Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro
Tarehe 15 Machi, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameiahidi Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kupitia TASAF kujenga wodi ya
kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati ya Kijiji cha Mkambarani
ili wananchi wa kijiji hicho wapate huduma bora za afya.
Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni utekelezaji
wa maelekezo ya kamati hiyo ya kudumu iliyoelekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) kujenga jengo la kina mama kwa ajili ya kuwapatia huduma stahiki, ikiwa
ni pamoja na kujenga maabara itakayotoa huduma bora ya vipimo kwa wananchi wa Kijiji
cha Mkambarani.
Mhe. Ndejembi amesema, kutokana na maelekezo
yaliyotolewa na kamati ofisi yake itajenga wodi ya akina mama ili kuwe na
faragha wakati wa kuwahudumia akina mama wajawazito.
Kuhusu maelekezo ya ujenzi wa maabara, Mhe. Ndejembi
ameihakikishia kamati na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani kujenga maabara ili
kuwaondolea adha wananchi hao ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya
maabara ambapo pia hulazimika kuingia gharama kubwa.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, lengo la
Serikali kujenga zahanati ya Mkambarani ni kuwasogezea karibu huduma za afya
wananchi wa eneo hilo ikizingatiwa kuwa, walengwa wa TASAF watanufaika pia na
huduma zinazotolewa na zahanati hiyo na hatimaye kuwa na afya bora
itakayowawezesha kupambana na umaskini kupitia ruzuku ya TASAF wanayoipata.
Awali, akitoa maelekezo kwa Serikali kwa niaba
ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) amesema Kamati imelazimika kutoa
maelekezo ya ujenzi wa Wodi ya akina mama na maabara kama sehemu ya kulinda utu
wa wananchi hususani akina mama wanaofuata huduma ya uzazi katika zahanati ya
Mkambarani.
Mhe. Polepole amesema, wodi ya akina mama
ikijengwa itaongeza usiri na faragha wakati wa kuwahudumia wajawazito tofauti
la ilivyo sasa ambapo hakuna usiri wa kutosha wala faragha pindi akina mama
wanapohudumiwa.
Kuhusiana na maelekezo ya ujenzi wa maabara,
Mhe. Polepole ameeleza kuwa, kamati yake imepata fursa ya kuitembelea zahanati
ya Mkambarani na kubaini kuwa hakuna maabara inayokidhi mahitaji ndio maana
kamati yake imeielekeza Serikali kujenga maabara itakayokidhi kutoa huduma
stahiki kwa wananchi wa Kijiji cha Mkambarani.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa imemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Dar es Salaam, Pwani
na Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi
zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akitoa maelekezo kwa Serikali kuhusu
ujenzi wa wodi ya kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati
ya Kijiji cha Mkambarani.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani-Morogoro wakimsikiliza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe.
Humphrey Polepole (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kijijini hapo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali
za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) na baadhi ya wajumbe wa kamati yake
pamoja na watendaji wa Serikali wakikagua zahanati ya Mkambarani wakati wa
ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF kijijini hapo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kuhusu utekelezaji wa
maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati
wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF katika Kijiji cha Mkambarani - Morogoro.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF wa Kijiji cha Mkambarani Mzee
Abdallah J. Kinyaku akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na TASAF kwa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya
kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mpiradi ya TASAF kijijini hapo.
No comments:
Post a Comment