Thursday, February 29, 2024
Monday, February 26, 2024
WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TASAF ITOE KIPAUMBELE KWA KAYA MASKINI ZENYE WATU WENYE ULEMAVU
Na.Lusungu Helela
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuweka nguvu zaidi katika kuziingiza kaya maskini zenye watu wenye ulemavu kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ili nao waweze kujiinua kiuchumi na kufikia malengo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona mpango huo unagusa makundi mengi zaidi yenye uhitaji.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Kinywang’anga Wilaya ya Iringa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.
Amesema TASAF imekuwa mkombozi kwa wananchi wanaonufaika kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na mpango huo huku akisisitiza kuwa katika awamu ijayo iwaangalie zaidi watu wenye ulemavu kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi kulingana na changamoto walizokuwa nazo.
"Kaya zenye watu wenye ulemavu na hazijiwezi kimaisha zina mzigo mara mbili ukilinganisha na kaya zisizojiweza na hazina watu wenye ulemavu, hivyo ni lazima kaya zenye walemavu zipewe kipaumbele zaidi" amesisitiza Mhe.Simbachawene
Amesema moja ya dhamira Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kaya maskini zenye walemavu zinapata uhakika wa milo mitatu kama zilivyo kaya nyingine masikini.
Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha zinazotoka zinafika kila mahali na kwa walengwa sahihi hasa waishio vijijini katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya TASAF.
Amesema miradi inayotekelezwa na TASAF inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kushirikisha jamii katika uhalisia wake akisema huo ndio msingi wa viongozi wa Tanzania.
“Lengo la miradi la TASAF ni kuondoa umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kaya, ndio maana kuna wanufaika wanaopewa fedha za moja kwa moja ili kuwapa ahueni katika hali zao za maisha,” amesema Mhe. Simbachawene.
Katika ziara hiyo, Mhe. Simbachawene alitembelea mradi wa ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Kinywanga’nga akiguswa na utekelezaji wa mradi huo ambao unakwenda kuinua sekta ya uvuvi na kugusa moja kwa moja maisha ya wafugaji.
Awali Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda Mfupi kutoka TASAF, Bw. Paul Kijazi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina afua tatu katika jamii ikiwemo ya kuhawilisha fedha inayotolewa kwa wananchi wa kaya zisizokuwa na uwezo wa kufanya kazi wakiwemo wazee.
“Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tuna vijiji 134 vyote vinahawilishiwa fedha, tumeshaleta shilingi bilioni 3.663 katika awamu ya pili ya TASAF kwa walengwa, lakini pia tulileta fedha shilingi bilioni 1.09 kwa ajili ya vifaa vilivyotumika katika ajira za muda mfupi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mara baada ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF mkoani Iringa.
Sehemu ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika eneo la Migori mkoani Iringa.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Veronica Kessy akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao mkoani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na baadhi ya wananchi akikagua mradi wa birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo mkoani Iringa
Sehemu ya birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo mkoani Iringa.
Kibao kinachoonesha moja ya mradi uliotekelezwa na walengwa wa TASAF
Friday, February 23, 2024
WAZIRI SIMBACHAWENE ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO, AITAKA IONGEZE KASI KUSANIFU MIFUMO
Na Lusungu Helela- Iringa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene aridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) huku akiitaka iongeze kasi zaidi katika kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa eGA-Kituo cha Iringa ambapo amewataka Watumishi hao kuhakikisha Serikali inaendeshwa kidigitali kwenye kila nyanja kupitia mifumo wanayoisanifu.
Amesema eGA ni taasisi muhimu katika dunia ya sasa ambapo Serikali inahitaji mapinduzi ya TEHAMA ili itoe huduma zake kwa wananchi kiurahisi na kwa haraka
“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa, hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma” amesema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka, mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.
Aidha, Mhe. Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.
Vile vile, amewasisitiza watumishi wa eGA kuhakikisha mifumo inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa.
Sehemu ya Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akitoa maelezo kuhusu Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na Watumishi hao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisaini kitabu mara baada ya kuwasili Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo hicho.
WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TAKUKURU KUWADHIBITI WACHEZEAJI RASILIMALI ZA NCHI
Na.Lusungu Helela- Iringa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kudhibiti mianya ya rushwa katika fedha za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali nchini ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.
Ametoa kauli hiyo leo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi za TAKUKURU mkoani Iringa ambapo amemtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ifikapo mwezi Juni mwaka huu kama ilivyopangwa ili watumishi wa taasisi hiyo waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri.
