Wednesday, April 19, 2023

MISINGI YA UTAWALA BORA NA USHIRIKISHWAJI KUIMARISHWA ILI KUWAWEZESHA WANANCHI KUPATA TAARIFA SAHIHI ZA MAAMUZI NA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA SERIKALI

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 19 Aprili, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema ofisi yake imejipanga kuhakikisha inaimarisha misingi ya utawala bora na ushirikishwaji, uwazi na uwajibikaji kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi za maamuzi na utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Mhe. Simbachawene amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hotuba kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24 ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mhe. Simbachawene amesema, ofisi yake itaimarisha pia mifumo ya mrejesho na utoaji wa huduma kwa wananchi ili Serikali itumie mrejesho huo kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi za umma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa, ofisi yake itahakikisha kunakuwa na utawala bora imara kuanzia katika ngazi ya uongozi hadi ngazi ya chini ili viongozi na watumishi wa umma nchini waweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Sanjari na hilo, Mhe. Simbachawene amesema kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/24 ofisi yake imelenga kuwa na utumishi wa umma unaotoa huduma bora kwa wakati kwa wananchi kwa kuzingatia Katiba ya nchi, Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa, dhamira ya ofisi yake ya kuimarisha utawala bora inaunga mkono kwa vitendo hotuba aliyoitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 21 Aprili 2021 wakati akilihutubia Bunge ambapo alimnukuu “Tutawapima viongozi na watumishi kwa namna wanavyotimiza majukumu yao, hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, tutaendeleza juhudi za kupambana na rushwa.

Aidha, Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa, kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24, Serikali itatoa kipaumbele katika usimamizi wa rasilimaliwatu na rasilimalifedha, itapandisha vyeo watumishi wa umma na kuwabadilisha kada, kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara na kuajiri watumishi wa umma wenye sifa watakaotoa huduma bora kwa wananchi.














 

 

 

No comments:

Post a Comment