Saturday, April 1, 2023

MHE. JENISTA AELEKEZA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUPATIWATAARIFA YA FEDHA ZINAZOPOKELEWA KUTEKELEZA MIRADI YA TASAF ILI WAISIMAMIE

 

Na. James K. Mwanamyoto-Mkuranga

Tarehe 01 Aprili, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka waratibu wa TASAF wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanawapatia taarifa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhusu kiasi cha fedha kinachopokelewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya TASAF, ili kuwawezesha viongozi hao kusimamia vema na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo katika maeneo yao ya Utawala.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo akiwa wilayani Mkuranga, wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.

Mhe. Jenista amesema, imekuwa ikitokea mara nyingi fedha za kutekeleza miradi ya TASAF zinawasilishwa katika Mikoa na Wilaya lakini Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakuwa hawana taarifa rasmi, hivyo ni jukumu la waratibu wa TASAF katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuwajulisha viongozi hao.

“Naendelea kuelekeza kila fedha ya TASAF inapopokelewa mkoani au wilayani, ni lazima Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wapewe taarifa zinazoanisha kiasi cha fedha kilichopokelewa ili iwe rahisi kwa viongozi hao kutekeleza jukumu la kuisimamia na kuifuatilia miradi yote ya TASAF,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, miradi yote ya TASAF inatakiwa kukamilika kwa wakati kama ambavyo miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inavyokamilika kwa wakati.

Aidha, Mhe. Jenista amevipongeza vikundi vya Walengwa wa TASAF wilayani Mkuranga baada ya kujionea bidhaa mbalimbali wanazozizalisha kwa kujishughulisha na ujasiriamali kwa lengo la kujiongezea kipato kitakachoboresha maisha yao.

Sanjari na hilo, Mhe. Jenista ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Mkuranga kwa kuamua kusimamia uanzishaji wa vikundi vya TASAF katika kila kata ili wananchi wanufaike na fedha za TASAF ikiwa ni pamoja na mikopo ya Halmashauri inayotolewa kwa wanachi walio katika vikundi.

“Sote ni mashaidi hapa, tumeona vikundi hivi vya walengwa wa TASAF namna vilivyozalisha mikeka, unga wa muhugo, batiki na fagio hivyo vimekuwa ni mfano bora wa kuigwa na wananchi na vikundi vingine nchini,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Ali amesema akina mama waliounda vikundi vya TASAF katika wilaya yake wamekuwa mstali wa mbele katika kuhakikisha watumia vema ruzuku wanayoipata kuendesha miradi waliyoibuni kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Khadija amesema, miradi mingi ambayo akina mama wilayani kwake wameiibua itaendelea kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa ndani ya wilaya ya Mkuranga, akitoa mfano wa uzalishaji wa unga wa muhogo, fagio na mikeka ambao unaendana na dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.

Naye, Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu, Bi. Halima Mtulia amesema TASAF imewawesha kupata mafunzo ya kutengeneza fagio za chelewa ambayo yameongeza thamani ya zao la minazi na kuongeza kuwa, kikundi chao kimepata eneo la kufanyia shughuli za biashara pamoja na kumpata mfadhili wa kujenga eneo maalum la kufanyia biashara.

Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja Wilayani Mkuranga, iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ambao unaratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho.

 

 

 

Sehemu ya walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokitembelea kijiji hicho kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani Mkuranga. Mbele ya walengwa hao ni bidhaa wanazozizalisha.


Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Ali akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo iliyolenga kukagua miradi ya TASAF wilayani humo.

 

Sehemu ya walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Khadija Ali wakati akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji hicho, wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo iliyolenga kukagua miradi ya TASAF wilayani humo.

 

Katibu wa Kikundi cha Umoja ni Nguvu, Bi. Halima Mtulia akitoa taarifa ya maendeleo ya kikundi chao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo katika Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, iliyolenga kukagua utekelezaji miradi ya TASAF.

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkuranga Bi. Safina Msemo, wakati akimfafanulia kuhusu bidhaa zinazozalishwa na walengwa wa TASAF walio katika vikundi vilivyopo Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 kwa Kikundi cha Umoja ni Nguvu kilichopo Kijiji cha Kiparang’anda, ikiwa ni mkopo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wenye lengo la kukiwezesha kikundi hicho kufanya shughuli za kiuchumi.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipokea zawadi kutoka kwa walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Kiparang’anda wilayani Mkuranga, ambazo ni bidhaa wanazozizalisha kupitia vikundi vyao.

 


 

 

No comments:

Post a Comment