“Tukawe watu wa kupekenyua pekenyua kwenye miradi hii inayotekelezwa na serikali kwani kuna watu wanatumia vibaya fedha za serikali, penyeni huko kuwadhibiti ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati na kwa viwango kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Mhe. Simbachwene
Amefafanua kuwa TAKUKURU inatakiwa kuhakikisha inasimamia na kudhibiti fedha zisipotee lakini bila kuathiri maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini.
"Palipo na shilingi ya Mama Samia waambieni TAKUKURU tupo ila katika kufanya haya tusikwamishe maendeleo" amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene ameitaka Taasisi hiyo kuwachukulia hatua wale wote wanaokwamisha shughuli za maendeleo na hivyo kukwamisha utendaji wa Rais Mhe. Dkt. Samia suluhu Hassan.
"Dhibitini mianya ya kuchezea rasilimali za nchi ikiwemo fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sehemu ambako fedha imesimamiwa vizuri matokeo mazuri yameonekana, naomba niwasihi kuendelea kuwadhibiti ipasavyo wachezea fedha za maendeleo" amesema Mhe. Simbachawene.
Ameongeza kuwa anataka kuona TAKUKURU ikichukua hatua kwa wale wote wanaokwamisha nia nzuri ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kama hatua hizo hazichukuliwi basi miradi mizuri iliyotekelezwa ionekane ili wananchi wazidi kuwa na imani na serikali yao.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni amesema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja hadi kukamilika kwake mwezi Juni mwaka huu utagharimu zaidi ya shilingi billioni 1.4.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo huku akiipongeza TAKUKURU kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia fedha za serikali zisipotee kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watu.
Sehemu
ya Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja
linaloendelea kujengwa mkoani humo
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Iringa (hawapo pichani) kabla ya Waziri Simbachawene mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja linaloendelea kujengwa mkoani humu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi wakati akikagua ujenzi wa jengo la TAKUKURU Mkoani Iringa linaloendelea kujengwa Mkoani humo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akiwa na baadhi ya Watumishi wa TAKUKURU Mkoani Iringa
wakati akikagua ujenzi wa jengo la TAKUKURU Mkoani Iringa linaloendelea
kujengwa Mkoani humo.
Wednesday, February 21, 2024
MHE. SIMBACHAWENE AELEKEZA KUSIMAMISHA MISHAHARA YA VIONGOZI WALIOSHINDWA KUSIMAMIA WATUMISHI KUTEKELEZA ZOEZI LA PEPMIS
Na. Lusungu Helela-Iringa
Tarehe 21 Februari, 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi
kusimamisha mishahara ya Viongozi walioshindwa kuwasimamia watumishi wao
kujisajili na kujaza mipango kazi yao katika Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji
Kazi kwa Watumishi wa Umma na Taasisi za Umma (PEPMIS/PIPMIS) na kukwamisha
utekelezaji wa zoezi hilo lenye masilahi mapana katika utumishi wa umma na
taifa kwa ujumla.
Mhe. Simbachawene
ametoa maelekezo hayo leo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa
Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara wakati akifungua
Baraza hilo.
Amesema ujenzi wa
mfumo wa PEPMIS/PIPMIS pamoja na mifumo mingine ya TEHAMA ni utekelezaji wa maelekezo
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ambaye amedhamiria kwa dhati kuwa na Serikali ya kidijitali itakayorahisisha
utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mfumo
huu wa PEPMIS na PIPMIS ni mbadala wa Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji kazi
(OPRAS) na Mfumo wa Mikataba wa Utendaji Kazi wa Taasisi (IPCS) ulioonekana
kuwa na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi
zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS hivyo mfumo huu
umeboreshwa ili kuondokana na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi
kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mfumo huu muhimu,” Mhe. Simbachawene
amesisitiza.
Amesema mifumo hii ya TEHAMA ni nyenzo muhimu
katika kutekeleza majukumu na inalenga kuleta tija, ufanisi na kuchangia kwa
kiwango kikubwa katika maendeleo ya watumishi wa Umma na nchi kwa ujumla.
Amesema wanaotakiwa kuwajibishwa kwanza kwa
kushindwa kutekeleza zoezi hili la PEPMIS/PIPMIS ni viongozi ambao wameshindwa
kuwasimamia watumishi wao, hivyo hatua za kusimamisha mshahara zianze kwa viongozi
huku watumishi ambao hawajatekeleza wapewe muda wa kutekeleza na wakishindwa,
hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.
Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya Waajiri
kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi wanazoziongoza na
baadhi kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na Mamlaka kwani kwa
kufanya hivyo ni ukosefu wa maadili na ni jambo ambalo halikubaliki.
