Wednesday, April 24, 2024

BIDII, WELEDI NA UADILIFU WAIBUA MFANYAKAZI HODARI OFISI YA RAIS-UTUMISHI

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 24 Aprili, 2024.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bibi Hilda Kabissa amewasisitiza watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu huku wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma katika kuwahudumia wananchi kwa ustawi wa taifa.

Mkurugenzi Kabissa ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi na watumishi hao kilicholenga kuzungumzia masuala ya kiutumishi na kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo.

Bibi Kabissa amesema watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wanapaswa kuwa mfano bora kwa wengine katika kuzingatia maadili wakati wa utekelezaji wa majukumu yao wakiwa ofisini na hata nje ya ofisi.

Awali akiongoza kikao kazi chake na watumishi wa Ofisi yake kabla ya kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi aliwasisitiza watumishi wa ofisi yake kumchagua mfanyakazi hodari kwa kuzingatia vigezo vya mfanyakazi hodari vilivyowekwa na sio kupendeleana.

Kwa upande wake Afisa Utumishi Bw. Juma Ijumaa ambaye ndiye alichaguliwa kuwa mfanyakazi hodari wa ofisi hiyo, amewashukuru viongozi na watendaji wa ofisi hiyo kwa kuwaongoza watumishi wote katika kusimamia maadili, kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kulitumikia taifa jambo ambalo limemfanya kuwa mfanyakazi hodari wa ofisi hiyo.

Aidha Bw. Ijumaa amewashukuru wafanyakazi wenzake kwa kumpa ushindi wa kwanza kwa kishindo na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa watumishi wa umma na wananchi wanaofuata huduma katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI akiamini kuwa kitendo hicho kitaendelea kujenga taswira nzuri zaidi ya ofisi pamoja na kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, mtumishi aliyeshika nafasi ya pili, Bi. Joyce Atanas ameahidi kuendelea kuwa mwadilifu na mchapa kazi katika kipindi chote cha utumishi wake ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Naye, Bw. Elias Mwandu, aliyeshika nafasi ya tatu, hakusita kuwashukuru watumishi wenzake kwa kumchagua kuwa miongoni mwa tatu bora wa Ofisi hiyo na kuongeza kuwa, kitendo hicho hakimaanishi kuwa wao si watumishi bora kiutendaji kwani amekuwa akishirikiana nao katika kuwahudumia wananchi na watumishi wa umma nchini.

Akihitimisha kikao kazi hicho, Mkurugenzi Kabissa, amewahamasisha watumishi wote wa ofisi hiyo ambao hawakubahatika kuchaguliwa kwa mwaka huu wa 2024, kujipanga kwa mwaka utakaofuata kwani anaamini utendajikazi mzuri wa kila mtumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akizungumza na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa ofisi hiyo kilicholenga kuzungumzia masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kuhusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Sehemu ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kuhusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Mussa Magufuli akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) kuzungumza na watumishi kuhusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bibi Hilda Kabissa akimtangaza mfanyakazi hodari aliyechaguliwa na watumishi wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024.

Sehemu ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao kuhusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Wafanyakazi hodari wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI (mstari wa kwanza) wakiwa katika kikao kazi kilichohusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Mtumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Evarist Venant, akichangia hoja wakati wa kikao kazi kilichohusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Mussa Magufuli (hayupo pichani) kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) kuzungumza na watumishi hao kwenye kikao kazi kilichohusu masuala ya kiutumishi na kuchagua Mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024 kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Mfanyakazi Hodari wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Ijumaa akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa ofisi hiyo, mara baada ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora kwa mwaka 2024.

Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakikamilisha zoezi la kupiga kura kumchagua mfanyakazi Hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2024.


Wakurugenzi wasaidizi na wawakilishi wa wafanyakazi bora kutoka katika Idara na Vitengo, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakishuhudia zoezi la kuhesabu kura za kumpata mfanyakazi Hodari wa ofisi yake kwa mwaka 2024.








No comments:

Post a Comment