Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 26 Aprili, 2023
Watumishi watatu waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2023 wamekiri kuwa, kitendo cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kujali na kusimamia stahiki na maslahi ya watumishi wa umma nchini kimewamotisha kufanya kazi kwa bidii na hatimaye kuchaguliwa kuwa wafanyakazi bora wa ofisi hiyo.
Mmoja wa watumishi hao ambaye ni Afisa Utumishi Bi. Frida Byakuzana aliyeshika nafasi ya tatu amesema, ufanyakazi bora alioupata umechagizwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kujali maslahi ya watumishi wa umma kwa kuwapandisha madaraja, kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara, kuboresha posho ya kufanya kazi katika muda wa ziada pamoja na posho ya safari za ndani ya nchi.
“Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma nchini kimekuwa ni chachu kwangu ya kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Sita la kutoa huduma bora kwa wananchi,” Bi. Byakuzana amefafanua.
Bi. Byakuzana ametoa wito kwa watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ikiwa ni sehemu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani amekuwa mstari wa mbele kusimamia maslahi ya watumishi wa umma kwa lengo la kujenga ari na morali ya watumishi wa umma katika kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi Bw. Juma Senzota aliyeshika nafasi ya pili ameahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa watumishi wa umma wanaofuata huduma katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI akiamini kuwa kitendo hicho kitawajengea morali watumishi hao kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi na hatimaye kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuliletea taifa maendeleo.
Bw. Senzota hakusita kuwashukuru watumishi wenzie kwa kumchagua kuwa miongoni mwa watumishi watatu bora wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuongeza kuwa, kitendo hicho hakimaanishi kuwa wao si watumishi bora kiutendaji kwani amekuwa akishirikiana nao katika kuwahudumia wananchi na watumishi wa umma wanaofuata huduma katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Naye, mfanyakazi bora aliyeshika nafasi ya kwanza Bi. Zainabu Waziri mwenye cheo cha Msaidizi wa Ofisi ambae anakaribia kustaafu ameahidi kuwa katika kipindi cha utumishi wa wake kilichosalia ataendelea kutoa huduma bora kwa wateja wanaofuata huduma Ofisi ya Rais-UTUMISHI ili kujenga taswira nzuri ya ofisi kwa umma.
Akipongeza utendaji kazi Bi. Zainabu Waziri anaetarajia kustaafu Julai, 2023 akiwa mfanyakazi bora wa ofisi, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi amesema watumishi wengine wanapaswa kujifunza mambo ya msingi kutoka kwa mtumishi huyo bila kujali nafasi anayostaafu nayo kwani amekuwa ni mtumishi mwadilifu na mchapa kazi katika kipindi chote cha utumishi wake.
“Nakupongeza Bi. Zainabu kwa utendaji kazi wako mzuri na niwaombe watu wa idara ya utawala ukifika wakati wa kumpatia zawadi apewe kwa wakati,” Bw. Daudi amesisitiza.
Aidha, Bw. Daudi
ametumia fursa hiyo kuwahamasisha watumishi wote wa ofisi yake ambao
hawakubahatika kuwa wafanyakazi bora kwa mwaka huu, kujipanga na kuendelea
kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili mwakani waweze kuchaguliwa kuwa
wafanyakazi bora.
Mfanyakazi bora
wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Zainabu
Waziri akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, mara baada ya kuchaguliwa
kuwa mfanyakazi bora wa ofisi hiyo kwa mwaka 2023.
Mfanyakazi bora
aliyeshika nafasi ya pili Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bw. Juma Senzoka akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na
maarifa, mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kwa mwaka 2023.
Mfanyakazi bora
aliyeshika nafasi ya tatu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bi. Frida Byakuzana akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na
weledi, mara baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo kwa mwaka 2023.
Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier
Daudi akiongoza kikao cha kuchagua wafanyakazi bora wa ofisi yake.
Mkurugenzi wa
Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Mussa Magufuli akitoa mwogozo wa vigezo vitakavyotumika
kumchagua mfanyakazi bora kabla ya watumishi wa ofisi yake kumchagua mfanyakazi
bora wa ofisi hiyo kwa mwaka 2023.
Baadhi ya
watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya
Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Bw. Mussa Magufuli wakati akifafanua vigezo vya
kumchagua mfanyakazi bora wa ofisi hiyo kwa mwaka 2023.
Sehemu ya
watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakipiga
kura kumchagua mfanyakazi bora wa ofisi hiyo kwa mwaka 2023.
Sehemu ya
watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
wakikamiliza zoezi la kupiga kura kumchagua mfanyakazi bora wa ofisi hiyo kwa
mwaka 2023.
Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier
Daudi (wa kwanza kulia) akishuhudia zoezi la kuhesabu kura za kumpata
mfanyakazi bora wa ofisi yake kwa mwaka 2023.
No comments:
Post a Comment