‘’Hili jambo sio sahihi kwenye Utumishi wa Umma
kwani kuna baadhi ya Waajiri wanaendesha ofisi za Umma kwa utashi na matakwa
binafsi’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene
Akitoa maelezo ya awali kuhusu baraza hilo, Katibu
Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema
elimu ya utekelezaji wa Mifumo ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa PEPMIS/PIPMIS na
Mfumo wa Kubaini Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR
Assessment) imetolewa nchi nzima lakini kumekuwa na kutowajibika kwa baadhi ya
viongozi katika kuwasimamia watumishi wao kutekeleza zoezi hilo.
Katibu Mkuu Mkomi amesema hatua zimeshaanza
kuchukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kwa wote ambao wameshindwa kutekeleza
zoezi hilo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa
Baraza, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma
Tanzania Bara, Bw. Joel Kaminyoge amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuboresha masilahi na stahiki za watumishi wa umma nchini kwani
malalamiko mengi ya watumishi ikiwemo kudai stahiki zao yamepungua kwa kiasi
kikubwa.
Amesema kufuatia maboresho makubwa aliyoyafanya
Mhe. Rais, jukumu walilo nalo sasa ni kuwahimiza watumishi wa umma kufanya kazi
kwa bidii na uadilifu ili kutoa huduma bora kwa umma kama ambavyo serikali
imekusudia.
Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma
Tanzania Bara lilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika
Utumishi wa Umma Sura 105.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika
Utumishi wa Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) alipokuwa akifungua Baraza hilo
leo mkoani Iringa.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa
Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) kabla ya Waziri Simbachawene kufungua Baraza
hilo leo mkoani Iringa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa maelezo kuhusu Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua Baraza hilo leo mkoani Iringa
Makamu
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara,
Bw. Joel Kaminyoge akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene baada
ya Waziri huyo kufungua Baraza Kuu la Tano la Wafanyakazi katika Utumishi wa
Umma Tanzania Bara leo mkoani Iringa
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza
Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara mara baada ya kufungua
Baraza hilo mkoani Iringa.
Tuesday, February 20, 2024
KATIBU MKUU-UTUMISHI AWATAKA MAAFISA RASILIMALIWATU KUWEKA KUMBUKUMBU SAHIHI ZA WATUMISHI KABLA YA KUSTAAFU I
Na. Lusungu
Helela-Dodoma
Tarehe 20 Februari,
2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amewataka
Maafisa Rasilimaliwatu wote serikalini kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi
za watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kabla ya miezi sita ili kuwaondolea
usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza
kwenye kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake, ikiwa ni mwendelezo
wa kuhimiza utendaji na uwajibikaji kwa
watumishi wa umma nchini.
Katibu Mkuu Mkomi amesema haikubaliki mtumishi anapewa barua ya
kustaafu huku baadhi ya taarifa za michango ya mafao yake haiko sawa.
‘’Mtumishi anapewa barua ya kumtaarifu kustaafu kabla ya miezi
sita halafu baadaye anaanza kusumbuliwa eti michango ya mafao haionekani, sasa
hiyo barua aliyopewa kabla ya miezi sita ilikuwa na maana gani" amehoji Bw.
Mkomi.
Amesisitiza kuwa suala hili lazima lifanyiwe kazi kwa kuwa
watumishi hao wanaostaafu wamelitumikia taifa kwa moyo hivyo kuhangaishwa sio
haki.
Katika hatua nyingine, Bw. Mkomi ametoa onyo kwa watumishi
wanaovujisha siri za serikali ambapo ameahidi wale wote watakaobainika watachukuliwa
hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Amesema kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya utumishi wa
umma ambapo ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi hao kujiepusha na tabia hiyo.
Pia, Katibu Mkuu Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia
maadili ya utendaji wanapotoa huduma kwa wananchi kwani maadili ndio msingi wa
utumishi wa umma.
Kwa kusisitiza hilo amewataka watumishi wa Ofisi yake kuwa mfano
wa uzingatiaji wa maadili kwa vile Ofisi hiyo ni kioo cha Utumishi wa umma
nchini.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa
Magufuli amemshukuru Katibu Mkuu Mkomi kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi
wa Ofisi yake licha ya majukumu mazito yanayomkabili huku akiahidi maagizo yote
aliyoyatoa yatatekelezwa.
Awali katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zilitolewa kwa
watumishi hao ikiwemo Maadili kwa Watumishi wa Umma, Kukabiliana
na Msongo wa Mawazo, PSSSF Kiganjani na faida ya kujiunga na SACCOS ya Ofisi ya
Rais-UTUMISHI.
Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na
watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na
watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akiteta na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu huyo na watumishi wa Ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma