Saturday, April 29, 2023

HAKIKISHENI MNAWASIMAMIA WATAALAM NA WATUMISHI KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI ILI WANANCHI WANUFAIKE - Mhe. Kairuki

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 29 Aprili, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki amewataka Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Mameneja na Maafisa wanaosimamia utawala na rasilimaliwatu katika taasisi za umma kuhakikisha wanawasimamia vema wataalam na watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya kimkakati ya Serilikali ili wananchi wanufaike na miradi hiyo kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali.

Mhe. Kairuki ametoa wito huo kwa wasimamizi wa utawala na rasilimaliwatu jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene.

Mhe. Kairuki amesema wataalamu hao wa utawala na rasilimaliwatu ndio wenye jukumu la kuhakikisha waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ya kimkakati, wanatekeleza miradi hiyo kwa wakati, uadilifu na kwa kuzingatia ubora ili iwe na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Mtakubaliana nami kwamba mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha wataalam wetu na watumishi wanaofanya kazi ya kutekeleza miradi mbalimbali wanaisimamia kwa uadilifu, ufanisi na weledi ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miradi ya kimkakati na maendeleo,” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Aidha, Mhe. Kairuki amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kuishauri Serikali kuhusiana na masuala ya usimamizi wa rasilimaliwatu ili kuwa na rasilimaliwatu itakayotoa mchango katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na maendeleo ya taifa.

Sanjari na hilo, Mhe. Kairuki amewataka wataalam hao wa utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu kutoka katika taasisi za umma nchini kutumia ujuzi na weledi wao kuishauri Serikali namna bora ya usimamizi wa rasilimaliwatu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi amesema, ofisi yake inatarajia mkutano huo wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania utaongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa wasimamizi hao wa masuala ya utawala na rasilimaliwatu nchini.

“Mkutano huu utakuwa na msaada mkubwa kwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika kuyatafutia ufumbuzi masuala mbalimbali ya kiutumishi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi na wadau wa taasisi zetu za umma,” Bw. Mkomi amefafanua.

Bw. Mkomi hakusita kuwataka Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Mameneja na Maafisa wanaosimamia utawala na rasilimaliwatu katika taasisi za umma kuhakikisha Makatibu Muhtasi wao kutojikweza na kuwa kikwazo kwa wananchi na wadau wanaofuata huduma katika ofisi zao.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania Bi. Leila Mavika amesema uongozi wake uliona ni vema kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania ambao ulikuwa haujafanyika kwa muda mrefu, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa masuala ya utawala na rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.

Bi. Mavika amesema jumla ya washiriki 281 kutoka katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Taasisi za Umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

 

Sehemu ya wataalam wa utawala na rasilimaliwatu katika taasisi za umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

 

 

 

Mwenyekiti wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) Bi. Leila Mavika akieleza lengo la mkutano wa 11 wa mwaka wa jumuia yake, kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki kuufunga mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

 


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Afisa Rasilimaliwatu Mkuu-Ofisi ya Mkemia Mkuu Bw. Mohammed Kanji, mara baada ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki akimsikiliza Afisa Rasilimaliwatu Mkuu-Ofisi ya Mkemia Mkuu Bw. Mohammed Kanji, mara baada ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa utawala na rasilimaliwatu, mara baada ya kuufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, Tawi ya Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.