavyotoa huduma kwa wateja kwani ndio kipimo cha tabia njema wakati wa utendaji kazi, jambo ambalo litaenda kuitangaza ofisi vizuri kwa maslahi mapana ya taifa,” amesisitiza Balozi Lyimo.

Akihitimisha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Bw. Musa Magufuli alimshukuru Balozi Lyimo kwa kutoa elimu hiyo kwa watumishi hao ambayo itaboresha utendaji kazi kwa watumishi wao.

Ofisi ya Rais-UTUMISHI iliandaa utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watumishi wake kila Jumatatu ya wiki kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali katika Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ustawi wa Taifa.

Balozi Nelson Lyimo (mstaafu) akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu Itifaki na Diplomasia kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli (aliyesimama mbele kulia) akitoa shukrani kwa  Balozi Nelson Lyimo (aliyesimama mbele kushoto) mara baada ya Balozi huyo kuhitimisha mada kuhusu Itifaki na Diplomasia wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala ya utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.





Friday, January 24, 2025








 

KAMATI YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA SEKRETARIETI YA AJIRA

 Na.Lusungu Helela — DODOMA

  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma  kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuhakikisha michakato ya ajira inafanyika kwa ufanisi na kwa uwazi wa hali ya juu.  

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo , Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma kwa niaba ya Kamati yake wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi ya mwezi Septemba 2024 hadi Januari  2025.

 

Mhe. Dkt. Mhagama mesema kitendo cha usaili kufanyika katika ngazi za mikoa badala ya kuwalazimu waombaji kazi wote kufika jijini Dodoma kumeleta  ahueni kubwa kwa waombaji kazi hao hususani wale waliotoka kwenye familia maskini.

 

 Hapo awali wazazi walilazimika kuuza ardhi au ngombe ili kijana wao aweze kusafiri kuja jijini Dodoma kwa ajili ya kufanya usaili ila ubunifu wa kufanya usaili kimkoa umerahisishia. Amesema  Mhe. Dkt. Mhagama amesema

 

Amesisitiza kuwa  utaratibu huo umeondoa usumbufu pamoja na kumfanya Muombaji  kazi  kutokutumia gharama ya usafiri kwa ajili ya kufika jijini Dodoma  kufanya usaili

 

 Akizungumzia matumizi ya mfumo wa Ajira Portal kwa waombaji kazi Mhe.Dkt. Mhagama  amesema mfumo juo umeondoa dhana ya upendeleo wa kupata ajira katika Utumishi wa Umma na kuchagiza ushindani miongoni mwa waombaji kwani hutoi fursa ya kuonana ana kwa ana na wahusika

 

Nimekuwa nikipokea simu nyingi kutoka kwa Watoto wa  familia masikini wa kutoka vijijini wakiwa wamepata ajira serikalini pasipo kumjua yeyote aliyepo serikalini amesisitiza Mhe.Dkt. Mhagama

 

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amesema ajira katika Utumishi wa Umma zinapatikana kwa ushindani kutokana na idadi kubwa ya wasomi iliyopo lakini nafasi ni chache

 

Ametumia fursa hiyo kuwaomba Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Mabalozi wa Sekretariet ya Ajira Katika Utumishi wa Umma kwa kuwaeleza wananchi kuwa ajira katika Utumishi wa Umma hazihitaji kumjua yeyote na cha msingi ni kufuata taratibu zilizowekwa na Sekretarieti hiyo wakati wa  kuomba kazi.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria , Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akizungumza na Wajumbe mara baada ya Naibu Waziri Mhe. Deus Sangu kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kwa niaba ya Waziri Mhe. George Simbachawene

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene  akijibu hoja zilizotolewa na Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria mara baada ya Wajumbe hao kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora

 



Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria  wakimsikiliza  Naibu Waziri Mhe. Deus Sangu mara baada ya  kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kwa niaba ya Waziri Mhe. George Simbachawene

 



Naibu Waziri , Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu  akiwasilisha  taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kwa niaba ya Waziri Mhe. George Simbachawene mbele ya Wajumbe wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria

 



Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika kikao  kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi ya Ofisi hiyo kilichofanyika leo Jijini Dodoma

 





 Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria  wakijadili mara baada ya  kupokea  taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kwa niaba ya Waziri Mhe. George Simbachawene

 

 

 

WAZIRI SIMBACHAWENE: USHINDANI WA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA NI JAMBO LISILOEPUKIKA KWA SASA

 Na.Lusungu Helela - SINGIDA  

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amesema suala la ushindani katika  upatikanaji wa ajira katika Utumishi wa Umma ni jambo lisiloepukika kutokana na idadi kubwa ya wasomi iliyopo kwa sasa 

 

Amesema dhamira hiyo ya kuhakikisha waombaji kazi wote wanafanya usaili kunasaidia  kuwapata watumishi wenye sifa stahiki katika utumishi wa umma na kuondoa dhana ya upendeleo iliyokuwa imejengeka miongoni mwa watu


 Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo alipotembelea kituo cha usaili wa kada ya Ualimu  Mkoani  Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo,  ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 na Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 inayoelekeza  kuwa ajira katika utumishi wa umma  zipatikane kwa ushindani


 "Hakuna palipoandikwa kuwa watu wote waliosoma wataajiriwa na Serikali ndio maana ajira za serikali ni za  ushindani kwani waliosoma  ni wengi lakini nafasi ni chache.

 Amesema Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma mara baada ya kutangaza kazi za  Ualimu, waombaji   201,707 walijitokeza kuomba  lakini baada ya mchujo kutokana na baadhi kutokukidhi vigezo ikiwemo kutokuweka  baadhi ya vyeti kama ilivyoelekezwa walichujwa  hadi kufikia waombaji 170,000

 

Hata hivyo,  Mhe.Simbachawene ametumia fursa hiyo kuwasihi waombaji kazi kuhakikisha wanaweka vyeti vyao vinavyotakiwa ili kuepuka na mchujo katika hatua za  awali.

 Usaili wa kada ya Ualimu unaendelea katika vituo mbalimbali nchi nzima na utakamilika  Februari 24 Mwaka huu.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene  akizungumza na wasailiwa wakati alipotembelea kituo cha usaili wa kada za Ualimu  Mkoani  Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo.

 

 


Baadhi ya Wasailiwa wa kada ya Ualimu wakimskiliza  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene  wakati alipotembelea kituo cha usaili wa kada za Ualimu  Mkoani  Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo, 

 



Mkuu wa Mkoa wa  ya Singida Mhe. Halima Dendego akizungumza leo wakati alipotembelea kituo cha usaili wa kada za Ualimu  Mkoani  Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo, 

 

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida  Mhe. Halima Dendego     pamoja na viongozi wengine  mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kutembelea kituo cha usaili wa kada za Ualimu  Mkoani  Singida ili kujionea mwenendo wa zoezi hilo,  

 

 

 

 

 

 

 

Wednesday, January 22, 2025

WAZIRI SIMBACHAWENE AMJIBU MHE. FREEMAN MBOWE

 Na Lusungu Helela - SINGIDA 

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amemshukia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Mhe. Freeman Mbowe kuhusiana na  hoja yake aliyoitoa ya kubeza juhudi ya Serikali ya kutaka kuondoa umaskini wa watu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kuwagawia fedha.

 

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo  leo mara baada ya kukagua miradi mbalimbali  ya maendeleo iliyotekelezwa kupitia  TASAF Mkoani Singida ambapo amesema TASAF ni mpango mmojawapo wa uwezeshaji wananchi  kiuchumi lakini Serikali ina mipango lukuki.

 

"Jana (juzi)  nilikuwa nasikiliza  ule Mkutano wa Uchaguzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  nilimsikia Mhe. Mbowe wakati akitoa taarifa ya Chama hicho kuwa  "Serikali ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) inataka kuondoa umaskini wa watu kupitia TASAF kwa kuwagawia fedha" 

 

"Ni kweli  Serikali ya CCM inataka kuondoa umaskini wa watu wake hasa wale wasiojiweza kabisa kwa kuwasaidia kifedha lakini pia Serikali hii inatumia mfuko wa TASAF kuondoa changamoto zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja  kwa kwenda kurekebisha miundombinu pamoja na vikwazo katika maisha yao ikiwemo ujenzi  wa vivuko ili waweze kwenda mashambani kwa urahisi hususan wakati wa msimu wa mvua"  amesisitiza Mhe. Simbachawene

 

Pia, Mhe. Simbachawene amesema Serikali kupitia  TASAF imekuwa ikijenga vituo vya afya mahali ambako kuna zahanati zisizokidhi mahitaji ya wananchi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya lengo likiwa ni kupambana na umaskini

 

"Nataka nimwambie Kaka yangu Mbowe kwamba  TASAF ni mpango mmojawapo wa kuwezesha wananchi wetu kiuchumi lakini Serikali yetu ina mipango mingi sana  na tunayo Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi" amesisitiza Mhe. Simbachawene 

 

Amesema Serikali ina  Mfuko wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ambapo kuna njia mbalimbali za kuwagusa kiuchumi ikiwemo  vijana na makundi mbalimbali lengo likiwa ni kupambana na umasikini na kuwapa ahueni katika hali zao za maisha

 

Ameongeza kuwa "Tuna mpango wa kuwawezesha kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa  Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ambapo asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hupelekwa kwa ajili ya kukopesha makundi hayo.

 

Mbali na mipango hiyo Mhe. Simbachawene ameitaja mipango mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa ni  utoaji  ruzuku kwenye  pembejeo za kilimo, utoaji wa mikopo ya elimu ya juu,  ujenzi wa Shule za Sekondari kila Kata pamoja  na Shule za Msingi kila Kijiji, utoaji wa mikopo ya Elimu ya juu pamoja na matibabu bure kwa wazee

 




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene  akizungumza na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Kinyakaya kilichopo katika   Mkoa wa  Singida

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akikagua Mradi wa upandaji  miti kupitia TASAF uliotekelezwa katika Kijiji cha Kinyakaya kilichopo katika   Mkoa wa  Singida



Baadhi ya Wanufaika wa TASAF wakimsikiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene wakati akizungumza nao katika Kijiji cha Kinyakaya kilichopo katika   Mkoa wa  Singida

 



Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe akizungumza na walengwa  wa TASAF katika  Kijiji cha Kinyakaya kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na walengwa hao Mkoani Singida 

 

 




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akiwa ameongoza na Mkuu wa Wilaya ya Singida  Mhe. Godwin Gondwe mara baada ya kuwasili Mkoani Singida kwa ajili ya ziara ya kikazi 

 

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiagana na wanufaika wa mpango wa kuondoa umasikini mara baada ya kuzungumza  nao katika Kijiji cha Kinyakaya kilichopo katika Mkoa wa  Singida